| ← Matthew (6/28) → |
| 1. | Angalieni msifanye wema wenu machoni pa watu, kusudi mtazamwe na wao; kwa maana mkifanya kama hayo, hampati thawabu kwa Baba yenu aliye mbinguni. |
| 2. | Basi wewe utoapo sadaka, usipige panda mbele yako, kama wanafiki wafanyavyo katika masinagogi na njiani, ili watukuzwe na watu. |
| 3. | Amin, nawaambieni, Wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe utoapo sadaka, hata mkono wako wa kushoto usijue ufanyalo mkono wako wa kuume; |
| 4. | sadaka yako iwe kwa siri; na Baba yako aonaye sirini atakujazi. |
| 5. | Tena msalipo, msiwe kama wanafiki; kwa maana wao wapenda kusali hali wamesimama katika masinagogi na katika pembe za njia, ili waonekane na watu. Amin, nawaambia, Wamekwisha kupata thawabu yao. |
| 6. | Bali wewe usalipo, ingia katika chumba chako cha ndani, na ukiisha kufunga mlango wako, usali mbele za Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi. |
| 7. | Nanyi mkiwa katika kusali, msipayuke-payuke, kama watu wa mataifa; maana wao hudhani ya kuwa watasikiwa kwa sababu ya maneno yao kuwa mengi. |
| 8. | Basi msifanane na hao; maana Baba yenu anajua mnayohitaji kabla ninyi hamjamwomba. |
| 9. | Basi ninyi salini hivi; Baba yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe, Ufalme wako uje, |
| 10. | Mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni. |
| 11. | Utupe leo riziki yetu. |
| 12. | Utusamehe deni zetu, kama sisi nasi tuwasamehevyo wadeni wetu. |
| 13. | Na usitutie majaribuni, lakini utuokoe na yule mwovu. [Kwa kuwa ufalme ni wako, na nguvu, na utukufu, hata milele. Amina.] |
| 14. | Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi. |
| 15. | Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu. |
| 16. | Tena mfungapo, msiwe kama wanafiki wenye uso wa kukunjamana; maana hujiumbua nyuso zao, ili waonekane na watu kuwa wanafunga. Amin, nawaambia, wamekwisha kupata thawabu yao. |
| 17. | Bali wewe ufungapo, jipake mafuta kichwani, unawe uso; |
| 18. | ili usionekane na watu kuwa unafunga, ila na Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi. |
| 19. | Msijiwekee hazina duniani, nondo na kutu viharibupo, na wevi huvunja na kuiba; |
| 20. | bali jiwekeeni hazina mbinguni, kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu, wala wevi hawavunji wala hawaibi; |
| 21. | kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako. |
| 22. | Taa ya mwili ni jicho; basi jicho lako likiwa safi, mwili wako wote utakuwa na nuru. |
| 23. | Lakini jicho lako likiwa bovu, mwili wako wote utakuwa na giza. Basi ile nuru iliyomo ndani yako ikiwa giza; si giza hilo! |
| 24. | Hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana atamchukia huyu, na kumpenda huyu; ama atashikamana na huyu, na kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali. |
| 25. | Kwa sababu hiyo nawaambieni, Msisumbukie maisha yenu, mle nini au mnywe nini; wala miili yenu, mvae nini. Maisha je! Si zaidi ya chakula, na mwili zaidi ya mavazi? |
| 26. | Waangalieni ndege wa angani, ya kwamba hawapandi, wala hawavuni, wala hawakusanyi ghalani; na Baba yenu wa mbinguni huwalisha hao. Ninyi je! Si bora kupita hao? |
| 27. | Ni yupi kwenu ambaye akijisumbua aweza kujiongeza kimo chake hata mkono mmoja? |
| 28. | Na mavazi, ya nini kuyasumbukia? Fikirini maua ya mashamba, jinsi yameavyo; hayafanyi kazi, wala hayasokoti |
| 29. | nami nawaambia, ya kwamba hata Sulemani katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo la hayo. |
| 30. | Basi, ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya kondeni, yaliyopo leo, na kesho hutupwa kalibuni, je! Hatazidi sana kuwavika ninyi, enyi wa imani haba? |
| 31. | Msisumbuke, basi, mkisema, Tule nini? Au Tunywe nini? Au Tuvae nini? |
| 32. | Kwa maana hayo yote Mataifa huyatafuta; kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote. |
| 33. | Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa. |
| 34. | Basi msisumbukie ya kesho; kwa kuwa kesho itajisumbukia yenyewe. Yatosha kwa siku maovu yake. |
| ← Matthew (6/28) → |