← Proverbs (5/31) → |
1. | Mwanangu, sikiliza hekima yangu; Tega sikio lako, mzisikie akili zangu; |
2. | Upate kuilinda busara, Na midomo yako iyahifadhi maarifa. |
3. | Maana midomo ya malaya hudondoza asali, Na kinywa chake ni laini kuliko mafuta; |
4. | Lakini mwisho wake ni mchungu kuliko pakanga; Ni mkali kama upanga wa makali kuwili. |
5. | Miguu yake inatelemkia mauti; Hatua zake zinashikamana na kuzimu; |
6. | Hata asiweze kuiona njia sawa ya uzima; Njia zake ni za kutanga-tanga wala hana habari. |
7. | Basi, wanangu, nisikilizeni sasa, Wala msiache maneno ya kinywa changu. |
8. | Itenge njia yako mbali naye, Wala usiukaribie mlango wa nyumba yake. |
9. | Usije ukawapa wengine heshima yako, Na wakorofi miaka yako; |
10. | Wageni wasije wakashiba nguvu zako; Kazi zako zikawa ndani ya nyumba ya mgeni; |
11. | Nawe ukaziombolea siku zako za mwisho, Nyama yako na mwili wako utakapoangamia; |
12. | Ukasema, Jinsi nilivyochukia maonyo, Na moyo wangu ukadharau kukemewa; |
13. | Wala sikuisikia sauti ya waalimu wangu, Wala sikuwategea sikio langu walionifundisha! |
14. | Nalikuwa karibu na kuingia katika maovu yote, Katikati ya mkutano na kusanyiko. |
15. | Unywe maji ya birika lako mwenyewe, Na maji yenye kububujika katika kisima chako. |
16. | Je! Chemchemi zako zitawanyike mbali, Na mito ya maji katika njia kuu? |
17. | Yawe yako mwenyewe peke yako, Wala si ya wageni pamoja nawe. |
18. | Chemchemi yako ibarikiwe; Nawe umfurahie mke wa ujana wako. |
19. | Ni ayala apendaye na paa apendezaye; Maziwa yake yakutoshe sikuzote; Na kwa upendo wake ushangilie daima. |
20. | Mwanangu! Mbona unashangilia malaya, Na kukikumbatia kifua cha mgeni? |
21. | Kwa maana njia za mwanadamu zi mbele za macho ya Bwana, Na mienendo yake yote huitafakari. |
22. | Maovu yake yeye yatampata mdhalimu, Naye atashikwa kwa kamba za dhambi zake. |
23. | Atakufa huyo kwa kukosa maonyo, Naye atapotea kwa wingi wa ujinga wake. |
← Proverbs (5/31) → |