| ← Proverbs (26/31) → |
| 1. | Kama theluji wakati wa joto, na mvua wakati wa mavuno; Kadhalika heshima haimpasi mpumbavu. |
| 2. | Kama shomoro katika kutanga-tanga kwake, Na kama mbayuwayu katika kuruka kwake; Kadhalika laana isiyo na sababu haimpigi mtu. |
| 3. | Mjeledi kwa farasi, lijamu kwa punda, Na fimbo kwa mgongo wa mpumbavu. |
| 4. | Usimjibu mpumbavu sawasawa na upumbavu wake; Usije ukafanana naye. |
| 5. | Umjibu mpumbavu sawasawa na upumbavu wake; Asije akawa mwenye hekima machoni pake. |
| 6. | Apelekaye ujumbe kwa mkono wa mpumbavu Hujikata miguu, na kunywa hasara. |
| 7. | Miguu yake achechemeaye huwa dhaifu; Kadhalika mithali katika kinywa cha mpumbavu. |
| 8. | Kama mfuko wa vito katika chungu ya mawe; Kadhalika mtu amheshimuye mpumbavu. |
| 9. | Kama mwiba uingiao katika mkono wa mlevi; Kadhalika mithali katika kinywa cha mpumbavu. |
| 10. | Fundi stadi hufanyiza vitu vyote; Bali amwajiriye mpumbavu ni kama awaajiriye watu wapitao. |
| 11. | Kama vile mbwa arudiavyo matapiko yake; Kadhalika mpumbavu afanya upumbavu tena. |
| 12. | Je! Wamwona mtu mwenye hekima machoni pake mwenyewe? Afadhali kumtumaini mpumbavu kuliko yeye. |
| 13. | Mtu mvivu husema, Simba yuko njiani, Simba yuko katika njia kuu. |
| 14. | Kama vile mlango ugeukavyo katika bawaba zake; Kadhalika mtu mvivu katika kitanda chake. |
| 15. | Mtu mvivu hutia mkono wake sahanini; Kwamchosha kuupeleka tena kinywani pake. |
| 16. | Mtu mvivu ni mwenye hekima machoni pake, Kuliko watu saba wawezao kutoa sababu. |
| 17. | Mtu apitaye na kujisumbua kwa ugomvi usio wake; Ni kama mtu ashikaye mbwa kwa masikio yake. |
| 18. | Kama mtu mwenye wazimu atupaye mienge, Na mishale, na mauti; |
| 19. | Ndivyo alivyo amdanganyaye mwenzake, Na kusema, Je! Sikufanya mzaha tu? |
| 20. | Moto hufa kwa kukosa kuni; Na bila mchongezi fitina hukoma. |
| 21. | Kama makaa juu ya makaa yanayowaka, Na kama kuni juu ya moto; Ndivyo mtu mgomvi achocheavyo uadui. |
| 22. | Maneno ya mchongezi ni kama vitoweo. Nayo hushukia pande za ndani za tumbo. |
| 23. | Midomo ijipendekezayo pamoja na moyo mbaya Ni kama kigae kilichofunikizwa taka za fedha. |
| 24. | Achukiaye huficha chuki kwa midomo yake; Naye huweka akiba ya hila moyoni mwake. |
| 25. | Anenapo maneno mazuri usimsadiki; Kwa maana ana machukizo saba moyoni mwake. |
| 26. | Ingawa chuki hufunikizwa kwa hila; Uovu wake utadhihirika mbele ya kusanyiko. |
| 27. | Achimbaye shimo atatumbukia mwenyewe; Naye abingirishaye jiwe litamrudia. |
| 28. | Ulimi unenao uongo huwachukia wale uliowajeruhi; Na kinywa cha kujipendekeza hutenda uharibifu. |
| ← Proverbs (26/31) → |