← Proverbs (13/31) → |
1. | Mwana mwenye hekima husikiliza mausia ya babaye; Bali mwenye dharau hasikilizi maonyo. |
2. | Mtu atakula mema kwa matunda ya kinywa chake; Bali nafsi ya mtu haini itakula jeuri. |
3. | Yeye alindaye kinywa chake huilinda nafsi yake; Bali afunuaye midomo yake atapata uharibifu. |
4. | Nafsi ya mtu mvivu hutamani asipate kitu; Bali nafsi ya mwenye bidii itanenepeshwa. |
5. | Mwenye haki huchukia kusema uongo; Bali mtu mbaya huwa karaha, hupatwa na aibu. |
6. | Haki humlinda yeye aliye mnyofu katika njia yake; Bali ubaya humwangusha mwenye dhambi. |
7. | Kuna mtu mwenye kujitajirisha, lakini hana kitu; Kuna ajifanyaye kuwa maskini, lakini ana mali nyingi. |
8. | Dia ya nafsi ya mtu ni utajiri wake; Bali mtu maskini hasikii ogofyo lo lote. |
9. | Nuru ya mwenye haki yang'aa sana; Bali taa ya mtu mbaya itazimika. |
10. | Kiburi huleta mashindano tu; Bali hekima hukaa nao wanaoshauriana. |
11. | Mali iliyopatikana kwa haraka itapunguka; Bali yeye achumaye kidogo kidogo atazidishiwa. |
12. | Kilichotarajiwa kikikawia kuja, moyo huugua. Bali haja ya mtu ikipatikana, ni mti wa uzima. |
13. | Kila alidharauye neno hujiletea uharibifu; Bali yeye aiogopaye amri atapewa thawabu. |
14. | Sheria ya mwenye akili ni chemchemi ya uzima, Ili kuepukana na tanzi za mauti. |
15. | Ufahamu mwema huleta upendeleo; Bali njia ya haini huparuza. |
16. | Kila aliye na busara hutenda kazi kwa maarifa; Bali mpumbavu hueneza upumbavu. |
17. | Mjumbe mbaya huanguka maovuni; Bali mjumbe mwaminifu ni afya. |
18. | Umaskini na fedheha zitampata yeye akataaye kurudiwa; Bali yeye aangaliaye maonyo ataheshimiwa. |
19. | Haja iliyopatikana ni tamu nafsini mwa mtu; Bali kujitenga na maovu ni chukizo kwa wapumbavu. |
20. | Enenda pamoja na wenye hekima, nawe utakuwa na hekima; Bali rafiki wa wapumbavu ataumia. |
21. | Uovu huwaandamia wenye dhambi; Bali mwenye haki atalipwa mema. |
22. | Mtu mwema huwaachia wana wa wanawe urithi; Na mali ya mkosaji huwa akiba kwa mwenye haki. |
23. | Chakula kingi chapatikana kwa ukulima wa maskini; Bali viko viharibiwavyo kwa sababu ya dhuluma. |
24. | Yeye asiyetumia fimbo yake humchukia mwanawe; Bali yeye ampendaye humrudi mapema. |
25. | Mwenye haki hula akaishibisha nafsi yake; Bali tumbo la mtu mbaya litaona njaa. |
← Proverbs (13/31) → |