| ← Proverbs (24/31) → |
| 1. | Usiwahusudu watu waovu, Wala usitamani kuwa pamoja nao; |
| 2. | Kwa maana moyo wao hufikiri dhuluma, Na midomo yao huongea madhara. |
| 3. | Nyumba hujengwa kwa hekima, Na kwa ufahamu huthibitika, |
| 4. | Na kwa maarifa vyumba vyake hujazwa Vitu vyote vya thamani na vya kupendeza. |
| 5. | Mtu mwenye hekima ana nguvu; Naam, mtu wa maarifa huongeza uwezo; |
| 6. | Maana kwa mashauri ya akili utafanya vita; Na kwa wingi wa washauri huja wokovu. |
| 7. | Kwa mpumbavu hekima haipatikani; Hafumbui kinywa chake langoni. |
| 8. | Mtu afikiriye kutenda maovu, Watu watamwita mtundu; |
| 9. | Fikira za mpumbavu ni dhambi, Na mwenye mzaha huwachukiza watu. |
| 10. | Ukizimia siku ya taabu, Nguvu zako ni chache. |
| 11. | Uwaokoe wanaochukuliwa ili wauawe; Nao walio tayari kuchinjwa uwaopoe. |
| 12. | Ukisema, Sisi hatukujua hayo; Je! Yeye aipimaye mioyo siye afahamuye? Naye ailindaye nafsi yako siye ajuaye? Je! Hatamlipa kila mtu sawasawa na kazi yake? |
| 13. | Mwanangu, ule asali, kwa maana ni njema, Na sega la asali lililo tamu ulionjapo. |
| 14. | Basi utaijua hekima kuwa tamu kwa nafsi yako; Ikiwa umekwisha kuiona; Ndipo itakapofuata thawabu; Wala tumaini lako halitabatilika. |
| 15. | Ewe mtu mbaya, usiyavizie makao yake mwenye haki; Wala usipaharibu mahali pake pa kupumzika; |
| 16. | Kwa maana mwenye haki huanguka mara saba akaondoka tena; Bali wasio haki hukwazwa na mabaya. |
| 17. | Usifurahi, adui yako aangukapo; Wala moyo wako usishangilie ajikwaapo; |
| 18. | Bwana asije akaliona hilo, likamkasirisha; Akageuzia mbali naye hasira yake. |
| 19. | Usikasirike kwa sababu ya watenda mabaya; Wala usiwahusudu wabaya; |
| 20. | Kwa maana mtu mbaya hapati thawabu; Taa ya mtu mbaya itazimika. |
| 21. | Mwanangu, mche Bwana, na mfalme; Wala usishirikiane na wenye kigeugeu; |
| 22. | Maana msiba wao utatokea kwa ghafula; Tena ni nani aujuaye uharibifu wa miaka yao. |
| 23. | Haya nayo pia ni maneno ya wenye akili. Kupendelea watu katika hukumu si kwema. |
| 24. | Amwambiaye mtu mwovu, Wewe una haki; Kabila za watu watamlaani, taifa watamchukia. |
| 25. | Bali kwao wakemeao furaha itakuwako; Na baraka ya kufanikiwa itawajilia. |
| 26. | Aibusu midomo atoaye jawabu la haki. |
| 27. | Tengeneza kazi yako huko nje, Jifanyizie kazi yako tayari shambani, Ukiisha, jenga nyumba yako. |
| 28. | Usimshuhudie jirani yako pasipo sababu, Wala usidanganye kwa midomo yako. |
| 29. | Usiseme, Nitamtenda kama alivyonitenda mimi; Nitamlipa mtu huyo sawasawa na tendo lake. |
| 30. | Nalipita karibu na shamba la mvivu, Na shamba la mizabibu la mtu asiye na akili. |
| 31. | Kumbe! Lote pia limemea miiba; Uso wake ulifunikwa kwa viwawi; Na ukuta wake wa mawe umebomoka. |
| 32. | Ndipo nilipoangalia na kufikiri sana; Naliona, nikapata mafundisho. |
| 33. | Bado kulala kidogo, kusinzia kidogo, Bado kukunja mikono upate usingizi! |
| 34. | Hivyo, umaskini wako huja kama mnyang'anyi, Na uhitaji wako kama mtu mwenye silaha. |
| ← Proverbs (24/31) → |