Micah (7/7)    

1. Ole wangu! Maana mimi ni kama hapo walipokwisha kuyachuma matunda ya wakati wa hari, kama zabibu zichumwazo baada ya mavuno; hapana shada la kuliwa; roho yangu inatamani tini iivayo kwanza.
2. Mtu amchaye Mungu ametoweka, asionekane katika nchi, wala hapana mtu mwenye adili katika wanadamu; wote huotea ili kumwaga damu; kila mtu humwinda ndugu yake kwa wavu.
3. Mikono yao inayashika mabaya wayatende kwa bidii; mtu mkuu aomba rushwa, kadhi yu tayari kuipokea; mtu mkubwa hunena madhara yaliyomo rohoni mwake; hivyo ndivyo wayafumavyo hayo pamoja.
4. Mtu aliye mwema miongoni mwao ni kama mbigili; mtu aliye mwenye adili miongoni mwao ni mbaya kuliko boma la michongoma; hiyo siku ya walinzi wako, yaani, siku ya kujiliwa kwako, imefika; sasa kutatokea kufadhaika kwao.
5. Msimwamini rafiki, msimwekee kiongozi tumaini; ilinde milango ya midomo ya kinywa chako ili mkeo alalaye kifuani mwako asijue habari.
6. Kwa maana mwana humwaibisha babaye, na binti huondoka ashindane na mamaye; na mwanamke aliyeolewa hushindana na mavyaaye; adui za mtu ni watu wa nyumbani mwake mwenyewe.
7. Lakini mimi, nitamtazamia Bwana; nitamngojea Mungu wa wokovu wangu; Mungu wangu atanisikia.
8. Usifurahi juu yangu, Ee adui yangu; niangukapo, nitasimama tena; nikaapo gizani, Bwana atakuwa nuru kwangu.
9. Nitaivumilia ghadhabu ya Bwana, kwa kuwa nimemwasi; hata atakaponitetea teto langu, na kunifanyia hukumu; atanileta nje kwenye nuru, nami nitaiona haki yake.
10. Ndipo adui yangu ataliona jambo hilo, na aibu itamfunika, yeye aliyeniambia, Yuko wapi Bwana, Mungu wako? Macho yangu yatamtazama; sasa atakanyagwa kama matope ya njia kuu.
11. Ni siku ya kujengwa kuta zako! Siku hiyo mpaka utasongezwa mbali.
12. Siku hiyo watakujia kutoka Ashuru na miji ya Misri, na kutoka Misri mpaka huo Mto, na kutoka bahari hii mpaka bahari hii, na kutoka mlima huu mpaka mlima huu.
13. Hata hivyo nchi itakuwa ukiwa kwa sababu ya hao wakaao ndani yake, kwa sababu ya matunda ya matendo yao.
14. Walishe watu wako kwa fimbo yako, kundi la urithi wako, wakaao peke yao, mwituni katikati ya Karmeli; na walishe katika Bashani na Gileadi, kama siku za kale.
15. Kama katika siku zile za kutoka kwako katika nchi ya Misri nitamwonyesha mambo ya ajabu.
16. Mataifa wataona, na kuzitahayarikia nguvu zao zote; wataweka mikono yao juu ya vinywa vyao, masikio yao yatakuwa na uziwi.
17. Watayaramba mavumbi kama nyoka, kama vitu vitambaavyo juu ya nchi watatoka katika mahali walimojificha, wakitetemeka; watakuja kwa Bwana, Mungu wetu, kwa hofu, nao wataogopa kwa sababu yako.
18. Ni nani aliye Mungu kama wewe, mwenye kusamehe uovu, na kuliachilia kosa la watu wa urithi wake waliosalia? Hashiki hasira yake milele, kwa maana yeye hufurahia rehema.
19. Atarejea na kutuhurumia; atayakanyaga maovu yetu; nawe utazitupa dhambi zao zote katika vilindi vya bahari.
20. Wewe utamtimilizia Yakobo kweli yako, na Ibrahimu rehema zako, ulizowaapia baba zetu tangu siku za kale.

  Micah (7/7)