| ← Proverbs (21/31) → |
| 1. | Moyo wa mfalme huwa katika mkono wa Bwana; Kama mifereji ya maji huugeuza po pote apendapo. |
| 2. | Kila njia ya mtu ni sawa machoni pake mwenyewe; Bali Bwana huipima mioyo. |
| 3. | Kutenda haki na hukumu Humpendeza Bwana kuliko kutoa sadaka. |
| 4. | Macho yenye kiburi, na moyo wa kutakabari, Hata ukulima wa waovu, ni dhambi. |
| 5. | Mawazo ya wenye bidii huuelekea utajiri tu; Bali kila mwenye pupa huuelekea uhitaji. |
| 6. | Kupata akiba ya mali kwa ulimi wa uongo Ni moshi upeperushwao; ni kutafuta mauti. |
| 7. | Jeuri ya wabaya itawaondolea mbali; Kwa sababu wamekataa kutenda hukumu. |
| 8. | Njia yake aliyelemewa na dhambi imepotoka sana; Bali mtu aliye safi, kazi yake ni sawasawa. |
| 9. | Ni afadhali kukaa katika pembe ya darini, Kuliko katika nyumba pana pamoja na mwanamke mgomvi. |
| 10. | Nafsi ya mtu mbaya hutamani uovu; Jirani yake hapati fadhili machoni pake. |
| 11. | Mwenye mzaha aadhibiwapo, mjinga hupata hekima; Na mwenye hekima afundishwapo, hupokea maarifa. |
| 12. | Mwenye haki huitafakari nyumba ya mtu mbaya; Jinsi wabaya waangushwavyo wakaangamia. |
| 13. | Azibaye masikio yake asisikie kilio cha maskini, Yeye naye atalia, lakini hatasikiwa. |
| 14. | Kipawa cha siri hutuliza hasira; Na rushwa bindoni humliza ghadhabu kali. |
| 15. | Ni furaha yao wenye haki kutenda hukumu; Lakini ni uharibifu kwao watendao maovu. |
| 16. | Mtu aikosaye njia ya busara Atakaa katika mkutano wao waliokufa. |
| 17. | Mtu apendaye anasa atakuwa maskini; Apendaye mvinyo na mafuta hatakuwa tajiri. |
| 18. | Mtu asiye haki ni fidia ya wenye haki; Naye afanyaye hila ni badala ya watu wa adili. |
| 19. | Ni afadhali kukaa katika nchi ya nyika; Kuliko na mwanamke mgomvi, mchokozi. |
| 20. | Kuna hazina ya thamani na mafuta katika maskani ya mwenye hekima; Bali mwanadamu aliye mpumbavu huyameza. |
| 21. | Aandamaye haki na fadhili, Ataona uhai na haki na heshima. |
| 22. | Mwenye hekima huupandia mji wao wenye nguvu; Na kuziangusha nguvu za tumaini lao. |
| 23. | Mtu azuiaye kinywa chake na ulimi wake, Atajilinda nafsi yake na taabu. |
| 24. | Mwenye kiburi na kutakabari, jina lake ni mbishi; Hutenda mambo katika majivuno ya kiburi chake. |
| 25. | Matakwa yake mtu mvivu humfisha, Kwa maana mikono yake hukataa kufanya kazi. |
| 26. | Kuna atamaniye kwa choyo mchana kutwa; Bali mwenye haki hutoa wala hanyimi. |
| 27. | Sadaka ya wasio haki ni chukizo; Si zaidi sana ailetapo mwenye nia mbaya! |
| 28. | Shahidi wa uongo atapotea; Bali mtu asikiaye atasema maneno yadumuyo. |
| 29. | Asiye haki huufanya uso wake kuwa mgumu; Bali mtu mnyofu huzifikiri njia zake. |
| 30. | Hapana hekima, wala ufahamu, Wala shauri, juu ya Bwana. |
| 31. | Farasi huwekwa tayari kwa siku ya vita; Lakini Bwana ndiye aletaye wokovu. |
| ← Proverbs (21/31) → |