Numbers (33/36)  

1. Hizi ndizo safari za wana wa Israeli, hapo walipotoka nchi ya Misri kwa jeshi zao chini ya mkono wa Musa na Haruni.
2. Musa akaandika jinsi walivyotoka katika safari zao, kwa amri ya Bwana; na hizi ndizo safari zao kama kutoka kwao kulivyokuwa.
3. Wakasafiri kutoka Ramesesi mwezi wa kwanza, siku ya kumi na tano ya mwezi wa kwanza; siku ya pili baada ya Pasaka, wana wa Israeli wakatoka kwa mkono wa nguvu mbele ya macho ya Wamisri wote,
4. hapo Wamisri walipokuwa wanazika wazaliwa wa kwanza wao wote, Bwana aliokuwa amewapiga kati yao; Bwana akafanya hukumu juu ya miungu yao nayo.
5. Wana wa Israeli wakasafiri kutoka Ramesesi, wakapanga katika Sukothi.
6. Kisha wakasafiri kutoka Sukothi, wakapanga Ethamu, palipo katika mwisho wa nyika.
7. Wakasafiri kutoka Ethamu, na kurudi nyuma hata Pi-hahirothi palipokabili Baal-sefoni; wakapanga mbele ya Migdoli.
8. Wakasafiri kutoka hapo mbele ya Hahirothi, wakapita katikati ya bahari na kuingia jangwani; kisha wakaenda safari ya siku tatu katika nyika ya Ethamu, wakapanga Mara.
9. Wakasafiri kutoka Mara, wakafikilia Elimu; huko Elimu palikuwa na chemchemi za maji kumi na mbili, na mitende sabini; nao wakapanga hapo.
10. Wakasafiri kutoka Elimu wakapanga karibu na Bahari ya Shamu.
11. Wakasafiri kutoka Bahari ya Shamu, wakapanga katika nyika ya Sini.
12. Wakasafiri kutoka nyika ya Sini, wakapanga Dofka.
13. Wakasafiri kutoka Dofka, wakapanga Alushi.
14. Wakasafiri kutoka Alushi, wakapanga Refidimu, ambapo hapakuwa na maji ya watu kunywa.
15. Wakasafiri kutoka Refidimu, wakapanga katika nyika ya Sinai.
16. Wakasafiri kutoka nyika ya Sinai, wakapanga Kibroth-hataava.
17. Wakasafiri kutoka Kibroth-hataava, wakapanga Haserothi.
18. Wakasafiri kutoka Haserothi, wakapanga Rithma.
19. Wakasafiri kutoka Rithma, wakapanga Rimon-peresi.
20. Wakasafiri kutoka Rimon-peresi, wakapanga Libna.
21. Wakasafiri kutoka Libna, wakapanga Risa.
22. Wakasafiri kutoka Risa, wakapanga Keheletha.
23. Wakasafiri kutoka Keheletha, wakapanga katika mlima wa Sheferi
24. Wakasafiri kutoka huo mlima wa Sheferi, wakapanga Harada.
25. Wakasafiri kutoka Harada, wakapanga Makelothi.
26. Wakasafiri kutoka Makelothi, wakapanga Tahathi.
27. Wakasafiri kutoka Tahathi wakapanga Tera.
28. Wakasafiri kutoka Tera, wakapanga Mithka.
29. Wakasafiri kutoka Mithka, wakapanga Hashmona.
30. Wakasafiri kutoka Hashmona, wakapanga Moserothi.
31. Wakasafiri kutoka Moserothi, wakapanga Bene-yakani.
32. Wakasafiri kutoka Bene-yakani, wakapanga Hor-hagidgadi.
33. Wakasafiri kutoka Hor-hagidgadi, wakapanga Yotbatha.
34. Wakasafiri kutoka Yotbatha, wakapanga Abrona.
35. Wakasafiri kutoka Abrona, wakapanga Esion-geberi.
36. Wakasafiri kutoka Esion-geberi, wakapanga katika nyika ya Sini (ni Kadeshi).
37. Wakasafiri kutoka Kadeshi wakapanga katika mlima wa Hori, katika mpaka wa nchi ya Edomu,
38. Haruni akakwea mlima wa Hori, kwa amri ya Bwana, akafa hapo, katika mwaka wa arobaini baada ya wana wa Israeli kutoka katika nchi ya Misri, mwezi wa tano, siku ya kwanza ya mwezi.
39. Naye Haruni alikuwa mtu wa umri wa miaka mia na ishirini na mitatu hapo alipokufa katika mlima wa Hori.
40. Ndipo Mkanaani, mfalme wa Aradi, aliyekaa pande za Negebu katika nchi ya Kanaani akasikia habari za kuja kwao wana wa Israeli.
41. Nao wakasafiri kutoka mlima wa Hori, wakapanga Salmona.
42. Wakasafiri kutoka Salmona, wakapanga Punoni.
43. Wakasafiri kutoka Punoni, wakapanga Obothi.
44. Wakasafiri kutoka Obothi, wakapanga Iye-abarimu, katika mpaka wa Moabu.
45. Wakasafiri kutoka Iye-abarimu, wakapanga Dibon-gadi.
46. Wakasafiri kutoka Dibon-gadi, wakapanga Almon-diblathaimu.
47. Wakasafiri kutoka Almon-diblathaimu, wakapanga katika milima ya Abarimu, kukabili Nebo.
48. Wakasafiri kutoka hiyo milima ya Abarimu, wakapanga katika nchi tambarare za Moabu, karibu na mto wa Yordani, hapo Yeriko.
49. Wakapanga karibu na Yordani, tangu Beth-yeshimothi hata kufikilia Abel-shitimu katika nchi tambarare za Moabu.
50. Kisha Bwana akanena na Musa hapo katika nchi tambarare za Moabu, karibu na Yordani, hapo Yeriko, na kumwambia,
51. Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Mtakapovuka mto wa Yordani na kuingia nchi ya Kanaani,
52. ndipo mtakapowafukuza wenyeji wote wa hiyo nchi mbele yenu, nanyi mtayaharibu mawe yao yote yenye kuchorwa sanamu, na kuziharibu sanamu zao zote za kusubu, kuvunja-vunja mahali pao pote palipoinuka;
53. nanyi mtaishika hiyo nchi kuimiliki na kuketi humo; kwa kuwa mimi nimewapa ninyi hiyo nchi ili mwimiliki.
54. Nanyi mtairithi nchi kwa kufanya kura, kama jamaa zenu zilivyo; hao walio wengi mtawapa urithi zaidi, na hao waliopunguka utawapa kama kupunguka kwao; mahali po pote kura itakapomwangukia mtu ye yote, mahali hapo ni pake; mtarithi kama kabila za baba zenu zilivyo.
55. Lakini kama hamtaki kuwafukuza wenyeji wa nchi watoke mbele yenu; ndipo hao ambao mtakaowasaza watakuwa kama sindano machoni mwenu, na kama miiba ubavuni mwenu, nao watawasumbua katika hiyo nchi ambayo mwakaa.
56. Kisha itakuwa, kama nilivyoazimia kuwatenda wao, ndivyo nitakavyowatenda ninyi.

  Numbers (33/36)