| ← Matthew (5/28) → |
| 1. | Naye alipowaona makutano, alipanda mlimani; na alipokwisha kuketi, wanafunzi wake walimjia; |
| 2. | akafumbua kinywa chake, akawafundisha, akisema, |
| 3. | Heri walio maskini wa roho; Maana ufalme wa mbinguni ni wao. |
| 4. | Heri wenye huzuni; Maana hao watafarijika. |
| 5. | Heri wenye upole; Maana hao watairithi nchi. |
| 6. | Heri wenye njaa na kiu ya haki; Maana hao watashibishwa. |
| 7. | Heri wenye rehema; Maana hao watapata rehema. |
| 8. | Heri wenye moyo safi; Maana hao watamwona Mungu. |
| 9. | Heri wapatanishi; Maana hao wataitwa wana wa Mungu. |
| 10. | Heri wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki; Maana ufalme wa mbinguni ni wao. |
| 11. | Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu. |
| 12. | Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu. |
| 13. | Ninyi ni chumvi ya dunia; lakini chumvi ikiwa imeharibika itatiwa nini hata ikolee? Haifai tena kabisa, ila kutupwa nje na kukanyagwa na watu. |
| 14. | Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu ya mlima. |
| 15. | Wala watu hawawashi taa na kuiweka chini ya pishi, bali juu ya kiango; nayo yawaangaza wote waliomo nyumbani. |
| 16. | Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni. |
| 17. | Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza. |
| 18. | Kwa maana, amin, |
| 19. | Basi mtu ye yote atakayevunja amri moja katika hizi zilizo ndogo, na kuwafundisha watu hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni; bali mtu atakayezitenda na kuzifundisha, huyo ataitwa mkubwa katika ufalme wa mbinguni. |
| 20. | Maana nawaambia ya kwamba, Haki yenu isipozidi hiyo haki ya waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni. |
| 21. | Mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, Usiue, na mtu akiua, itampasa hukumu. |
| 22. | Bali mimi nawaambieni, Kila amwoneaye ndugu yake hasira itampasa hukumu; na mtu akimfyolea ndugu yake, itampasa baraza; na mtu akimwapiza, itampasa jehanum ya moto. |
| 23. | Basi ukileta sadaka yako madhabahuni, na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako, |
| 24. | iache sadaka yako mbele ya madhabahu, uende zako, upatane kwanza na ndugu yako, kisha urudi uitoe sadaka yako. |
| 25. | Patana na mshitaki wako upesi, wakati uwapo pamoja naye njiani; yule mshitaki asije akakupeleka kwa kadhi, na kadhi akakupeleka kwa askari, ukatupwa gerezani. |
| 26. | Amin, nakuambia, Hutoki humo kamwe hata uishe kulipa senti ya mwisho. |
| 27. | Mmesikia kwamba imenenwa, Usizini; |
| 28. | lakini mimi nawaambia, Kila mtu atazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake. |
| 29. | Jicho lako la kuume likikukosesha, ling'oe ulitupe mbali nawe; kwa maana yakufaa kiungo chako kimoja kipotee wala mwili wako mzima usitupwe katika jehanum. |
| 30. | Na mkono wako wa kuume ukikukosesha, ukate uutupe mbali nawe; kwa maana yakufaa kiungo chako kimoja kipotee wala mwili wako mzima usitupwe katika jehanum. |
| 31. | Imenenwa pia, Mtu akimwacha mkewe, na ampe hati ya talaka; |
| 32. | lakini mimi nawaambia, Kila mtu amwachaye mkewe, isipokuwa kwa habari ya uasherati, amfanya kuwa mzinzi; na mtu akimwoa yule aliyeachwa, azini. |
| 33. | Tena mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, Usiape uongo, ila mtimizie Bwana nyapo zako; |
| 34. | lakini mimi nawaambia, Usiape kabisa; hata kwa mbingu, kwa maana ndicho kiti cha enzi cha Mungu; |
| 35. | wala kwa nchi, kwa maana ndiyo pa kuwekea miguu yake; wala kwa Yerusalemu, kwa maana ndio mji wa Mfalme mkuu. |
| 36. | Wala usiape kwa kichwa chako, maana huwezi kufanya unywele mmoja kuwa mweupe au mweusi. |
| 37. | Bali maneno yenu yawe Ndiyo, ndiyo; Siyo, siyo; kwa kuwa yazidiyo hayo yatoka kwa yule mwovu. |
| 38. | Mmesikia kwamba imenenwa, Jicho kwa jicho, na jino kwa jino; |
| 39. | Lakini mimi nawaambia, Msishindane na mtu mwovu; lakini mtu akupigaye shavu la kuume, mgeuzie na la pili. |
| 40. | Na mtu atakaye kukushitaki na kuitwaa kanzu yako, mwachie na joho pia. |
| 41. | Na mtu atakayekulazimisha mwendo wa maili moja, nenda naye mbili. |
| 42. | Akuombaye, mpe; naye atakaye kukopa kwako, usimpe kisogo. |
| 43. | Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako; |
| 44. | lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi, |
| 45. | ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki. |
| 46. | Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru, je! Nao hawafanyi yayo hayo? |
| 47. | Tena mkiwaamkia ndugu zenu tu, mnatenda tendo gani la ziada? Hata watu wa mataifa, je! Nao hawafanyi kama hayo? |
| 48. | Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu. |
| ← Matthew (5/28) → |