← Proverbs (29/31) → |
1. | Aonywaye mara nyingi akishupaza shingo, Atavunjika ghafula, wala hapati dawa. |
2. | Wenye haki wakiwa na amri, watu hufurahi; Bali mwovu atawalapo, watu huugua. |
3. | Apendaye hekima humfurahisha babaye; Bali ashikamanaye na makahaba hutapanya mali. |
4. | Mfalme huithibitisha nchi kwa hukumu; Bali yeye apokeaye rushwa huipindua. |
5. | Mwenye kujipendekeza kwa jirani yake, Hutandika wavu ili kuitega miguu yake. |
6. | Kuna mtego katika kosa la mtu mbaya; Bali mwenye haki huimba na kufurahi. |
7. | Mwenye haki huyaangalia madai ya maskini; Bali mtu mbaya hana ufahamu hata ayajue. |
8. | Watu wenye dharau huwasha mji moto; Bali wenye hekima hugeuzia mbali ghadhabu. |
9. | Mwenye hekima akijadiliana na mpumbavu; Akikasirika au akicheka, pia hapana raha. |
10. | Wamwagao damu humchukia mtu mkamilifu; Bali wenye haki humtunza nafsi yake. |
11. | Mpumbavu hudhihirisha hasira yake yote; Bali mwenye hekima huizuia na kuituliza. |
12. | Mwenye kutawala akisikiliza uongo; Basi watumishi wake wote watakuwa waovu. |
13. | Maskini na mdhalimu hukutana pamoja; Bwana huwatia nuru macho yao wote wawili. |
14. | Mfalme awahukumuye maskini kwa uaminifu; Kiti chake cha enzi kitathibitika milele. |
15. | Fimbo na maonyo hutia hekima; Bali mwana aliyeachiliwa humwaibisha mamaye. |
16. | Waovu wakiongezeka, maasi huongezeka; Bali wenye haki watayatazama maanguko yao. |
17. | Mrudi mwanao naye atakustarehesha; Naam, atakufurahisha nafsi yako. |
18. | Pasipo maono, watu huacha kujizuia; Bali ana heri mtu yule aishikaye sheria. |
19. | Haitoshi mtumwa kuonywa kwa maneno; Maana ajapoyafahamu hataitika. |
20. | Je! Umemwona mtu mwenye kuhamaki katika maneno? Afadhali kumtumaini mpumbavu kuliko yeye. |
21. | Amtunduiaye mtumwa wake tangu utoto, Mwisho wake atakuwa ni mwanawe. |
22. | Mtu wa hasira huchochea ugomvi; Na mtu mwenye ghadhabu huasi sana. |
23. | Kiburi cha mtu kitamshusha; Bali mwenye roho ya unyenyekevu ataheshimiwa. |
24. | Mshiriki wa mwivi huichukia nafsi yake mwenyewe; Asikia maapizo, wala hana neno. |
25. | Kuwaogopa wanadamu huleta mtego; Bali amtumainiye Bwana atakuwa salama. |
26. | Watu wengi hutafuta upendeleo wa mkuu; Bali hukumu ya kila mtu hutoka kwa Bwana |
27. | Mtu aliye dhalimu ni chukizo kwa wenye haki; Na mnyofu wa mwenendo ni chukizo kwa waovu. |
← Proverbs (29/31) → |