Micah (4/7)  

1. Lakini itakuwa katika siku za mwisho, ya kwamba mlima wa nyumba ya Bwana utawekwa imara juu ya milima, nao utainuliwa juu ya vilima; na watu wa mataifa watauendea makundi makundi.
2. Na mataifa mengi watakwenda na kusema, Njoni, twende juu mlimani kwa Bwana, na nyumbani kwa Mungu wa Yakobo; naye atatufundisha njia zake, nasi tutakwenda katika mapito yake; kwa maana katika Sayuni itatoka sheria, na neno la Bwana litatoka Yerusalemu.
3. Naye atafanya hukumu kati ya watu wa kabila nyingi, naye atawakemea mataifa wenye nguvu walio mbali; nao watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu; taifa halitainua upanga juu ya taifa lingine, wala hawatajifunza vita tena kamwe.
4. Bali wataketi kila mtu chini ya mzabibu wake, na chini ya mtini wake; wala hapana mtu atakayewatia hofu; kwa kuwa kinywa cha Bwana wa majeshi kimesema hivi.
5. Kwa maana mataifa yote watakwenda, kila moja kwa jina la mungu wake, na sisi tutakwenda kwa jina la Bwana, Mungu wetu, milele na milele.
6. Katika siku ile, asema Bwana, nitamkusanya yeye achechemeaye, nami nitamrudisha yeye aliyefukuzwa, na yeye niliyemtesa.
7. Nami nitamfanya yeye aliyechechemea kuwa mabaki, na yeye aliyetupwa mbali kuwa taifa lenye nguvu, na Bwana atawamiliki katika mlima Sayuni tangu sasa na hata milele.
8. Na wewe, Ee mnara wa kundi, kilima cha binti Sayuni, utajiliwa; naam, mamlaka ya kwanza yatakuja, ufalme wa binti Yerusalemu.
9. Sasa mbona unapiga kelele? Je! Hakuna mfalme kwako, mshauri wako amepotea, hata umeshikwa na utungu kama mwanamke wakati wa kuzaa?
10. Uwe na utungu, utaabike ili uzae, Ee binti Sayuni, kama mwanamke mwenye utungu; maana sasa utatoka mjini, nawe utakaa katika mashamba; utafika hata Babeli; huko ndiko utakakookolewa; huko ndiko Bwana atakakokukomboa katika mikono ya adui zako.
11. Na sasa mataifa mengi wamekusanyika juu yako, wasemao, Na atiwe unajisi; macho yetu na yaone shari ya Sayuni.
12. Lakini wao hawayajui mawazo ya Bwana, wala hawafahamu shauri lake; kwa maana amewakusanya kama miganda sakafuni.
13. Haya, simama upure, Ee binti Sayuni; kwa maana nitafanya pembe yako kuwa chuma, na kwato zako kuwa shaba; nawe utaponda-ponda mataifa mengi, na faida yao utaiweka wakfu kwa Bwana, na mali zao kwa Bwana wa dunia yote.

  Micah (4/7)