| ← Proverbs (27/31) → |
| 1. | Usijisifu kwa ajili ya kesho; Kwa maana hujui yatakayozaliwa na siku moja. |
| 2. | Mwingine na akusifu wala si kinywa chako mwenyewe; Mtu mgeni wala si midomo yako wewe. |
| 3. | Jiwe ni zito, na mchanga hulemea; Lakini ghadhabu ya mpumbavu ni nzito kuliko hivi vyote viwili. |
| 4. | Ghadhabu ni kali, na hasira ni gharika; Lakini ni nani awezaye kusimama mbele ya wivu. |
| 5. | Lawama ya wazi ni heri, Kuliko upendo uliositirika. |
| 6. | Jeraha utiwazo na rafiki ni amini; Bali kubusu kwa adui ni kwingi sana. |
| 7. | Nafsi iliyoshiba hukinai sega la asali; Bali nafsi yenye njaa huona kila kitu kichungu kuwa kitamu. |
| 8. | Kama ndege aendaye huko na huko mbali na kitundu chake; Ndivyo alivyo mtu aendaye huko na huko mbali na mahali pake. |
| 9. | Marhamu na manukato huufurahisha moyo; Kadhalika utamu wa rafiki ya mtu utokao katika kusudi la moyo wake. |
| 10. | Usimwache rafiki yako mwenyewe, wala rafiki ya baba yako, Wala usiende nyumbani mwa ndugu yako siku ya msiba wako. Afadhali jirani aliye karibu kuliko ndugu aliye mbali. |
| 11. | Mwanangu, uwe na hekima na kunifurahisha moyo wangu; Ili nipate kumjibu anilaumuye. |
| 12. | Mwenye busara huyaona mabaya na kujificha; Bali wajinga huendelea mbele wakaumia. |
| 13. | Twaa nguo yake amdhaminiye mgeni; Mtoza rehani aliye mdhamini wa malaya. |
| 14. | Mtu ambarikiye mwenzake kwa sauti kuu asubuhi na mapema; Itahesabiwa kuwa ni laana kwake. |
| 15. | Kutona-tona daima siku ya mvua nyingi, Na mwanamke mgomvi ni sawasawa; |
| 16. | Atakaye kumzuia huyo huuzuia upepo; Na mkono wake wa kuume hukuta mafuta. |
| 17. | Chuma hunoa chuma; Ndivyo mtu aunoavyo uso wa rafiki yake. |
| 18. | Yeye autunzaye mtini atakula matunda yake; Naye amhudumiaye bwana wake ataheshimiwa. |
| 19. | Kama uso ufananavyo na uso katika maji; Kadhalika moyo wa mtu na mwenzake. |
| 20. | Kuzimu na Uharibifu havishibi; Wala macho ya wanadamu hayashibi. |
| 21. | Kalibu ni kwa fedha, na tanuru kwa dhahabu; Na mtu hujaribiwa kwa sifa zake. |
| 22. | Hata ukimtwanga mpumbavu kwa mchi kinuni pamoja na ngano; Upumbavu wake hautamtoka. |
| 23. | Fanya bidii kuijua hali ya makundi yako; Na kuwaangalia sana ng'ombe zako. |
| 24. | Kwa maana mali haziwi za milele; Na taji je! Yadumu tangu kizazi hata kizazi? |
| 25. | Manyasi huchukuliwa, na majani mabichi huonekana, Na maboga ya milimani hukusanyika. |
| 26. | Wana-kondoo hufaa kwa mavazi yako; Na mbuzi ni thamani ya shamba |
| 27. | Tena yatakuwapo maziwa ya mbuzi, Ya kukutosha kwa chakula chako, Na chakula cha watu wa nyumbani mwako, Na posho la vijakazi vyako. |
| ← Proverbs (27/31) → |