Philemon (1/1) |
1. | Paulo, mfungwa wa Kristo Yesu, na Timotheo aliye ndugu yetu, kwa Filemoni mpendwa wetu, mtenda kazi pamoja nasi, |
2. | na kwa Afia, ndugu yetu, na kwa Arkipo askari mwenzetu, na kwa kanisa lililo katika nyumba yako. |
3. | Neema na iwe kwenu, na amani, zitokazo kwa Mungu, Baba yetu, na kwa Bwana Yesu Kristo. |
4. | Namshukuru Mungu wangu sikuzote, nikikukumbuka katika maombi yangu; |
5. | nikisikia habari za upendo wako na imani uliyo nayo kwa Bwana Yesu na kwa watakatifu wote; |
6. | ili kwamba ushirika wa imani yako ufanye kazi yake, katika ujuzi wa kila kitu chema kilicho kwetu, katika Kristo. |
7. | Maana nalikuwa na furaha nyingi na faraja kwa sababu ya upendo wako, kwa kuwa mioyo ya watakatifu imeburudishwa nawe, ndugu yangu. |
8. | Kwa hiyo, nijapokuwa nina ujasiri katika Kristo kukuagiza likupasalo; |
9. | lakini, kwa ajili ya upendo nakusihi, kwa kuwa ni kama nilivyo, Paulo mzee, na sasa mfungwa wa Kristo Yesu pia. |
10. | Nakusihi kwa ajili ya mtoto wangu niliyemzaa katika vifungo vyangu, yaani, Onesimo; |
11. | ambaye zamani alikuwa hakufai, bali sasa akufaa sana, wewe na mimi pia; |
12. | niliyemtuma kwako, yeye mwenyewe, maana ni moyo wangu hasa; |
13. | ambaye mimi nalitaka akae kwangu, apate kunitumikia badala yako katika vifungo vya Injili. |
14. | Lakini sikutaka kutenda neno lo lote isipokuwa kwa shauri lako, ili kwamba wema wako usiwe kama kwa lazima, bali kwa hiari. |
15. | Maana, labda ndiyo sababu alitengwa nawe kwa muda, ili uwe naye tena milele; |
16. | tokea sasa, si kama mtumwa, bali zaidi ya mtumwa, ndugu mpendwa; kwangu mimi sana, na kwako wewe zaidi sana, katika mwili na katika Bwana. |
17. | Basi kama ukiniona mimi kuwa mshirika nawe, mpokee huyu kama mimi mwenyewe. |
18. | Na kama amekudhulumu, au unamwia kitu, ukiandike hicho juu yangu. |
19. | Mimi Paulo nimeandika kwa mkono wangu mwenyewe, mimi nitalipa. Sikuambii kwamba nakuwia hata nafsi yako. |
20. | Naam, ndugu yangu, nipate faida kwako katika Bwana; uniburudishe moyo wangu katika Kristo. |
21. | Kwa kuwa nakuamini kutii kwako ndiyo maana nimekuandikia, nikijua ya kuwa utafanya zaidi ya hayo nisemayo. |
22. | Na pamoja na hayo uniwekee tayari mahali pa kukaa; maana nataraji ya kwamba kwa maombi yenu mtajaliwa kunipata. |
23. | Epafra, aliyefungwa pamoja nami katika Kristo Yesu, akusalimu; |
24. | na Marko, na Aristarko, na Dema, na Luka, watendao kazi pamoja nami. |
25. | Neema ya Bwana Yesu Kristo na iwe pamoja na roho zenu. |
Philemon (1/1) |