Micah (5/7)  

1. Sasa utajikusanya vikosi vikosi, Ee binti wa vikosi; yeye amemhusuru; watampiga mwamuzi wa Israeli shavuni mwake kwa fimbo.
2. Bali wewe, Bethlehemu Efrata, uliye mdogo kuwa miongoni mwa elfu za Yuda; kutoka kwako wewe atanitokea mmoja atakayekuwa mtawala katika Israeli; ambaye matokeo yake yamekuwa tangu zamani za kale, tangu milele.
3. Kwa sababu hiyo atawatoa, hata wakati wa kuzaa kwake aliye na utungu; ndipo hayo mabaki ya nduguze watawarudia wana wa Israeli.
4. Naye atasimama, na kulisha kundi lake kwa nguvu za Bwana, kwa enzi ya jina la Bwana, Mungu wake; nao watakaa; maana sasa atakuwa mkuu hata miisho ya dunia.
5. Na mtu huyu atakuwa amani yetu; wakati Mwashuri atakapoingia katika nchi yetu, na kuyakanyaga majumba yetu, hapo mtaondokesha wachungaji saba juu yake, na wakuu wanane.
6. Nao wataiharibu nchi ya Ashuru kwa upanga, na nchi ya Nimrodi katika malango yake; naye atatuokoa na Mwashuri, atakapoingia katika nchi yetu, na kukanyaga ndani ya mipaka yetu.
7. Na hayo mabaki ya Yakobo yatakuwa kati ya kabila nyingi mfano wa umande utokao kwa Bwana, mfano wa manyunyu katika manyasi; yasiyomngojea mtu, wala kuwakawilia wanadamu.
8. Na hayo mabaki ya Yakobo yatakuwa kati ya mataifa, kati ya kabila nyingi, mfano wa simba kati ya wanyama wa msituni, kama mwana-simba kati ya makundi ya kondoo, ambaye, akiwa anapita katikati, hukanyaga-kanyaga na kurarua-rarua, wala hakuna wa kuokoa.
9. Mkono wako na uinuliwe juu ya adui zako, na adui zako wote wakauliwe mbali.
10. Kisha itakuwa katika siku hiyo, asema Bwana, nitawakatilia mbali farasi zako watoke kati yako, nami nitayaharibu magari yako ya vita;
11. nami nitaikatilia mbali miji ya nchi yako, na ngome zako zote nitaziangusha;
12. nami nitakatilia mbali uchawi, usiwe mkononi mwako; wala hutakuwa tena na watu wenye kutabana;
13. nami nitakatilia mbali sanamu zako na nguzo zako, zitoke kati yako; wala hutaiabudu tena kazi ya mikono yako.
14. Nami nitayang'oa maashera yenu, yasiwe kati yako; nami nitaiangamiza miji yako.
15. Nami nitajilipiza kisasi katika hasira na ghadhabu juu ya mataifa wasiosikiliza.

  Micah (5/7)