← Proverbs (22/31) → |
1. | Heri kuchagua jina jema kuliko mali nyingi; Na neema kuliko fedha na dhahabu. |
2. | Tajiri na maskini hukutana pamoja; Bwana ndiye aliyewaumba wote wawili. |
3. | Mwenye busara huyaona mabaya na kujificha; Bali wajinga huendelea mbele wakaumia. |
4. | Thawabu ya unyenyekevu ambao ni kumcha Bwana Ni utajiri, na heshima, nayo ni uzima. |
5. | Miiba na mitego huwa katika njia ya mshupavu; Yeye aitunzaye nafsi yake atakuwa mbali nayo. |
6. | Mlee mtoto katika njia impasayo, Naye hataiacha, hata atakapokuwa mzee. |
7. | Tajiri humtawala maskini, Naye akopaye ni mtumwa wake akopeshaye. |
8. | Yeye apandaye uovu atavuna msiba, Na fimbo ya ghadhabu yake itakoma. |
9. | Mwenye jicho la ukarimu atabarikiwa; Maana huwapa maskini chakula chake. |
10. | Mtupe nje mwenye dharau, na ugomvi utatoka; Naam, fitina na fedheha zitakoma. |
11. | Apendaye usafi wa moyo, na neema ya midomo; Mfalme atakuwa rafiki yake. |
12. | Macho ya Bwana humhifadhi mwenye maarifa; Bali huyapindua maneno ya mtu haini. |
13. | Mtu mvivu husema, Simba yuko nje; Nitauawa katika njia kuu. |
14. | Kinywa cha malaya ni shimo refu; Anayechukiwa na Bwana atatumbukia ndani yake. |
15. | Ujinga umefungwa ndani ya moyo wa mtoto; Lakini fimbo ya adhabu itaufukuzia mbali. |
16. | Yeye awaoneaye maskini ili kuongeza mapato, Naye ampaye tajiri, hupata hasara. |
17. | Tega sikio lako uyasikie maneno ya wenye hekima, na kuuelekeza moyo wako kwa maarifa yangu; |
18. | maana ni vizuri kuyahifadhi ndani yako, hali yakithibitika pamoja midomoni mwako. |
19. | Ili matumaini yako uyaweke kwa Bwana, leo nimekujulisha wewe haya, naam, wewe. |
20. | Je! Sikukuandikia mambo makuu juu ya mashauri na juu ya maarifa; |
21. | ili kukujulisha hakika ya maneno ya kweli, uwarudishie wakutumao maneno ya kweli? |
22. | Usimnyang'anye maskini, kwa kuwa ni maskini; Wala usimdhulumu mtu mnyonge langoni; |
23. | Kwa sababu Bwana atawatetea; Naye atawateka uhai wao waliowateka. |
24. | Usifanye urafiki na mtu mwenye hasira nyingi; Wala usiende na mtu wa ghadhabu nyingi; |
25. | Usije ukajifunza njia zake; Na kujipatia nafsi yako mtego. |
26. | Usiwe mmoja wao wawekao rehani; Au walio wadhamini kwa deni za watu; |
27. | Kama huna kitu cha kulipa; Kwani ukaondolee kitanda chako chini yako? |
28. | Usiiondoe alama ya mpaka wa zamani, Uliowekwa na baba zako. |
29. | Je! Wamwona mtu mwenye bidii katika kazi zake? Huyo atasimama mbele ya wafalme; Hatasimama mbele ya watu wasio na cheo. |
← Proverbs (22/31) → |