Proverbs (28/31)  

1. Waovu hukimbia wasipofuatiwa na mtu; Bali wenye haki ni wajasiri kama simba.
2. Kwa sababu ya maasi ya nchi wakuu wake huwa wengi; Bali kwa wenye ufahamu na maarifa hali ya nchi hudumishwa
3. Mtu mhitaji awaoneaye maskini, Ni kama mvua ya dhoruba isiyosaza chakula.
4. Wao waiachao sheria huwasifu waovu; Bali wao waishikao hushindana nao.
5. Watu wabaya hawaelewi na hukumu; Bali wamtafutao Bwana huelewa na yote.
6. Afadhali maskini aendaye katika unyofu wake, Kuliko mpotofu wa njia angawa ni tajiri.
7. Yeye aishikaye sheria ni mwana mwenye hekima; Bali aliye rafiki wa walafi humwaibisha babaye.
8. Yeye azidishaye mali yake kwa riba na faida, Humkusanyia mtu awahurumiaye maskini.
9. Yeye aligeuzaye sikio lake asiisikie sheria, Hata sala yake ni chukizo.
10. Kila mtu awapotezaye wenye haki katika njia mbaya, Ataanguka katika rima lake mwenyewe; Bali wakamilifu watarithi mema.
11. Mtu tajiri ana hekima machoni pake mwenyewe; Bali maskini mwenye ufahamu humchunguza sana.
12. Wenye haki washindapo, uko utukufu mwingi; Bali waovu waondokapo, watu hujificha.
13. Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema.
14. Mwanadamu mwenye kicho yu heri sikuzote; Bali mshupavu wa moyo ataangukia madhara.
15. Kama simba angurumaye, na dubu mwenye njaa; Ndivyo alivyo mtu mbaya awatawalaye maskini.
16. Mkuu aliyepungukiwa na akili huwaonea watu sana; Bali achukiaye kutamani ataongeza siku zake.
17. Aliyelemewa na damu ya mtu Atalikimbilia shimo; wala mtu asimzuie.
18. Aendaye kwa unyofu ataokolewa; Bali mkaidi wa njia zake ataanguka mara.
19. Alimaye shamba lake atakuwa na chakula tele; Bali afuataye mambo ya upuzi atapata umaskini wa kumtosha.
20. Mtu mwaminifu atakuwa na baraka tele; Lakini afanyaye haraka kuwa tajiri hakosi ataadhibiwa.
21. Kupendelea watu si kwema; Wala mtu kuasi kwa ajili ya kipande cha mkate.
22. Mwenye husuda afanya haraka kuwa tajiri; Wala haufikiri uhitaji utakaomjilia.
23. Amkemeaye mwenzake hatimaye atapata kibali; Zaidi ya mtu ajipendekezaye kwa ulimi wake.
24. Aibaye mali ya babaye au mamaye, na kusema, Si kosa; Mwana huyo ni rafiki wa mtu mharibifu.
25. Mwenye nafsi ya kutamani huchochea fitina; Bali amtumainiye Bwana atawandishwa.
26. Mwenye kujitumainia moyo wake ni mjinga; Bali yeye aendaye kwa busara ataokolewa.
27. Mwenye kuwagawia maskini hatahitaji kitu; Bali afichaye macho yake atakuwa na laana nyingi.
28. Wasio haki wainukapo, wanadamu hujificha; Bali waangamiapo, wenye haki huongezeka.

  Proverbs (28/31)