Proverbs (12/31)  

1. Kila apendaye mafundisho hupenda maarifa; Bali yeye achukiaye kulaumiwa ni kama mnyama.
2. Mtu mwema atapata upendeleo kwa Bwana; Bali mtu wa hila atahukumiwa naye.
3. Mtu hatathibitika kwa njia ya uovu; Shina la mwenye haki halitaondolewa kamwe.
4. Mwanamke mwema ni taji ya mumewe; Bali aaibishaye ni kama kuoza mifupani mwake.
5. Mawazo ya mwenye haki ni adili; Bali mashauri ya mtu mwovu ni hadaa.
6. Maneno ya waovu huotea damu; Bali kinywa cha wanyofu kitawaokoa.
7. Waovu huangamia, hata hawako tena; Bali nyumba ya mwenye haki itasimama.
8. Mtu atasifiwa kwa kadiri ya akili zake; Bali mwenye moyo wa ukaidi atadharauliwa.
9. Afadhali mtu anayedharauliwa, ikiwa ana mtumwa, Kuliko ajisifuye, ikiwa anahitaji chakula.
10. Mwenye haki huufikiri uhai wa mnyama wake; Bali huruma za mtu mwovu ni ukatili.
11. Alimaye shamba lake atakuwa na chakula tele; Bali afuataye mambo ya upuzi hana ufahamu.
12. Asiye haki hutamani nyavu za wabaya; Bali shina lao wenye haki huleta matunda.
13. Katika kosa la midomo kuna mtego kwa mbaya; Bali mwenye haki atatoka katika taabu.
14. Mtu atashiba mema kwa matunda ya kinywa chake; Na atarudishiwa matendo ya mikono yake.
15. Njia ya mpumbavu imenyoka machoni pake mwenyewe; Bali yeye aliye na hekima husikiliza shauri.
16. Ghadhabu ya mpumbavu hujulika mara; Bali mtu mwerevu husitiri aibu.
17. Atamkaye maneno ya kweli hufunua haki; Bali shahidi wa uongo hutamka hila.
18. Kuna anenaye bila kufikiri, kama kuchoma kwa upanga; Bali ulimi wa mwenye haki ni afya.
19. Mdomo wa kweli utathibitishwa milele; Bali ulimi wa uongo ni wa kitambo tu.
20. Hila imo mioyoni mwao wafikirio uovu; Bali wafanyao mashauri ya amani, kwao kuna furaha.
21. Mwenye haki hatapatikana na msiba wo wote; Bali wasio haki watajazwa mabaya.
22. Midomo ya uongo ni chukizo kwa Bwana; Bali watendao uaminifu ndio furaha yake.
23. Mwanadamu mwenye busara husitiri maarifa; Bali moyo wa wapumbavu hutangaza upumbavu.
24. Mkono wa mwenye bidii utatawala; Bali mvivu atalipishwa kodi.
25. Uzito katika moyo wa mtu huuinamisha; Bali neno jema huufurahisha.
26. Mwenye haki ni kiongozi cha mwenzake; Bali njia ya wasio haki huwakosesha.
27. Mtu mvivu hapiki mawindo yake; Bali mwenye bidii anazo mali za thamani.
28. Katika njia ya haki kuna uhai; Wala hakuna mauti katika mapito yake.

  Proverbs (12/31)