| ← Numbers (30/36) → | 
| 1. | Kisha Musa akanena na wale vichwa vya kabila za wana wa Israeli, na kuwaambia, Neno hili ndilo aliloliagiza Bwana. | 
| 2. | Mtu atakapomwekea Bwana nadhiri, au, atakapoapa kiapo ili kufunga nafsi yake kwa kifungo, asilitangue neno lake; atafanya sawasawa na hayo yote yamtokayo kinywani mwake. | 
| 3. | Tena mtu mke atakapomwekea Bwana nadhiri, na kufunga nafsi yake kwa kifungo, naye aketi katika nyumba ya babaye, katika ujana wake; | 
| 4. | babaye naye akasikia nadhiri yake, na kile kifungo chake alichofungia nafsi yake, na babaye akamnyamazia; ndipo nadhiri zake zote zitathibitika, na kila kifungo alichofungia nafsi yake kitathibitika. | 
| 5. | Lakini kama huyo babaye akimkataza siku hiyo aliyosikia; nadhiri zake ziwazo zote, wala vifungo vyake alivyoifungia nafsi yake havitathibitika; na Bwana atamsamehe, kwa kuwa babaye alimkataza. | 
| 6. | Tena kama amekwisha kuolewa na mume, wakati huo wa nadhiri zake, au wa neno hilo alilolitamka kwa midomo yake pasipo kufikiri, alilojifungia; | 
| 7. | na mumewe akasikia, naye akamnyamazia siku hiyo aliyosikia neno hilo; ndipo nadhiri zake zitathibitika, na vile vifungo ambavyo ameifunga nafsi yake vitathibitika. | 
| 8. | Lakini kama mumewe akimkataza siku hiyo aliyolisikia; ndipo ataitangua nadhiri yake iliyo juu yake na neno alilolitamka kwa midomo yake pasipo kufikiri, alilojifungia; na Bwana atamsamehe | 
| 9. | Lakini nadhiri ya mjane, au ya mwanamke aliyeachishwa mume, kila neno ambalo ameifunga nafsi yake kwalo, litathibitika juu yake. | 
| 10. | Tena kama aliweka nadhiri nyumbani mwa mumewe, au kama aliifunga nafsi yake kwa kifungo pamoja na kiapo, | 
| 11. | na mumewe alisikia akamnyamazia, wala hakumkataza; ndipo nadhiri zake zote zitathibitika, na kila kifungo alichojifungia kitathibitika. | 
| 12. | Lakini kama mumewe alizibatilisha na kuzitangua siku hiyo aliyozisikia, ndipo kila neno lililotoka midomoni mwake katika hizo nadhiri zake, au katika kile kifungo cha nafsi yake, halitathibitika; huyo mumewe amezitangua; na Bwana atamsamehe. | 
| 13. | Kila nadhiri, na kila kiapo kifungacho, ili kuitaabisha nafsi ya mwanamke mumewe aweza kuthibitisha, au mumewe aweza kutangua. | 
| 14. | Lakini mumewe akimnyamazia mkewe kabisa siku hata siku ndipo azithibitisha nadhiri zote za mkewe, au vifungo vyake vyote vilivyo juu yake; yeye amezithibitisha, kwa kuwa alimnyamazia mkewe siku hiyo aliyozisikia nadhiri zake. | 
| 15. | Lakini akizibatilisha na kuzitangua baada ya kuzisikia; ndipo yeye atachukua uovu wa mkewe. | 
| 16. | Hizi ndizo amri, ambazo Bwana alimwagiza Musa, kati ya mtu mume na mkewe, kati ya baba na binti yake, katika ujana wake, ali nyumbani mwa babaye. | 
| ← Numbers (30/36) → |