Proverbs (1/31) → |
1. | Mithali za Sulemani, mwana wa Daudi, mfalme wa Israeli. |
2. | Kujua hekima na adabu; kutambua maneno ya ufahamu; |
3. | kufundishwa matendo ya busara, katika haki na hukumu na adili. |
4. | Kuwapa wajinga werevu, na kijana maarifa na hadhari; |
5. | mwenye hekima asikie na kuongezewa elimu, na mwenye ufahamu ayafikie mashauri yenye njia. |
6. | Kufahamu mithali na kitendawili, na maneno ya wenye hekima na mafumbo yao. |
7. | Kumcha Bwana ni chanzo cha maarifa, Bali wapumbavu hudharau hekima na adabu. |
8. | Mwanangu, yasikilize mafundisho ya baba yako, Wala usiiache sheria ya mama yako, |
9. | Kwa maana hayo yatakuwa kilemba cha neema kichwani pako, Na mikufu shingoni mwako. |
10. | Mwanangu, wenye dhambi wakikushawishi, Wewe usikubali. |
11. | Wakisema, Haya! Njoo pamoja nasi, Na tuvizie ili kumwaga damu; Tumwotee asiye na hatia, bila sababu; |
12. | Tuwameze hai kama kuzimu, Na wazima, kama wao washukao shimoni. |
13. | Tutapata mali yote ya thamani, Tutazijaza nyumba zetu mateka. |
14. | Wewe utashirikiana nasi; Tutakuwa na vitu vyote shirika. |
15. | Mwanangu, usiende njiani pamoja nao; Uzuie mguu wako usiende katika mapito yao. |
16. | Maana miguu yao huenda mbio maovuni, Nao hufanya haraka ili kumwaga damu. |
17. | Kwa kuwa mtego hutegwa bure, Mbele ya macho ya ndege ye yote. |
18. | Na hao hujiotea damu yao wenyewe, Hujinyemelea nafsi zao wenyewe. |
19. | Ndivyo zilivyo njia za kila mwenye tamaa ya mali; Huuondoa uhai wao walio nayo. |
20. | Hekima hupaza sauti yake katika njia kuu, Hutoa sauti yake katika viwanja; |
21. | Hulia penye mikutano mikubwa ya watu, Mahali pa kuyaingilia malango, Ndani ya mji hutamka maneno yake. |
22. | Enyi wajinga, hata lini mtapenda ujinga? Na wenye dharau kupenda dharau yao, Na wapumbavu kuchukia maarifa? |
23. | Geukeni kwa ajili ya maonyo yangu; Tazama, nitawamwagia roho yangu, Na kuwajulisheni maneno yangu. |
24. | Kwa kuwa nimeita, nanyi mkakataa; Nimeunyosha mkono wangu, asiangalie mtu; |
25. | Bali mmebatilisha shauri langu, Wala hamkutaka maonyo yangu; |
26. | Mimi nami nitacheka siku ya msiba wenu, Nitadhihaki hofu yenu ifikapo; |
27. | Hofu yenu ifikapo kama tufani, Na msiba wenu ufikapo kama kisulisuli, Dhiki na taabu zitakapowafikia. |
28. | Ndipo watakaponiita, lakini sitaitika; Watanitafuta kwa bidii, wasinione. |
29. | Kwa kuwa walichukia maarifa, Wala hawakuchagua kumcha Bwana. |
30. | Hawakukubali mashauri yangu, Wakayadharau maonyo yangu yote. |
31. | Kwa hiyo watakula matunda ya njia yao, Watashiba mashauri yao wenyewe. |
32. | Maana kurudi nyuma kwao wajinga kutawaua, Na kufanikiwa kwao wapumbavu kutawaangamiza. |
33. | Bali kila anisikilizaye atakaa salama, Naye atatulia bila kuogopa mabaya. |
Proverbs (1/31) → |