| ← Proverbs (6/31) → |
| 1. | Mwanangu, kama umekuwa mdhamini wa rafiki yako, Ikiwa wewe na mgeni mmepana mikono, |
| 2. | Basi umetegwa kwa maneno ya kinywa chako, Umekamatwa kwa maneno ya kinywa chako, |
| 3. | Sasa, mwanangu, fanya hivi ukajiokoe, Kwa kuwa umejitia mkononi mwa jirani yako; Nenda ukanyenyekee, na kumsihi jirani yako. |
| 4. | Usiache macho yako kupata usingizi, Wala kope za macho yako kusinzia. |
| 5. | Ujiponye kama paa na mkono wa mwindaji, Na kama ndege katika mkono wa mtega mitego. |
| 6. | Ewe mvivu, mwendee chungu, Zitafakari njia zake ukapate hekima. |
| 7. | Kwa maana yeye hana akida, Wala msimamizi, wala mkuu, |
| 8. | Lakini hujiwekea akiba ya chakula wakati wa jua; Hukusanya chakula chake wakati wa mavuno. |
| 9. | Ewe mvivu, utalala hata lini? Utaondoka lini katika usingizi wako? |
| 10. | Bado kulala kidogo, kusinzia kidogo, Bado kukunja mikono upate usingizi! |
| 11. | Hivyo umaskini wako huja kama mnyang'anyi, Na uhitaji wako kama mtu mwenye silaha. |
| 12. | Mtu asiyefaa kitu, mtu wa uovu; Huenda njiani mwenye kinywa cha upotofu. |
| 13. | Hukonyeza kwa macho, hunena kwa miguu, Huwaashiria watu kwa vidole vyake. |
| 14. | Mna upotofu moyoni mwake, hutunga uovu daima, Hupanda mbegu za magomvi. |
| 15. | Basi msiba utampata kwa ghafula; Ghafula atavunjika, bila njia ya kupona. |
| 16. | Kuna vitu sita anavyovichukia Bwana; Naam, viko saba vilivyo chukizo kwake. |
| 17. | Macho ya kiburi, ulimi wa uongo, Na mikono imwagayo damu isiyo na hatia; |
| 18. | Moyo uwazao mawazo mabaya; Miguu iliyo myepesi kukimbilia maovu; |
| 19. | Shahidi wa uongo asemaye uongo; Naye apandaye mbegu za fitina kati ya ndugu. |
| 20. | Mwanangu, shika maagizo ya baba yako, Wala usiiache sheria ya mama yako. |
| 21. | Yafunge hayo katika moyo wako daima; Jivike hayo shingoni mwako. |
| 22. | Uendapo yatakuongoza, ulalapo yatakulinda, Na uamkapo yatazungumza nawe. |
| 23. | Maana maagizo hayo ni taa, na sheria hiyo ni nuru, Na maonyo ya kumwadilisha mtu ni njia ya uzima. |
| 24. | Yakulinde na mwanamke mwovu, asikupate, Na kukuponya na ubembelezi wa mgeni. |
| 25. | Usiutamani uzuri wake moyoni mwako; Wala usikubali akunase kwa kope za macho yake. |
| 26. | Maana kwa malaya mtu hutiwa katika hali ya kuhitaji kipande cha mkate; Na kahaba humwinda mtu anase nafsi yake iliyo ya thamani |
| 27. | Je! Mtu aweza kuua moto kifuani pake, Na nguo zake zisiteketezwe? |
| 28. | Je! Mtu aweza kukanyaga makaa ya moto, Na nyayo zake zisiungue? |
| 29. | Ndivyo alivyo aingiaye kwa mke wa jirani yake; Kila mtu amgusaye huyo atakuwa na hatia. |
| 30. | Watu hawamdharau mwivi, Akiiba ili kujishibisha, iwapo aona njaa; |
| 31. | Lakini akipatikana, atalipa mara saba; Atatoa mali yote ya nyumba yake. |
| 32. | Mtu aziniye na mwanamke hana akili kabisa; Afanya jambo litakalomwangamiza nafsi yake. |
| 33. | Atapata jeraha na kuvunjiwa heshima; Wala fedheha yake haitafutika. |
| 34. | Maana wivu ni ghadhabu ya mtu; Wala hatahurumia siku ya kujilipiza kisasi. |
| 35. | Hatakubali ukombozi uwao wote; Wala hatakuwa radhi, ujapomlipa vitu vingi. |
| ← Proverbs (6/31) → |