← Matthew (9/28) → |
1. | Akapanda chomboni, akavuka, akafika mjini kwao. |
2. | Na tazama, wakamletea mtu mwenye kupooza, amelala kitandani; naye Yesu, alipoiona imani yao, alimwambia yule mwenye kupooza, Jipe moyo mkuu, mwanangu, umesamehewa dhambi zako. |
3. | Na tazama, baadhi ya waandishi wakasema nafsini mwao, Huyu anakufuru. |
4. | Naye Yesu, hali akijua mawazo yao, akasema, Mbona mnawaza maovu mioyoni mwenu? |
5. | Kwa maana rahisi ni lipi, ni kusema, Umesamehewa dhambi zako, au ni kusema, Ondoka, uende? |
6. | Lakini mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi, (amwambia yule mwenye kupooza) Ondoka, ujitwike kitanda chako, uende nyumbani kwako. |
7. | Akaondoka, akaenda zake nyumbani kwake. |
8. | Makutano walipomwona, walishikwa na hofu, wakamtukuza Mungu, aliyewapa watu amri ya namna hii. |
9. | Naye Yesu alipokuwa akipita kutoka huko aliona mtu ameketi forodhani, aitwaye Mathayo, akamwambia, Nifuate. Akaondoka, akamfuata. |
10. | Ikawa alipoketi nyumbani ale chakula, tazama, watoza ushuru wengi na wenye dhambi walikuja wakaketi pamoja na Yesu na wanafunzi wake. |
11. | Mafarisayo walipoona, waliwaambia wanafunzi wake, Mbona mwalimu wenu anakula pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi? |
12. | Naye aliposikia, aliwaambia, Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio hawawezi. |
13. | Lakini nendeni, mkajifunze maana yake maneno haya, Nataka rehema, wala si sadaka; kwa maana sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi. |
14. | Wakati ule wanafunzi wake Yohana wakamwendea, wakasema, Kwa nini sisi na Mafarisayo twafunga, bali wanafunzi wako hawafungi? |
15. | Yesu akawaambia, Walioalikwa arusini wawezaje kuomboleza, muda bwana arusi akiwapo pamoja nao? Lakini siku zitakuja watakapoondolewa bwana arusi; ndipo watakapofunga. |
16. | Hakuna mtu atiaye kiraka cha nguo mpya katika vazi kuukuu; maana kile kilichotiwa huondoa kipande cha lile vazi, na pale palipotatuka huzidi. |
17. | Wala watu hawatii divai mpya katika viriba vikuukuu; na kama wakitia, vile viriba hupasuka, divai ikamwagika, na viriba vikaharibika; bali hutia divai mpya katika viriba vipya, vikahifadhika vyote. |
18. | Alipokuwa akiwaambia hayo, tazama, akaja jumbe mmoja, akamsujudia, akisema, Binti yangu sasa hivi amekufa; lakini njoo, uweke mkono wako juu yake, naye ataishi. |
19. | Akaondoka Yesu, akamfuata, pamoja na wanafunzi wake. |
20. | Na tazama, mwanamke aliyekuwa na ugonjwa wa kutoka damu muda wa miaka kumi na miwili, alikuja kwa nyuma, akaugusa upindo wa vazi lake. |
21. | Kwa maana alisema moyoni mwake, Nikigusa tu upindo wa vazi lake nitapona. |
22. | Yesu akageuka, akamwona, akamwambia, Jipe moyo mkuu, binti yangu; imani yako imekuponya. Yule mwanamke akapona tangu saa ile. |
23. | Yesu alipofika nyumbani kwa yule jumbe, aliona wapiga filimbi, na makutano wakifanya maombolezo, |
24. | akawaambia, Ondokeni; kwa maana kijana hakufa, amelala tu. Wakamcheka sana. |
25. | Lakini makutano walipoondoshwa, aliingia, akamshika mkono; yule kijana akasimama. |
26. | Zikaenea habari hizi katika nchi ile yote. |
27. | Yesu alipokuwa akipita kutoka huko, vipofu wawili wakamfuata wakipaza sauti, wakisema, Uturehemu, Mwana wa Daudi. |
28. | Naye alipofika nyumbani, wale vipofu walimwendea; Yesu akawaambia, Mnaamini kwamba naweza kufanya hili? Wakamwambia, Naam, Bwana. |
29. | Ndipo alipowagusa macho, akasema, Kwa kadiri ya imani yenu mpate. |
30. | Macho yao yakafumbuka. Naye Yesu akawaagiza kwa nguvu, akisema, Angalieni hata mtu mmoja asijue. |
31. | Lakini wakatoka, wakaeneza habari zake katika nchi ile yote. |
32. | Hata hao walipokuwa wakitoka, tazama, walimletea mtu bubu mwenye pepo. |
33. | Na pepo alipotolewa, yule bubu alinena, makutano wakastajabu, wakasema, Haijaonekana hivi katika Israeli wakati wo wote. |
34. | Lakini Mafarisayo wakasema, Kwa nguvu za mkuu wa pepo atoa pepo. |
35. | Naye Yesu alikuwa akizunguka katika miji yote na vijiji, akifundisha katika masinagogi yao, na kuihubiri habari njema ya ufalme, na kuponya magonjwa yote na udhaifu wa kila aina. |
36. | Na alipowaona makutano, aliwahurumia, kwa sababu walikuwa wamechoka na kutawanyika kama kondoo wasio na mchungaji. |
37. | Ndipo alipowaambia wanafunzi wake, Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache. |
38. | Basi mwombeni Bwana wa mavuno, apeleke watenda kazi katika mavuno yake. |
← Matthew (9/28) → |