Proverbs (2/31)  

1. Mwanangu, kama ukiyakubali maneno yangu, Na kuyaweka akiba maagizo yangu;
2. Hata ukatega sikio lako kusikia hekima, Ukauelekeza moyo wako upate kufahamu;
3. Naam, ukiita busara, Na kupaza sauti yako upate ufahamu;
4. Ukiutafuta kama fedha, Na kuutafutia kama hazina iliyositirika;
5. Ndipo utakapofahamu kumcha Bwana, Na kupata kumjua Mungu.
6. Kwa kuwa Bwana huwapa watu hekima; Kinywani mwake hutoka maarifa na ufahamu;
7. Huwawekea wanyofu akiba ya hekima kamili; Yeye ni ngao kwao waendao kwa ukamilifu;
8. Apate kuyalinda mapito ya hukumu, Na kuhifadhi njia ya watakatifu wake.
9. Ndipo utakapofahamu haki na hukumu, Na adili, na kila njia njema.
10. Maana hekima itaingia moyoni mwako, Na maarifa yatakupendeza nafsi yako;
11. Busara itakulinda; Ufahamu utakuhifadhi.
12. Ili kukuokoa na njia ya uovu, Na watu wanenao yaliyopotoka;
13. Watu waziachao njia za unyofu, Ili kuziendea njia za giza;
14. Wafurahio kutenda mabaya; Wapendezwao na upotoe wa waovu;
15. Waliopotoka katika njia zao; Walio wakaidi katika mapito yao.
16. Ili kuokoka na malaya, Naam, malaya mwenye kubembeleza kwa maneno yake;
17. Amwachaye rafiki wa ujana wake, Na kulisahau agano la Mungu wake.
18. Maana nyumba yake inaelekea mauti, Na mapito yake yanakwenda kwenye wafu.
19. Katika hao wamwendeao harudi hata mmoja, Wala hawazifikilii njia za uzima.
20. Ili upate kwenda katika njia ya watu wema, Na kuyashika mapito ya wenye haki.
21. Maana wanyofu watakaa katika nchi, Na wakamilifu watadumu ndani yake.
22. Bali waovu watatengwa na nchi, Nao wafanyao hila watang'olewa.

  Proverbs (2/31)