Proverbs (10/31)  

1. Mwana mwenye hekima humfurahisha babaye; Bali mwana mpumbavu ni mzigo wa mamaye.
2. Hazina za uovu hazifaidii kitu; Bali haki huokoa na mauti.
3. Bwana hataiacha nafsi ya mwenye haki ife na njaa; Bali tamaa ya mtu mwovu huisukumia mbali.
4. Atendaye mambo kwa mkono mlegevu huwa maskini; Bali mkono wake aliye na bidii hutajirisha.
5. Akusanyaye wakati wa hari ni mwana mwenye hekima; Bali asinziaye wakati wa mavuno ni mwana mwenye kuaibisha.
6. Baraka humkalia mwenye haki kichwani; Bali jeuri hufunika kinywa chake mtu mwovu.
7. Kuwakumbuka wenye haki huwa na baraka; Bali jina la mtu mwovu litaoza.
8. Aliye na akili moyoni mwake atapokea agizo; Bali mpumbavu mwenye maneno mengi ataanguka.
9. Aendaye kwa unyofu huenda salama; Bali apotoshaye njia zake atajulikana.
10. Akonyezaye kwa jicho huleta masikitiko; Bali mpumbavu mwenye maneno mengi ataanguka.
11. Kinywa chake mwenye haki ni chemchemi ya uzima; Bali jeuri hufunika kinywa chake mtu mwovu,
12. Kuchukiana huondokesha fitina; Bali kupendana husitiri makosa yote.
13. Hekima hupatikana midomoni mwa mwenye ufahamu; Bali fimbo hufaa kwa mgongo wake asiye na ufahamu.
14. Watu wenye akili huweka akiba ya maarifa; Bali kinywa cha mpumbavu ni uangamivu ulio karibu.
15. Mali ya mtu tajiri ni mji wake wa nguvu; Uangamivu wa maskini ni umaskini wao.
16. Kazi yake mwenye haki huuelekea uzima; Mazao ya wabaya huuelekea dhambi.
17. Akubaliye kurudiwa huwa katika njia ya uzima; Bali yeye aachaye maonyo hukosa.
18. Yeye afichaye chuki ana midomo ya uongo, Na yeye asingiziaye ni mpumbavu.
19. Katika wingi wa maneno hapakosi kuwa na maovu; Bali yeye azuiaye midomo yake hufanya akili.
20. Ulimi wa mwenye haki ni kama fedha teule; Moyo wa mtu mbaya haufai kitu.
21. Midomo ya mwenye haki hulisha watu wengi; Bali wapumbavu hufa kwa kuwa hawana ufahamu.
22. Baraka ya Bwana hutajirisha, Wala hachanganyi huzuni nayo.
23. Kwa mpumbavu kutenda maovu ni kama mchezo; Bali mtu mwenye ufahamu ana hekima.
24. Aogopacho mtu asiye haki ndicho kitakachomjilia; Na wenye haki watapewa matakwa yao.
25. Kisulisuli kikiisha pita asiye haki hayuko tena; Bali mwenye haki ni msingi wa milele.
26. Kama siki menoni, na kama moshi machoni, Ndivyo alivyo mtu mvivu kwao wamtumao.
27. Kumcha Bwana kwaongeza siku za mtu; Bali miaka yao wasio haki itapunguzwa.
28. Matumaini yao wenye haki yatakuwa furaha; Bali kutaraji kwao wasio haki kutapotea.
29. Njia ya Bwana ni kimbilio lake mtu mkamilifu; Bali ni uharibifu kwao watendao maovu.
30. Mwenye haki hataondolewa milele; Bali wasio haki hawatakaa katika nchi.
31. Kinywa cha mwenye haki hutoa hekima; Bali ulimi wa ukaidi utakatiliwa mbali.
32. Midomo ya mwenye haki huyajua yatakayokubaliwa; Bali kinywa chao wasio haki hunena ukaidi.

  Proverbs (10/31)