Proverbs (18/31)  

1. Ajitengaye na wenzake hutafuta matakwa yake mwenyewe; Hushindana na kila shauri jema.
2. Mpumbavu hapendezwi na ufahamu; Ila moyo wake udhihirike tu.
3. Ajapo asiye haki, huja dharau pia; Na pamoja na aibu huja lawama.
4. Maneno ya kinywa cha mtu ni kama maji ya vilindi; Kijito kibubujikacho; chemchemi ya hekima.
5. Kukubali uso wake asiye haki si vizuri; Wala kumpotosha mwenye haki hukumuni.
6. Midomo ya mpumbavu huingia katika fitina, Na kinywa chake huita mapigo.
7. Kinywa cha mpumbavu ni uharibifu wake, Na midomo yake ni mtego wa nafsi yake.
8. Maneno ya mchongezi ni kama vitoweo; Nayo hushukia pande za ndani za tumbo.
9. Yeye naye aliye mvivu katika kazi yake, Ni ndugu yake aliye mharabu.
10. Jina la Bwana ni ngome imara; Mwenye haki huikimbilia, akawa salama.
11. Mali ya mtu tajiri ni mji wake wa nguvu; Ni kama ukuta mrefu katika mawazo yake.
12. Kabla ya uharibifu moyo wa mwanadamu hujivuna; Na kabla ya heshima hutangulia unyenyekevu.
13. Yeye ajibuye kabla hajasikia, Ni upumbavu na aibu kwake.
14. Roho ya mtu itastahimili udhaifu wake; Bali roho iliyovunjika nani awezaye kuistahimili?
15. Moyo wa mwenye busara hupata maarifa; Na sikio la mwenye hekima hutafuta maarifa.
16. Zawadi ya mtu humpatia nafasi; Humleta mbele ya watu wakuu.
17. Ajiteteaye kwanza huonekana kuwa ana haki; Lakini jirani yake huja na kumchunguza.
18. Kura hukomesha mashindano; Hukata maneno ya wakuu.
19. Ndugu aliyechukizwa ni mgumu kuliko mji wa nguvu; Na mashindano ni kama mapingo ya ngome.
20. Tumbo la mtu litajazwa matunda ya kinywa chake; Atashiba mazao ya midomo yake.
21. Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi; Na wao waupendao watakula matunda yake.
22. Apataye mke apata kitu chema; Naye ajipatia kibali kwa Bwana.
23. Maskini hutumia maombi; Bali tajiri hujibu kwa ukali.
24. Ajifanyiaye rafiki wengi ni kwa uangamivu wake mwenyewe; Lakini yuko rafiki aambatanaye na mtu kuliko ndugu.

  Proverbs (18/31)