← Proverbs (31/31) |
1. | Maneno ya mfalme Lemueli; mausia aliyofundishwa na mama yake. |
2. | Ni nini, mwanangu? Tena ni nini, mwana wa tumbo langu? Tena, ni nini mwana wa nadhiri zangu? |
3. | Usiwape wanawake nguvu zako; Wala moyo wako usiwape wale wawaharibuo wafalme. |
4. | Ee Lemueli, kunywa mvinyo hakuwafai wafalme, hakuwafai wafalme; Wala haifai wakuu waseme, Ki wapi kileo? |
5. | Wasije wakanywa na kuisahau sheria, Na kuipotosha hukumu ya mtu aliye taabuni. |
6. | Mpe kileo yeye aliye karibu na kupotea; Kampe divai yeye aliye na uchungu nafsini. |
7. | Anywe akausahau umaskini wake; Asiikumbuke tena taabu yake. |
8. | Fumbua kinywa chako kwa ajili yake aliye bubu; Uwatetee watu wote walioachwa peke yao; |
9. | Fumbua kinywa chako, uhukumu kwa haki; Uwapatie maskini na wahitaji haki yao. |
10. | Mke mwema, ni nani awezaye kumwona? Maana kima chake chapita kima cha marijani. |
11. | Moyo wa mumewe humwamini, Wala hatakosa kupata mapato. |
12. | Humtendea mema wala si mabaya, Siku zote za maisha yake. |
13. | Hutafuta sufu na kitani; Hufanya kazi yake ya mikono kwa moyo. |
14. | Afanana na merikebu za biashara; Huleta chakula chake kutoka mbali. |
15. | Tena huamka, kabla haujaisha usiku; Huwapa watu wa nyumbani mwake chakula; Na wajakazi wake sehemu zao. |
16. | Huangalia shamba, akalinunua; Kwa mapato ya mikono yake hupanda mizabibu. |
17. | Hujifunga nguvu viunoni kama mshipi; Hutia mikono yake nguvu. |
18. | Huona kama bidhaa yake ina faida; Taa yake haizimiki usiku. |
19. | Hutia mikono yake katika kusokota; Na mikono yake huishika pia. |
20. | Huwakunjulia maskini mikono yake; Naam, huwanyoshea wahitaji mikono yake. |
21. | Hawahofii theluji watu wa nyumbani mwake; Maana wote wa nyumbani mwake huvikwa nguo nyekundu. |
22. | Hujifanyia mazulia ya urembo; Mavazi yake ni kitani safi na urujuani. |
23. | Mume wake hujulikana malangoni; Aketipo pamoja na wazee wa nchi. |
24. | Hufanya nguo za kitani na kuziuza; Huwapa wafanya biashara mishipi. |
25. | Nguvu na hadhi ndiyo mavazi yake; Anaucheka wakati ujao. |
26. | Hufumbua kinywa chake kwa hekima, Na sheria ya wema i katika ulimi wake. |
27. | Huangalia sana njia za watu wa nyumbani mwake; Wala hali chakula cha uvivu. |
28. | Wanawe huondoka na kumwita heri; Mumewe naye humsifu, na kusema, |
29. | Binti za watu wengi wamefanya mema, Lakini wewe umewapita wote. |
30. | Upendeleo hudanganya, na uzuri ni ubatili; Bali mwanamke amchaye Bwana, ndiye atakayesifiwa. |
31. | Mpe mapato ya mikono yake, Na matendo yake yamsifu malangoni. |
← Proverbs (31/31) |