| ← Nehemiah (13/13) |
| 1. | Siku hiyo walisoma katika kitabu cha Musa masikioni mwa watu; na ndani yake yalionekana maneno haya yameandikwa, ya kwamba Mwamoni na Mmoabi wasiingie katika kusanyiko la Mungu milele; |
| 2. | kwa sababu hawakuwalaki wana wa Israeli kwa chakula na maji, bali walimwajiri Balaamu juu yao ili awalaani; lakini Mungu aliigeuza ile laana kuwa baraka. |
| 3. | Ikawa walipoisikia torati, wakawatenga Israeli na umati wa watu waliochanganyika nao. |
| 4. | Na kabla ya hayo, Eliashibu, kuhani, aliyewekwa avisimamie vyumba vya nyumba ya Mungu wetu, kwa kuwa alikuwa karibu yake Tobia, |
| 5. | alikuwa amemtengenezea chumba kikubwa, hapo walipoweka zamani sadaka za unga, na ubani, na vyombo, na zaka za nafaka, na divai, na mafuta, walivyoamriwa kuwapa Walawi, na waimbaji, na mabawabu; tena sadaka za kuinuliwa zilizokuwa za makuhani. |
| 6. | Lakini wakati huo wote mimi sikuwako huko Yerusalemu; maana katika mwaka wa thelathini na mbili wa Artashasta, mfalme wa Babeli, nalimrudia mfalme; na baada ya siku kadha wa kadha nikaomba ruhusa tena kwa mfalme. |
| 7. | Nami nikaja Yerusalemu, nikafahamu yale mabaya, ambayo Eliashibu ameyatenda kwa ajili ya Tobia, kwa kumtengenezea chumba katika nyua za nyumba ya Mungu. |
| 8. | Nami nikasikitika sana; basi nikavitupa nje vyombo vyote vya Tobia vitoke humo chumbani. |
| 9. | Kisha nikatoa amri, nao wakavisafisha vyumba; nami nikavirudisha humo vyombo vya nyumba ya Mungu, pamoja na sadaka za unga na ubani. |
| 10. | Tena nikaona ya kwamba Walawi hawakupewa sehemu zao; basi wamekimbia Walawi na waimbaji, waliofanya kazi, kila mtu shambani kwake. |
| 11. | Ndipo nikagombana na mashehe, nikasema, Mbona nyumba ya Mungu imeachwa? Kisha nikawakusanya, nikawaweka mahali pao. |
| 12. | Ndipo Yuda wote walipoleta zaka za nafaka, na mvinyo, na mafuta, kwenye hazina. |
| 13. | Nami nikawaweka watunza hazina juu ya hazina, yaani, Shelemia kuhani, na Sadoki mwandishi, na wa Walawi, Pedaya; na wa pili wao alikuwa Hanani, mwana wa Zakuri, mwana wa Matania; kwani walihesabiwa kuwa waaminifu, na ilikuwa juu yao kuwagawia ndugu zao. |
| 14. | Unikumbukie hayo, Ee Mungu wangu, wala usifute fadhili zangu nilizozitenda kwa ajili ya nyumba ya Mungu wangu, na kwa taratibu zake. |
| 15. | Siku hizo naliona katika Yuda watu wengine waliokanyaga mashinikizo ya mvinyo siku ya sabato, na wengine waliochukua miganda, na kuwapakia punda zao; tena na mvinyo, na zabibu, na tini, na namna zote za mizigo, waliyoileta Yerusalemu, siku ya sabato; nami nikashuhudia juu yao siku ile waliyouza vyakula. |
| 16. | Tena wakakaa humo watu wa Tiro, walioleta samaki, na biashara za kila namna, wakawauzia wana wa Yuda siku ya sabato, na mumo humo Yerusalemu. |
| 17. | Ndipo nikagombana na wakuu wa Yuda, nikawaambia, Ni neno baya gani hili mnalofanya ninyi, na kuinajisi siku ya sabato? |
| 18. | Je! Sivyo hivyo walivyofanya baba zenu; na Mungu wetu, je! Hakuyaleta mabaya haya yote juu yetu, na juu ya mji huu? Nanyi hata hivyo mwazidi kuleta ghadhabu juu ya Israeli kwa kuinajisi sabato! |
| 19. | Ikawa malango ya Yerusalemu yalipoanza kuwa na giza kabla ya sabato, naliamuru milango ifungwe, nikaamuru isifunguliwe hata sabato iishe; na baadhi ya watumishi wangu nikawaweka juu ya malango, ili usiingizwe mzigo wo wote siku ya sabato. |
| 20. | Basi wenye biashara na wachuuzi wa bidhaa za kila namna wakalala nje ya Yerusalemu mara mbili tatu. |
| 21. | Ndipo nikawashuhudia, nikawaambia, Mbona mwalala mbele ya ukuta? Mkitenda hivi tena, nitawakamata. Tangu wakati ule hawakuja tena siku ya sabato. |
| 22. | Kisha nikawaamuru Walawi wajitakase, nao waje kuyalinda malango, ili kuitakasa siku ya sabato. Unikumbukie hayo nayo, Ee Mungu wangu, ukaniachilie sawasawa na wingi wa rehema zako. |
| 23. | Tena siku zizo hizo nikawaona wale Wayahudi waliokuwa wameoa wanawake wa Ashdodi, na Amoni, na Moabu; |
| 24. | na watoto wao wakanena nusu kwa lugha ya Ashdodi, wala hawakuweza kunena kwa Kiyahudi, bali kwa lugha ya watu hao mojawapo. |
| 25. | Nikagombana nao, nikawalaani, nikawapiga baadhi yao, na kuwang'oa nywele zao; nikawaapisha kwa Mungu, nikasema, Msiwaoze wana wao binti zenu, wala msiwatwae binti zao ili waolewe na wana wenu, wala na ninyi wenyewe. |
| 26. | Je! Sulemani, mwana wa Daudi, hakufanya dhambi kwa kutenda hayo? Lakini katika mataifa mengi hapakuwa na mfalme mwingine mfano wake. Tena alipendwa na Mungu wake, naye Mungu akamfanya mfalme juu ya Israeli; walakini wanawake wageni walimkosesha hata yeye. |
| 27. | Basi, na sisi, je! Tuwasikilize ninyi kutenda neno hili baya, hata kumhalifu Mungu wetu kwa kuwaoa wanawake wageni? |
| 28. | Na mwana mmoja wa Yoyada, mwana wa Eliashibu, kuhani mkuu, alikuwa mkwewe Sanbalati, Mhoroni, basi nikamfukuza kwangu. |
| 29. | Uwakumbuke, Ee Mungu wangu, jinsi walivyounajisi ukuhani, na agano la ukuhani na la Walawi. |
| 30. | Hivyo nikawatakasa na kila kitu kigeni, nami nikawaagizia zamu makuhani na Walawi, kila mtu kazini mwake; |
| 31. | na matoleo ya kuni nyakati zilizoamriwa, na malimbuko. Nikumbuke, Ee Mungu wangu, ili unitendee mema. |
| ← Nehemiah (13/13) |