| ← Proverbs (19/31) → |
| 1. | Afadhali maskini aendaye katika unyofu wake, Kuliko mpotofu wa midomo aliye mpumbavu. |
| 2. | Tena si vizuri nafsi ya mtu ikose maarifa; Naye afanyaye haraka kwa miguu hutenda dhambi. |
| 3. | Upumbavu wa mtu hupotosha njia yake; Na moyo wake hununa juu ya Bwana. |
| 4. | Utajiri huongeza rafiki wengi; Bali maskini hutengwa na rafiki yake. |
| 5. | Shahidi wa uongo hakosi ataadhibiwa; Wala asemaye uongo hataokoka. |
| 6. | Watu wengi watamsihi mkuu ili awafadhili; Na kila mtu ni rafiki yake atoaye tunu. |
| 7. | Ndugu zote wa maskini humchukia; Jinsi gani rafiki zake huzidi kujitenga naye! Huwafuata kwa maneno, lakini wametoweka. |
| 8. | Apataye hekima hujipenda nafsi yake; Ashikaye ufahamu atapata mema. |
| 9. | Shahidi wa uongo hakosi ataadhibiwa; Naye asemaye uongo ataangamia. |
| 10. | Maisha ya anasa hayampasi mpumbavu; Sembuse mtumwa awatawale wakuu. |
| 11. | Busara ya mtu huiahirisha hasira yake; Nayo ni fahari yake kusamehe makosa. |
| 12. | Ghadhabu ya mfalme ni kama ngurumo ya simba; Bali hisani yake kama umande juu ya majani. |
| 13. | Mwana mpumbavu ni msiba kwa babaye; Na ugomvi wa mke kama kutona-tona daima. |
| 14. | Nyumba na mali ni urithi apatao mtu kwa babaye; Bali mke mwenye busara, mtu hupewa na Bwana. |
| 15. | Uvivu humtia mtu katika usingizi mzito; Na nafsi yake mvivu itaona njaa. |
| 16. | Yeye aihifadhiye amri huihifadhi nafsi yake; Bali yeye asiyeziangalia njia zake atakufa. |
| 17. | Amhurumiaye maskini humkopesha Bwana; Naye atamlipa kwa tendo lake jema. |
| 18. | Mrudi mwanao, kwa maana liko tumaini; Wala usiikaze nafsi yako kwa kuangamia kwake. |
| 19. | Mtu wa hasira nyingi atachukua adhabu yake, Maana ujapomwokoa huna budi kufanya tena. |
| 20. | Sikiliza mashauri, ukapokee mafundisho, Upate kuwa na hekima siku zako za mwisho. |
| 21. | Mna hila nyingi moyoni mwa mtu; Lakini shauri la Bwana ndilo litakalosimama. |
| 22. | Haja ya mwanadamu ni hisani yake; Ni afadhali maskini kuliko mwongo. |
| 23. | Kumcha Bwana huelekea uhai; Atakaa ameshiba; hatajiliwa na ubaya. |
| 24. | Mtu mvivu hutia mkono wake sahanini; Ila hataki hata kuupeleka kinywani pake. |
| 25. | Mpige mwenye mzaha, na mjinga atapata busara; Mwonye mwenye ufahamu, naye atatambua maarifa. |
| 26. | Apotezaye mali za babaye na kumfukuza mamaye, Ni mwana aaibishaye, na kuleta lawama. |
| 27. | Mwanangu, acha kusikia mafundisho, Ukitaka tu kuyaasi maneno ya maarifa. |
| 28. | Shahidi asiyefaa kitu hudhihaki hukumu, Na vinywa vya wasio haki humeza uovu. |
| 29. | Hukumu zimewekwa tayari kwa wenye mzaha; Na mapigo kwa mgongo wa wapumbavu. |
| ← Proverbs (19/31) → |