← Proverbs (7/31) → |
1. | Mwanangu, yashike maneno yangu, Na kuziweka amri zangu akiba kwako. |
2. | Uzishike amri zangu ukaishi, Na sheria yangu kama mboni ya jicho lako. |
3. | Zifunge katika vidole vyako; Ziandike juu ya kibao cha moyo wako. |
4. | Mwambie hekima, Wewe ndiwe umbu langu; Mwite ufahamu jamaa yako mwanamke. |
5. | Wapate kukulinda na malaya, Na mgeni akubembelezaye kwa maneno yake. |
6. | Maana katika dirisha la nyumba yangu Nalichungulia katika shubaka yake; |
7. | Nikaona katikati ya wajinga, Nikamtambua miongoni mwa vijana, Kijana mmoja asiyekuwa na akili, |
8. | Akipita njiani karibu na pembe yake, Akiishika njia iendayo nyumbani kwake, |
9. | Wakati wa magharibi, wakati wa jioni, Usiku wa manane, gizani. |
10. | Na tazama, mwanamke akamkuta, Ana mavazi ya kikahaba, mwerevu wa moyo; |
11. | Ana kelele, na ukaidi; Miguu yake haikai nyumbani mwake. |
12. | Mara yu katika njia kuu, mara viwanjani, Naye huotea kwenye pembe za kila njia. |
13. | Basi akamshika, akambusu, Akamwambia kwa uso usio na haya, |
14. | Kwangu ziko sadaka za amani; Leo hivi nimeziondoa nadhiri zangu; |
15. | Ndiyo maana nikatoka nikulaki, Nikutafute uso wako kwa bidii, nami nimekuona. |
16. | Nimetandika kitanda changu, magodoro mazuri, Kwa matandiko ya Kimisri yenye mistari. |
17. | Nimetia kitanda changu manukato, Manemane na udi na mdalasini. |
18. | Haya, na tushibe upendo hata asubuhi, Tujifurahishe nafsi zetu kwa mahaba. |
19. | Maana mume wangu hayumo nyumbani, Amekwenda safari ya mbali; |
20. | Amechukua mfuko wa fedha mkononi; Atarudi wakati wa mwezi mpevu. |
21. | Kwa maneno yake mengi na ulaini akamshawishi, Kwa ubembelezi wa midomo yake akamshinda. |
22. | Huyo akafuatana naye mara hiyo, Kama vile ng'ombe aendavyo machinjoni; Au mpumbavu kuadhibiwa katika pingu; |
23. | Hata mshale umchome maini; Kama ndege aendaye haraka mtegoni; Wala hajui ya kuwa ni hasara ya nafsi yake. |
24. | Basi, wanangu, nisikilizeni sasa, Mkayaangalie maneno ya kinywa changu. |
25. | Moyo wako usizielekee njia zake, Wala usipotee katika mapito yake. |
26. | Maana amewaangusha wengi waliojeruhi, Naam, jumla ya waliouawa naye ni jeshi kubwa. |
27. | Nyumba yake ni njia ya kwenda kuzimu, Hushuka mpaka vyumba vya mauti. |
← Proverbs (7/31) → |