← Proverbs (17/31) → |
1. | Afadhali mego kavu pamoja na utulivu, Kuliko nyumba yenye karamu nyingi pamoja na magomvi. |
2. | Mtumwa atendaye kwa busara atamtawala mwana atendaye mambo ya aibu; Tena atapata sehemu ya urithi kati ya ndugu. |
3. | Kalibuni kwa fedha, na tanuru kwa dhahabu; Bali Bwana huijaribu mioyo. |
4. | Mtenda mabaya husikiliza midomo ya uovu; Na mwongo hutega sikio lake kusikiliza ulimi wa madhara. |
5. | Amdhihakiye maskini humsuta Muumba wake; Naye aufurahiaye msiba hatakosa adhabu. |
6. | Wana wa wana ndio taji ya wazee, Na utukufu wa watoto ni baba zao. |
7. | Maneno mazuri hayapendezi kinywani mwa mpumbavu; Siuze midomo ya uongo kinywani mwa mkuu. |
8. | Kipawa ni kama kito cha thamani machoni pake yeye aliye nacho; Kila kigeukapo hufanikiwa. |
9. | Afunikaye kosa hutafuta kupendwa; Bali yeye akashifuye neno hutenga rafiki. |
10. | Lawama hupenya moyoni mwa mwenye ufahamu, Kuliko mapigo mia moyoni mwa mpumbavu. |
11. | Mtu mwovu hataki neno ila kuasi tu; Kwa hiyo mjumbe mkali atatumwa kwake. |
12. | Afadhali mtu akutwe na dubu aliyenyang'anywa watoto wake, Kuliko na mpumbavu katika upumbavu wake. |
13. | Yeye arudishaye mabaya badala ya mema, Mabaya hayataondoka nyumbani mwake. |
14. | Mwanzo wa ugomvi ni kama kutoboa penye maji; Basi acheni ugomvi kabla haujafurika. |
15. | Yeye asemaye kwamba asiye haki ana haki; naye asemaye kwamba mwenye haki hana haki; Hao wote wawili ni chukizo kwa Bwana. |
16. | Nini maana yake, mpumbavu kuwa na fedha mkononi mwake ya kununulia hekima, Ikiwa hana moyo wa ufahamu? |
17. | Rafiki hupenda sikuzote; Na ndugu amezaliwa kwa siku ya taabu. |
18. | Aliyepungukiwa na akili hupana mkono na mtu; Na kuwa mdhamini mbele ya mwenzake. |
19. | Apendaye ugomvi hupenda dhambi; Auinuaye sana mlango wake hutafuta uharibifu. |
20. | Mtu mwenye moyo wa ukaidi hatapata mema; Na mwenye ulimi wa upotofu huanguka katika misiba. |
21. | Azaaye mpumbavu ni kwa huzuni yake mwenyewe; Wala baba wa mpumbavu hana furaha. |
22. | Moyo uliochangamka ni dawa nzuri; Bali roho iliyopondeka huikausha mifupa. |
23. | Asiye haki hutoa rushwa kifuani, Ili kuzipotosha njia za hukumu. |
24. | Hekima huwa machoni pake mwenye ufahamu; Bali macho ya mpumbavu huwa katika ncha za dunia. |
25. | Mwana mpumbavu ni huzuni kwa babaye, Na uchungu kwa mamaye aliyemzaa. |
26. | Tena kumwadhibu mwenye haki si vizuri; Wala si kwema kuwapiga wakuu kwa unyofu wao. |
27. | Azuiaye maneno yake ni mwenye maarifa; Na mwenye roho ya utulivu ana busara. |
28. | Hata mpumbavu akinyamaza, huhesabiwa hekima; Akifumba midomo yake, huhesabiwa ufahamu. |
← Proverbs (17/31) → |