Proverbs (15/31)  

1. Jawabu la upole hugeuza hasira; Bali neno liumizalo huchochea ghadhabu.
2. Ulimi wa mwenye hekima hutamka maarifa vizuri; Bali vinywa vya wapumbavu humwaga upumbavu.
3. Macho ya Bwana yako kila mahali; Yakimchunguza mbaya na mwema.
4. Ulimi safi ni mti wa uzima; Bali ukorofi wa ulimi huvunja moyo.
5. Mpumbavu hudharau kurudiwa na babaye; Bali yeye aangaliaye maonyo hupata busara.
6. Katika nyumba ya mwenye haki mna akiba nyingi; Bali mapato ya mtu mbaya huwa taabu tu.
7. Midomo ya mwenye haki hueneza maarifa; Bali moyo wa mpumbavu haufanyi hivyo.
8. Sadaka ya mtu mbaya ni chukizo kwa Bwana; Bali maombi ya mtu mnyofu ni furaha yake.
9. Njia ya mtu mbaya ni chukizo kwa Bwana; Bali humpenda mtu afuatiaye wema.
10. Adhabu kali ina yeye aiachaye njia; Naye achukiaye kukemewa atakufa.
11. Kuzimu na Uharibifu vi wazi mbele za Bwana; Si zaidi basi, mioyo ya wanadamu?
12. Mwenye mzaha hapendi kukaripiwa; Wala yeye hawaendei wenye hekima.
13. Moyo wa furaha huchangamsha uso; Bali kwa huzuni ya moyo roho hupondeka.
14. Moyo wa mwenye ufahamu hutafuta maarifa; Bali kinywa cha wapumbavu hula upumbavu.
15. Siku zote za mtu ateswaye ni mbaya; Bali ukunjufu wa moyo ni karamu ya daima.
16. Kuwa na mali chache pamoja na kumcha Bwana; Ni bora kuliko mali nyingi pamoja na taabu.
17. Chakula cha mboga penye mapendano; Ni bora kuliko ng'ombe aliyenona pamoja na kuchukiana.
18. Mtu wa hasira huchochea ugomvi; Bali asiye mwepesi wa hasira hutuliza mashindano.
19. Njia ya mtu mvivu ni kama boma la miiba; Bali mapito yao wenye unyofu hufanyika njia kuu.
20. Mwana mwenye hekima humfurahisha babaye; Bali mpumbavu humdharau mamaye.
21. Upumbavu ni furaha kwake aliyepungukiwa na akili; Bali mwenye ufahamu huunyosha mwenendo wake.
22. Pasipo mashauri makusudi hubatilika; Bali kwa wingi wa washauri huthibithika.
23. Mtu hulifurahia jibu la kinywa chake; Na neno linenwalo wakati wa kufaa ni jema kama nini!
24. Kwa mtu mwenye akili njia ya uhai huenda juu; Ili atoke katika kuzimu chini.
25. Bwana ataing'oa nyumba ya mwenye kiburi; Bali atauthibitisha mpaka wa mjane.
26. Mashauri mabaya ni chukizo kwa Bwana; Bali maneno yapendezayo ni safi.
27. Atamaniye faida huifadhaisha nyumba yake mwenyewe; Bali achukiaye zawadi ataishi.
28. Moyo wa mwenye haki hufikiri jinsi atakavyojibu; Bali kinywa cha wasio haki humwaga mabaya.
29. Bwana yu mbali na wasio haki; Bali huisikia sala ya mwenye haki.
30. Mng'ao wa macho huufurahisha moyo; Habari njema huinenepesha mifupa.
31. Sikio lisikilizalo lawama yenye uhai Litakaa kati yao wenye hekima.
32. Akataaye maonyo huidharau nafsi yake mwenyewe; Bali yeye asikilizaye lawama hujipatia ufahamu.
33. Kumcha Bwana ni maonyo ya hekima; Na kabla ya heshima hutangulia unyenyekevu.

  Proverbs (15/31)