← Proverbs (25/31) → |
1. | Hizi nazo ni mithali za Sulemani, ambazo watu wa Hezekia, mfalme wa Yuda, walizinakili. |
2. | Ni utukufu wa Mungu kuficha jambo; Bali ni utukufu wa mfalme kuchunguza jambo. |
3. | Mbingu huenda juu sana, na nchi huenda chini; Lakini mioyo ya wafalme haichunguziki. |
4. | Ondoa takataka katika fedha, Na chombo kitatokea kwa mtakasaji; |
5. | Mwondoe asiye haki mbele ya mfalme, Na kiti chake cha enzi kitathibitika katika haki. |
6. | Usijitukuze mbele ya uso wa mfalme; Wala usisimame mahali pa watu wakuu; |
7. | Kwa maana ni heri kuambiwa, Njoo huku mbele; Kuliko kuwekwa nyuma machoni pa mkuu. Yale uliyoyaona kwa macho, |
8. | Usitoke nje kwa haraka ili kuyashindania; Usije ukakosa kujua la kutenda hatimaye, Mwenzako atakapokuwa amekuaibisha. |
9. | Ujitetee na mwenzako peke yake; Bali usiifunue siri ya mtu mwingine; |
10. | Yeye asikiaye asije akakutukana; Na aibu yako isiondoke. |
11. | Neno linenwalo wakati wa kufaa, Ni kama machungwa katika vyano vya fedha. |
12. | Kipuli cha dhahabu, na pambo la dhahabu safi; Ndivyo alivyo mwonyaji mwenye hekima kwa sikio lisikialo. |
13. | Kama baridi ya theluji wakati wa mavuno; Ndivyo alivyo mjumbe mwaminifu kwao wamtumao; Kwa maana huwaburudisha bwana zake nafsi zao. |
14. | Kama mawingu na upepo pasipo mvua; Ndivyo alivyo yeye ajisifiaye karama kwa uongo. |
15. | Kwa uvumilivu mwingi mkuu husadikishwa; Na ulimi laini huvunja mfupa. |
16. | Je! Umeona asali? Kula kadiri ya kukutosha; Usije ukashiba na kuitapika. |
17. | Mguu wako usiingie katika nyumba ya jirani yako ila kwa kiasi; Asije akakukinai na kukuchukia. |
18. | Mtu amshuhudiaye jirani yake uongo Ni nyundo, na upanga, na mshale mkali. |
19. | Kumtumaini asiye mwaminifu wakati wa taabu Ni kama jino lililovunjika, au mguu ulioteguka. |
20. | Amwimbiaye nyimbo mtu mwenye moyo mzito, Ni kama yeye avuaye nguo wakati wa baridi; Ni kama siki juu ya magadi. |
21. | Adui yako akiwa ana njaa, mpe chakula; Tena akiwa ana kiu, mpe maji ya kunywa; |
22. | Maana utatia makaa ya moto kichwani pake; Na Bwana atakupa thawabu. |
23. | Upepo wa kusi huleta mvua; Vile vile asingiziaye huleta uso wa ghadhabu. |
24. | Ni afadhali kukaa katika pembe ya darini, Kuliko katika nyumba pana pamoja na mwanamke mgomvi. |
25. | Kama vile maji ya baridi kwa mtu mwenye kiu, Ndivyo ilivyo habari njema itokayo katika nchi ya mbali. |
26. | Mwenye haki amwangukiapo mtu mbaya Ni kama chemchemi iliyochafuka, Na kisima kilichokanyagwa. |
27. | Haifai kula asali nyingi mno; Vile vile mtu kutafuta utukufu wake mwenyewe si utukufu. |
28. | Asiyetawala roho yake Ni mfano wa mji uliobomolewa, usio na kuta. |
← Proverbs (25/31) → |