← Proverbs (23/31) → |
1. | Utakapoketi kwa chakula pamoja na mtawala, Mwangalie sana yeye aliye mbele yako. |
2. | Tena ujitie kisu kooni, Kama ukiwa mlafi. |
3. | Usivitamani vyakula vyake vya anasa; Kwa maana ni vyakula vya hila. |
4. | Usijitaabishe ili kupata utajiri; Acha kuzitegemea akili zako mwenyewe. |
5. | Je! Utavikazia macho vile ambavyo si kitu? Maana bila shaka mali hujifanyia mabawa, Kama tai arukaye mbinguni. |
6. | Usile mkate wa mtu mwenye husuda; Wala usivitamani vyakula vyake vya anasa; |
7. | Maana aonavyo nafsini mwake, ndivyo alivyo. Akuambia, Haya, kula, kunywa; Lakini moyo wake hauwi pamoja nawe. |
8. | Tonge lile ulilokula utalitapika, Na maneno yako matamu yatakupotea. |
9. | Usiseme masikioni mwa mpumbavu; Maana atadharau hekima ya maneno yako. |
10. | Usiiondoe alama ya mpaka wa zamani; Wala usiingie katika mashamba ya yatima; |
11. | Kwa sababu mkombozi wao ana nguvu; Atawatetea juu yako. |
12. | Elekeza moyo wako kusikiliza mafundisho; Tega masikio yako kusikia maneno ya maarifa. |
13. | Usimnyime mtoto wako mapigo; Maana ukimpiga kwa fimbo hatakufa. |
14. | Utampiga kwa fimbo, Na kumwokoa nafsi yake na Kuzimu. |
15. | Mwanangu, kama moyo wako una hekima, Moyo wangu utafurahi, naam, moyo wangu; |
16. | Naam, viuno vyangu vitafurahi, Midomo yako inenapo maneno mema. |
17. | Moyo wako usiwahusudu wenye dhambi; Bali mche Bwana mchana kutwa; |
18. | Maana bila shaka iko thawabu; Na tumaini lako halitabatilika. |
19. | Sikia, mwanangu, uwe na hekima, Na kuuongoza moyo wako katika njia njema. |
20. | Usiwe miongoni mwao wanywao mvinyo; Miongoni mwao walao nyama kwa pupa. |
21. | Kwa maana mlevi na mlafi huingia umaskini, Na utepetevu humvika mtu nguo mbovu. |
22. | Msikilize baba yako aliyekuzaa, Wala usimdharau mama yako akiwa mzee. |
23. | Inunue kweli, wala usiiuze; Naam, hekima, na mafundisho, na ufahamu. |
24. | Baba yake mwenye haki atashangilia; Naye amzaaye mtoto mwenye hekima atamfurahia. |
25. | Na wafurahi baba yako na mama yako; Na afurahi aliyekuzaa. |
26. | Mwanangu, nipe moyo wako; Macho yako yapendezwe na njia zangu. |
27. | Kwa maana kahaba ni shimo refu; Na malaya ni rima jembamba. |
28. | Naam, huotea kama mnyang'anyi; Huwaongeza wenye hila katika wanadamu. |
29. | Ni nani apigaye, Yowe? Ni nani aliaye, Ole? Ni nani mwenye ugomvi? Ni nani mwenye mguno? Ni nani aliye na jeraha zisizo na sababu? Ni nani aliye na macho mekundu? |
30. | Ni wale wakaao sana kwenye mvinyo; Waendao kutafuta divai iliyochanganyika. |
31. | Usiitazame mvinyo iwapo ni nyekundu; Iitiapo bilauri rangi yake, ishukapo taratibu; |
32. | Mwisho wake huuma kama nyoka; Huchoma kama fira. |
33. | Macho yako yataona mambo mageni; Na moyo wako utatoa yaliyopotoka. |
34. | Naam, utakuwa kama alalaye katikati ya bahari; Au kama yeye asinziaye juu ya mlingoti. |
35. | Utasema, Wamenichapa wala sikuumia; Wamenipiga wala sina habari; Nitaamka lini, nitazidi kuitafuta tena. |
← Proverbs (23/31) → |