← Proverbs (14/31) → |
1. | Kila mwanamke aliye na hekima hujenga nyumba yake; Bali aliye mpumbavu huibomoa kwa mikono yake mwenyewe. |
2. | Yeye aendaye kwa unyofu wake humcha Bwana; Bali aliye mkaidi katika njia zake humdharau. |
3. | Katika kinywa cha mpumbavu mna fimbo ya kiburi, Bali midomo ya wenye hekima huwahifadhi. |
4. | Zizi ni safi ambapo hapana ng'ombe; Bali nguvu za ng'ombe zaleta faida nyingi. |
5. | Shahidi mwaminifu hatasema uongo; Bali shahidi wa uongo, pumzi zake ni uongo. |
6. | Mwenye dharau hutafuta hekima, asiipate; Bali maarifa huwa mepesi kwa mwenye ufahamu. |
7. | Toka mbele ya uso wa mpumbavu, Maana hutaona kwake midomo ya maarifa. |
8. | Akili za mwenye busara ni kujua njia yake; Lakini upumbavu wa wapumbavu ni udanganyifu. |
9. | Wapumbavu huidharau hatia; Bali upo upendeleo kwa wenye haki. |
10. | Moyo huujua uchungu wa nafsi yake, Wala mgeni haishiriki furaha yake. |
11. | Nyumba ya mtu mbaya itabomolewa; Bali hema ya mwenye haki itafanikiwa. |
12. | Iko njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu, Lakini mwisho wake ni njia za mauti. |
13. | Hata wakati wa kucheka moyo huwa na huzuni; Na mwisho wa furaha ni uzito wa moyo. |
14. | Ageukaye moyoni hushiba njia zake mwenyewe; Na mtu mwema ataridhika nafsini mwake. |
15. | Mjinga huamini kila neno; Bali mwenye busara huangalia sana aendavyo. |
16. | Mwenye hekima huogopa, akajitenga na uovu; Bali mpumbavu ana ufidhuli, na kujitumai. |
17. | Yeye aonaye hasira upesi atatenda kwa ujinga; Na mtu mwenye hila mbaya huzirwa. |
18. | Wajinga hurithi upumbavu; Bali wenye busara huvikwa taji ya maarifa. |
19. | Wabaya huinama mbele ya wema, Na wasio haki malangoni mwao wenye haki. |
20. | Maskini huchukiwa hata na jirani yake; Bali tajiri ana rafiki wengi. |
21. | Amdharauye mwenzake afanya dhambi; Bali amhurumiaye maskini ana heri. |
22. | Je! Hawakosi wawazao mabaya? Bali fadhili na kweli zina wao wawazao mema. |
23. | Katika kila kazi mna faida; Bali maneno ya midomo huleta hasara tu. |
24. | Taji ya wenye hekima ni mali zao; Bali upumbavu wa wajinga ni upumbavu tu. |
25. | Shahidi wa kweli huponya nafsi za watu; Bali atoaye uongo hudanganya. |
26. | Kumcha Bwana ni tumaini imara; Watoto wake watakuwa na kimbilio. |
27. | Kumcha Bwana ni chemchemi ya uzima, Ili kuepukana na tanzi za mauti. |
28. | Utukufu wa mfalme ni wingi wa watu wake; Bali uchache wa watu ni uharibifu wa mkuu wao. |
29. | Asiye mwepesi wa hasira ana fahamu nyingi; Bali mwenye roho ya hamaki hutukuza upumbavu. |
30. | Moyo ulio mzima ni uhai wa mwili; Bali husuda ni ubovu wa mifupa. |
31. | Amwoneaye maskini humsuta Muumba wake; Bali yeye awahurumiaye wahitaji humheshimu. |
32. | Mtu mbaya husukumwa chini katika kutenda mabaya kwake; Bali mwenye haki ana matumaini katika kufa kwake. |
33. | Hekima hukaa katika moyo wake mwenye ufahamu; Bali yaliyo ndani ya wapumbavu hudhihirika. |
34. | Haki huinua taifa; Bali dhambi ni aibu ya watu wo wote. |
35. | Upendeleo wa mfalme humwelekea mtumwa atendaye kwa busara; Bali ghadhabu yake itakuwa juu yake aletaye aibu. |
← Proverbs (14/31) → |