← Numbers (21/36) → |
1. | Na Mkanaani, mfalme wa Aradi, aliyeketi upande wa Negebu, alisikia habari ya kuwa Israeli alikuja kwa njia ya Atharimu; basi akapigana na Israeli, na watu kadha wa kadha miongoni mwao akawateka mateka. |
2. | Basi Israeli akaweka nadhiri kwa Bwana akasema, Kama wewe utawatia watu hawa mikononi mwangu kweli ndipo mimi nitaiharibu miji yao kabisa. |
3. | Bwana akasikiza sauti ya Israeli, akawatia Wakanaani mikononi mwao; nao wakawaharibu wao na miji yao kabisa; na jina la mahali hapo likaitwa Horma. |
4. | Wakasafiri kutoka mlima wa Hori kwa njia ya Bahari ya Shamu; ili kuizunguka nchi ya Edomu, watu wakafa moyo kwa sababu ya ile njia. |
5. | Watu wakamnung'unikia Mungu, na Musa, Mbona mmetupandisha huku kutoka nchi ya Misri, ili tufe jangwani? Maana hapana chakula, wala hapana maji, na roho zetu zinakinai chakula hiki dhaifu. |
6. | Bwana akatuma nyoka za moto kati ya watu, wakawauma, watu wengi wakafa. |
7. | Watu wakamwendea Musa, wakasema, Tumefanya dhambi kwa sababu tumemnung'unikia Mungu, na wewe; utuombee kwa Bwana, atuondolee nyoka hawa. Basi Musa akawaombea watu. |
8. | Bwana akamwambia Musa, Jifanyie nyoka ya shaba, ukaiweke juu ya mti, na itakuwa kila mtu aliyeumwa, aitazamapo ataishi. |
9. | Musa akafanya nyoka ya shaba, akaiweka juu ya mti, hata ikiwa nyoka amemwuma mtu, alipoitazama ile nyoka ya shaba, akaishi. |
10. | Kisha wana wa Israeli wakasafiri, wakapanga marago Obothi. |
11. | Wakasafiri kutoka Obothi, wakapanga Iye-abarimu, katika jangwa iliyoelekea Moabu, upande wa maawio ya jua. |
12. | Kutoka huko wakasafiri, wakapanga katika bonde la Zeredi. |
13. | Kutoka huko wakasafiri, wakapanga upande wa pili wa Arnoni, ulio jangwani, utokao katika mpaka wa Waamori; maana, Arnoni ndio mpaka wa Moabu, kati ya Moabu na Waamori. |
14. | Kwa hiyo imesemwa katika chuo cha Vita vya Bwana, Wahebu katika Sufa, Na bonde za Arnoni, |
15. | Na matelemko ya hizo bonde Kwenye kutelemkia maskani ya Ari, Na kutegemea mpaka wa Moabu. |
16. | Kutoka huko wakasafiri kwenda Beeri; ni kisima ambacho Bwana alimwambia Musa, Uwakutanishe watu, nami nitawapa maji. |
17. | Ndipo Israeli wakaimba wimbo huu; Bubujika Ee kisima; kiimbieni; |
18. | Kisima walichokichimba wakuu, Ambacho wakuu wa watu wakakifukua, Kwa fimbo za enzi, kwa fimbo zao. |
19. | na kutoka Matana wakaenda Nahalieli; na kutoka Nahalieli wakaenda Bamothi; |
20. | na kutoka Bamothi wakaenda bondeni kwenye konde la Moabu, hata kilele cha Pisga, kielekeacho chini jangwani. |
21. | Kisha Israeli akatuma wajumbe kumwendea Sihoni mfalme wa Waamori, na kusema, |
22. | Nipe ruhusa nipite katika nchi yako; hatutageuka kando kwenda mashambani, wala kuingia katika mashamba ya mizabibu hatutakunywa maji ya visimani; tutakwenda kwa njia kuu ya mfalme, hata tutakapokuwa tumepita mpaka wako. |
23. | Lakini Sihoni hakukubali kumwacha Israeli kupita katika mpaka wake; bali Sihoni akawakutanisha watu wake wote, akatoka aende kupigana na Israeli jangwani, akafika mpaka Yahasa; akapigana na Israeli. |
24. | Israeli wakampiga kwa makali ya upanga, na kuimiliki nchi yake, tangu mto wa Arnoni hata mto wa Yaboki, mpaka nchi ya wana wa Amoni; kwa kuwa mpaka wa wana wa Amoni ulikuwa una nguvu. |
25. | Basi Israeli wakaitwaa miji hiyo yote; Israeli wakakaa katika miji yote ya Waamori, katika Heshboni, na miji yake yote. |
26. | Kwa kuwa Heshboni ulikuwa ni mji wa Sihoni mfalme wa Waamori, aliyekuwa akipigana na mfalme wa Moabu wa mbele, na kumpokonya nchi yake yote mkononi mwake, mpaka mto wa Arnoni. |
27. | Kwa hiyo, hao wanenao kwa mithali wasema, Njoni Heshboni, Mji wa Sihoni na ujengwe na kuthibitishwa; |
28. | Maana, moto umetoka Heshboni, Umekuwa Ari ya Moabu, Mwali wa moto umetoka mji wa Sihoni; Wakuu wa mahali palipoinuka Arnoni |
29. | Ole wako Moabu! Umeangamia, enyi watu wa Kemoshi; Amewatoa wanawe kuwa wakimbizi, Na binti zake waende utumwani, Wamwendee Sihoni mfalme wa Waamori. |
30. | Tumewapigia mishale; Heshboni umepotea mpaka Diboni, Nasi tumeharibu mpaka Nofa, Ifikiliayo Medeba. |
31. | Basi hivyo Israeli akaketi katika nchi ya Waamori. |
32. | Kisha Musa akapeleka watu ili kupeleleza Yazeri, nao wakaitwaa miji yake, wakawafukuza Waamori waliokuwamo. |
33. | Kisha wakageuka na kukwea kwa njia ya Bashani; na Ogu mfalme wa Bashani akaondoka apigane nao huko Edrei, yeye na watu wake wote. |
34. | Bwana akamwambia Musa, Usimche; kwa kuwa nimekwisha mtia mkononi mwako, na watu wake wote, na nchi yake; nawe utamtenda kama ulivyomtenda Sihoni mfalme wa Waamori, aliyeketi Heshboni. |
35. | Basi wakampiga, na wanawe, na watu wake wote, hata wasisaze kwake mtu ye yote; nao wakaimiliki nchi yake. |
← Numbers (21/36) → |