← Proverbs (20/31) → |
1. | Mvinyo hudhihaki, kileo huleta ugomvi; Na akosaye kwa vitu hivyo hana hekima. |
2. | Utisho wa mfalme ni kama ngurumo ya simba; Amkasirishaye huitendea dhambi nafsi yake. |
3. | Mtu kujitenga na ugomvi ni heshima kwake; Bali kila mpumbavu ataka kugombana. |
4. | Mtu mvivu hataki kulima wakati wa baridi; Hivyo wakati wa mavuno ataomba, hana kitu. |
5. | Mashauri ya moyoni ni kama kilindi; Lakini mtu mwenye ufahamu atayateka. |
6. | Wanadamu hutangaza kila mtu hisani yake mwenyewe; Bali mtu aliye mwaminifu, ni nani awezaye kumpata? |
7. | Mwenye haki aendaye katika unyofu wake, Watoto wake wabarikiwa baada yake. |
8. | Mfalme aketiye katika kiti cha hukumu, Huyapepeta mabaya yote kwa macho yake. |
9. | Nani awezaye kusema, Nimesafisha moyo wangu; Nimetakasika dhambi yangu? |
10. | Vipimo mbalimbali, na pishi mbalimbali, Vyote viwili ni chukizo kwa Bwana. |
11. | Hata mtoto hujijulisha kwa matendo yake; Kwamba kazi yake ni safi, kwamba ni adili. |
12. | Sikio lisikialo, na jicho lionalo, Bwana ndiye aliyeyafanya yote mawili. |
13. | Usipende usingizi usije ukawa maskini; Fumbua macho yako nawe utashiba chakula. |
14. | Haifai kitu, haifai kitu, asema mnunuzi; Lakini akiisha kwenda zake hujisifu. |
15. | Dhahabu iko, na marijani tele; Lakini midomo ya maarifa ni kito cha thamani. |
16. | Twaa nguo yake amdhaminiye mgeni; Mtoze rehani aliye mdhamini wa wageni. |
17. | Chakula cha uongo ni kitamu kwa mtu; Lakini halafu kinywa chake kitajaa changarawe. |
18. | Kila kusudi huthibitika kwa kushauriana; Na kwa shauri la akili fanya vita. |
19. | Mwenye kitango akisingizia hufunua siri; Basi, usishirikiane naye afunuaye midomo yake sana. |
20. | Amlaaniye babaye au mamaye, Taa yake itazimika katika giza kuu. |
21. | Urithi uliopatikana mwanzo kwa haraka, Mwisho wake, lakini, hautabarikiwa. |
22. | Usiseme, Mimi nitalipa mabaya; Mngojee Bwana, naye atakuokoa. |
23. | Vipimo mbalimbali ni chukizo kwa Bwana; Tena mizani ya hila si njema. |
24. | Mwenendo wa mtu watoka kwa Bwana; Basi, awezaje mtu kuelewa na njia yake? |
25. | Ni mtego, mtu aseme kwa haraka, Kitu hiki ni wakfu; Na baada ya kuweka nadhiri kuuliza-uliza habari. |
26. | Mfalme mwenye hekima huwapepeta wasio haki; Naye hulipitisha gurudumo la kupuria juu yao. |
27. | Pumzi ya mwanadamu ni taa ya Bwana; Hupeleleza yote yaliyomo ndani yake. |
28. | Fadhili na uaminifu humhifadhi mfalme, Na kiti chake cha enzi huthibitishwa kwa fadhili. |
29. | Fahari ya vijana ni nguvu zao, Na uzuri wa wazee ni kichwa chenye mvi. |
30. | Machubuko ya fimbo husafisha uovu, Na mapigo hufikilia ndani ya mtima. |
← Proverbs (20/31) → |