| ← Numbers (23/36) → |
| 1. | Balaamu akamwambia Balaki, Nijengee hapa madhabahu saba, ukaniandalie hapa ng'ombe waume saba, na kondoo waume saba. |
| 2. | Balaki akafanya kama Balaamu alivyonena. Balaki na Balaamu wakatoa sadaka, ng'ombe mume mmoja na kondoo mume mmoja juu ya kila madhabahu. |
| 3. | Balaamu akamwambia Balaki, Simama karibu na sadaka yako, nami nitakwenda, labda Bwana atakuja kuonana nami; na lo lote atakalonionyesha nitakuambia. Akaenda hata mahali peupe juu ya kilima. |
| 4. | Mungu akakutana na Balaamu; naye Balaamu akamwambia, Nimetengeneza madhabahu saba, nami nimetoa sadaka ng'ombe mume mmoja na kondoo mume mmoja juu ya kila madhabahu. |
| 5. | Bwana akatia neno katika kinywa chake Balaamu, akasema, Umrudie Balaki; ukaseme maneno haya. |
| 6. | Akarudi kwake, na tazama, amesimama karibu na sadaka yake ya kuteketezwa, yeye na wakuu wote wa Moabu pamoja naye. |
| 7. | Akatunga mithali yake, akasema, Balaki amenileta kutoka Aramu, Mfalme wa Moabu kutoka milima ya mashariki, Njoo! Unilaanie Yakobo, Njoo! Unishutumie Israeli. |
| 8. | Nimlaanije, yeye ambaye Mungu hakumlaani? Nimshutumuje, yeye ambaye Bwana hakumshutumu? |
| 9. | Kutoka kilele cha majabali namwona; Na kutoka milimani namtazama; Angalia, ni watu wakaao peke yao, Wala hawatahesabiwa pamoja na mataifa. |
| 10. | Ni nani awezaye kufanya idadi ya mavumbi ya Yakobo, Au kuhesabu robo ya Israeli? Na nife kifo chake mwenye haki, Na mwisho wangu uwe mfano wa mwisho wake. |
| 11. | Balaki akamwambia Balaamu, Umenitendea nini? Nimekuleta ili Uwalaani adui zangu, na tazama, umewabariki kabisa kabisa. |
| 12. | Naye akajibu, akasema, Je! Hainipasi kuangalia, niseme neno lile Bwana atialo kinywani mwangu? |
| 13. | Balaki akamwambia, Haya! Njoo, tafadhali, hata mahali pengine, na kutoka huko utaweza kuwaona; utaona upande wa mwisho wao tu, wala hutawaona wote, ukanilaanie hao kutoka huko. |
| 14. | Akamchukua mpaka shamba la Sofimu, hata kilele cha Pisga, akajenga madhabahu saba, akatoa sadaka ng'ombe mume mmoja na kondoo mume mmoja juu ya kila madhabahu. |
| 15. | Akamwambia Balaki, Simama hapa karibu na sadaka yako ya kuteketezwa, nami nitaonana na Bwana kule. |
| 16. | Bwana akaonana na Balaamu akatia neno kinywani mwake, akasema, Umrudie Balaki, ukaseme hivi. |
| 17. | Akafika kwake, na tazama, amesimama karibu na sadaka yake ya kuteketezwa, na wakuu wa Moabu pamoja naye. Balaki akamwambia, Bwana amenena nini? |
| 18. | Naye akatunga mithali yake, akasema, Ondoka Balaki, ukasikilize; Nisikilize, Ee mwana wa Sipori; |
| 19. | Mungu si mtu, aseme uongo; Wala si mwanadamu, ajute; Iwapo amesema, hatalitenda? Iwapo amenena, hatalifikiliza? |
| 20. | Tazama, nimepewa amri kubariki, Yeye amebariki, nami siwezi kulitangua. |
| 21. | Hakutazama uovu katika Yakobo, Wala hakuona ukaidi katika Israeli. Bwana, Mungu wake, yu pamoja naye, Na sauti kuu ya mfalme i katikati yao. |
| 22. | Mungu amewaleta kutoka Misri, Naye ana nguvu kama nguvu za nyati. |
| 23. | Hakika hapana uchawi juu ya Yakobo, Wala hapana uganga juu ya Israeli. Sasa habari za Yakobo na Israeli zitasemwa, Ni mambo gani aliyoyatenda Mungu! |
| 24. | Tazama, watu hawa wanaondoka kama simba mke, Na kama simba anajiinua nafsi yake, Hatalala hata atakapokula mawindo, Na kunywa damu yao waliouawa. |
| 25. | Balaki akamwambia Balaamu, Basi usiwalaani kabisa, wala usiwabariki kabisa. |
| 26. | Lakini Balaamu akajibu akamwambia Balaki, Je! Sikukuambia ya kwamba, Kila neno Bwana atakalolisema sina budi kulitenda? |
| 27. | Kisha Balaki akamwambia Balaamu, Haya, njoo sasa, nikupeleke mahali pengine; labda Mungu ataridhia kwamba unilaanie watu hao huko. |
| 28. | Basi Balaki akamchukua Balaamu akaenda naye mpaka kilele cha mlima Peori, mahali paelekeapo upande wa nyika iliyo chini yake. |
| 29. | Balaamu akamwambia Balaki, Haya, unijengee hapa madhabahu saba, kisha uniandalie ng'ombe waume saba, na kondoo waume saba. |
| 30. | Basi Balaki akafanya kama Balaamu alivyosema, akasongeza sadaka ng'ombe mume na kondoo mume juu ya kila madhabahu. |
| ← Numbers (23/36) → |