← Proverbs (16/31) → |
1. | Maandalio ya moyo ni ya mwanadamu; Bali jawabu la ulimi hutoka kwa Bwana. |
2. | Njia zote za mtu ni safi machoni pake mwenyewe; Bali Bwana huzipima roho za watu. |
3. | Mkabidhi Bwana kazi zako, Na mawazo yako yatathibitika. |
4. | Bwana amefanya kila kitu kwa kusudi lake; Naam, hata wabaya kwa siku ya ubaya. |
5. | Kila mwenye moyo wa kiburi ni chukizo kwa Bwana; Hakika, hatakosa adhabu. |
6. | Kwa rehema na kweli uovu husafishwa; Kwa kumcha Bwana watu hujiepusha na maovu. |
7. | Njia za mtu zikimpendeza Bwana, Hata adui zake huwapatanisha naye. |
8. | Afadhali mali kidogo pamoja na haki, Kuliko mapato mengi pamoja na udhalimu. |
9. | Moyo wa mtu huifikiri njia yake; Bali Bwana huziongoza hatua zake. |
10. | Kukata maneno huwa katika midomo ya mfalme; Kinywa chake hakitakosa katika hukumu. |
11. | Mizani ya haki na vitanga vyake ni vya Bwana; Mawe yote ya mfukoni ni kazi yake. |
12. | Wafalme wakitenda yasiyo haki ni chukizo; Maana kiti cha enzi huthibitika kwa haki. |
13. | Midomo ya haki ni furaha ya wafalme; Nao humpenda yeye asemaye yaliyo sawa. |
14. | Hasira ya mfalme ni kama wajumbe wa mauti; Lakini mtu mwenye hekima ataituliza. |
15. | Kuna uhai katika nuru ya uso wa mfalme, Na fadhili zake ni kama wingu la masika. |
16. | Si afadhali kupata hekima kuliko dhahabu? Naam, yafaa kuchagua ufahamu kuliko fedha. |
17. | Njia kuu ya mwenye haki ni kujitenga na uovu; Yeye ashikaye njia yake huihifadhi nafsi yake. |
18. | Kiburi hutangulia uangamivu; Na roho yenye kutakabari hutangulia maanguko. |
19. | Afadhali kuwa na roho ya unyenyekevu pamoja na maskini, Kuliko kugawanya nyara pamoja na wenye kiburi. |
20. | Atakayelitafakari neno atapata mema; Na kila amwaminiye Bwana ana heri. |
21. | Aliye na hekima moyoni ataitwa mwenye busara; Utamu wa maneno huongeza elimu. |
22. | Ufahamu ni chemchemi ya uzima kwake aliye nao; Bali kufundishwa kwa wapumbavu ni upuzi wao. |
23. | Moyo wake mwenye hekima hufundisha kinywa chake; Huzidisha elimu ya midomo yake. |
24. | Maneno yapendezayo ni kama sega la asali; Ni tamu nafsini, na afya mifupani. |
25. | Iko njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu; Lakini mwisho wake ni njia za mauti. |
26. | Nafsi yake mfanya kazi hujifanyia kazi; Maana kinywa chake humtia bidii. |
27. | Mtu asiyefaa kitu huchimba shimo la madhara; Katika midomo yake mna moto uteketezao. |
28. | Mtu mshupavu huondokesha fitina; Na mchongezi huwafarakanisha rafiki. |
29. | Mtu mkali humshawishi mwenzake; Humwongoza katika njia isiyo njema. |
30. | Afumbaye macho, kusudi lake ni kuwaza yaliyopotoka; Aikazaye midomo yake hutokeza mabaya. |
31. | Kichwa chenye mvi ni taji ya utukufu, Kama kikionekana katika njia ya haki. |
32. | Asiye mwepesi wa hasira ni mwema kuliko shujaa; Na mtu aitawalaye roho yake kuliko mtu atekaye mji. |
33. | Kura hutupwa katika mikunjo ya nguo; Lakini hukumu zake zote ni za Bwana. |
← Proverbs (16/31) → |