Proverbs (11/31)  

1. Mizani ya hadaa ni chukizo kwa Bwana; Bali vipimo vilivyo sawasawa humpendeza.
2. Kijapo kiburi ndipo ijapo aibu; Bali hekima hukaa na wanyenyekevu.
3. Ukamilifu wao wenye haki utawaongoza Bali ukaidi wao wenye fitina utawaangamiza.
4. Mali hazifaidii kitu siku ya ghadhabu; Bali haki huokoa na mauti.
5. Haki yake mtu mkamilifu itamwongoza njia yake; Bali mtu mwovu ataanguka kwa uovu wake.
6. Haki yao wenye haki itawaokoa; Bali wafanyao fitina watanaswa kwa hila yao wenyewe.
7. Mtu mwovu atakapokufa, taraja lake lapotea; Na matumaini ya uovu huangamia.
8. Mwenye haki huokolewa katika dhiki, Na mtu mwovu ataiingia badala yake.
9. Asiyemcha Mungu humpoteza jirani yake kwa kinywa chake; Bali wenye haki watapona kwa maarifa.
10. Wenye haki wasitawipo, mji hufurahi; Waovu waangamiapo, watu hupiga kelele.
11. Mji hutukuzwa kwa mbaraka wa mwenye haki; Bali mji hupinduliwa kwa kinywa cha mwovu.
12. Asiye na akili humdharau mwenziwe; Bali mtu aliye na ufahamu hunyamaza.
13. Mwenye kitango akisingizia hufunua siri; Bali mwenye roho ya uaminifu husitiri mambo.
14. Pasipo mashauri taifa huanguka; Bali kwa wingi wa washauri huja wokovu.
15. Amdhaminiye mgeni hakosi ataumia; Achukiaye mambo ya dhamana yu salama.
16. Mwanamke wa adabu huheshimiwa daima; Na watu wakali hushika mali siku zote.
17. Mwenye rehema huitendea mema nafsi yake; Aliye mkali hujisumbua mwili wake.
18. Mtu mwovu hupata mshahara wa udanganyifu; Apandaye haki ana thawabu ya hakika.
19. Haki huelekea uzima; Afuataye maovu hufuata mauti yake mwenyewe.
20. Wenye kuhalifu moyoni ni chukizo kwa Bwana; Walio wakamilifu katika njia zao humpendeza.
21. Hakika, mtu mwovu hatakosa adhabu; Bali wazao wa wenye haki wataokoka.
22. Kama pete ya dhahabu katika pua ya nguruwe, Kadhalika mwanamke mzuri asiye na akili.
23. Haja ya mwenye haki ni mema tu; Bali kutaraji kwake mtu mwovu ni ghadhabu.
24. Kuna atawanyaye, lakini huongezewa zaidi; Kuna azuiaye isivyo haki, lakini huelekea uhitaji.
25. Nafsi ya mtu mkarimu itawandishwa; Anyweshaye atanyweshwa mwenyewe.
26. Awanyimaye watu nafaka, watu watamlaani; Auzaye nafaka, baraka itakuwa kichwani pake.
27. Atafutaye mema kwa bidii hutafuta fadhili; Atafutaye madhara, hayo yatamjia.
28. Azitegemeaye mali zake ataanguka; Mwenye haki atasitawi kama jani.
29. Ataabishaye nyumba yake mwenyewe ataurithi upepo; Mpumbavu atakuwa mtumwa wa mtu mwenye moyo wa akili.
30. Mazao ya mwenye haki ni mti wa uzima; Na mwenye hekima huvuta roho za watu.
31. Tazama, mwenye haki atalipwa duniani; Basi mwovu na mkosaji si mara nyingi zaidi?

  Proverbs (11/31)