Proverbs (3/31)  

1. Mwanangu, usiisahau sheria yangu, Bali moyo wako uzishike amri zangu.
2. Maana zitakuongezea wingi wa siku. Na miaka ya uzima, na amani.
3. Rehema na kweli zisifarakane nawe; Zifunge shingoni mwako; Ziandike juu ya kibao cha moyo wako.
4. Ndivyo utakavyopata kibali na akili nzuri, Mbele za Mungu na mbele ya mwanadamu.
5. Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe;
6. Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako.
7. Usiwe mwenye hekima machoni pako; Mche Bwana, ukajiepushe na uovu.
8. Itakuwa afya mwilini pako,
9. Mheshimu Bwana kwa mali yako, Na kwa malimbuko ya mazao yako yote.
10. Ndipo ghala zako zitakapojazwa kwa wingi, Na mashinikizo yako yatafurika divai mpya.
11. Mwanangu, usidharau kuadhibiwa na Bwana, Wala usione ni taabu kurudiwa naye.
12. Kwa kuwa Bwana ampendaye humrudi, Kama vile baba mwanawe ampendezaye.
13. Heri mtu yule aonaye hekima, Na mtu yule apataye ufahamu.
14. Maana biashara yake ni bora kuliko biashara ya fedha, Na faida yake ni nyingi kuliko dhahabu safi.
15. Yeye ana thamani kuliko marijani, Wala vyote uvitamanivyo havilingani naye.
16. Ana wingi wa siku katika mkono wake wa kuume, Utajiri na heshima katika mkono wake wa kushoto.
17. Njia zake ni njia za kupendeza sana, Na mapito yake yote ni amani.
18. Yeye ni mti wa uzima kwao wamshikao sana; Ana heri kila mtu ashikamanaye naye.
19. Kwa hekima Bwana aliiweka misingi ya nchi; Kwa akili zake akazifanya mbingu imara;
20. Kwa maarifa yake vilindi viligawanyika; Na mawingu yadondoza umande.
21. Mwanangu, yasiondoke haya machoni pako, Shika hekima kamili na busara.
22. Basi yatakuwa uzima kwa nafsi yako, Na neema shingoni mwako.
23. Ndipo utakapokwenda katika njia yako salama, Wala mguu wako hautakwaa.
24. Ulalapo hutaona hofu; Naam, utalala na usingizi wako utakuwa mtamu.
25. Usiogope hofu ya ghafula, Wala uharibifu wa waovu utakapofika.
26. Kwa kuwa Bwana atakuwa tumaini lako, Naye atakulinda mguu wako usinaswe.
27. Usiwanyime watu mema yaliyo haki yao, Ikiwa katika uwezo wa mkono wako kuyatenda.
28. Usimwambie jirani yako, Nenda, urudi halafu, na kesho nitakupa; Nawe unacho kitu kile karibu nawe.
29. Usiwaze mabaya juu ya jirani yako, Ambaye anakaa karibu nawe na kujiona salama.
30. Usishindane na mtu bila sababu, Ikiwa hakukudhuru kwa lo lote.
31. Usimhusudu mtu mwenye jeuri, Wala usiichague mojawapo ya njia zake.
32. Maana mtu mkaidi ni chukizo kwa Bwana, Bali siri yake ni pamoja na wanyofu.
33. Laana ya Bwana i katika nyumba ya waovu, Bali huibariki maskani ya mwenye haki.
34. Hakika yake huwadharau wenye dharau, Bali huwapa wanyenyekevu neema.
35. Wenye hekima wataurithi utukufu, Bali kukuzwa kwa wapumbavu ni fedheha.

  Proverbs (3/31)