| ← Matthew (26/28) → |
| 1. | Ikawa Yesu alipomaliza maneno hayo yote, aliwaambia wanafunzi wake, |
| 2. | Mnajua ya kuwa baada ya siku mbili itakuwa Pasaka, na Mwana wa Adamu atasalitiwa asulibiwe. |
| 3. | Wakati ule wakuu wa makuhani, na wazee wa watu, wakakusanyika katika behewa ya Kuhani Mkuu, jina lake Kayafa; |
| 4. | wakafanya shauri pamoja, ili wamkamate Yesu kwa hila na kumwua. |
| 5. | Lakini wakasema, Isiwe wakati wa sikukuu, isije ikatokea ghasia katika watu. |
| 6. | Naye Yesu alipokuwapo Bethania katika nyumba ya Simoni mkoma, |
| 7. | mwanamke mwenye kibweta cha marhamu ya thamani kubwa alimkaribia akaimimina kichwani pake alipoketi chakulani. |
| 8. | Wanafunzi wake walipoona, wakachukiwa, wakasema, Ni wa nini upotevu huu? |
| 9. | Maana marhamu hii ingaliweza kuuzwa kwa fedha nyingi wakapewa maskini. |
| 10. | Yesu akatambua akawaambia, Mbona mnamtaabisha mwanamke? Maana ni kazi njema aliyonitendea mimi. |
| 11. | Kwa maana siku zote mnao maskini pamoja nanyi; lakini mimi hamnami siku zote. |
| 12. | Maana kwa kunimwagia mwili wangu marhamu hiyo, ametenda hivyo ili kuniweka tayari kwa maziko yangu. |
| 13. | Amin, nawaambieni, Kila patakapohubiriwa Injili hii katika ulimwengu wote, tendo hilo alilolitenda huyu litatajwa pia kwa kumbukumbu lake. |
| 14. | Wakati huo mmoja wa wale Thenashara, jina lake Yuda Iskariote, aliwaendea wakuu wa makuhani, |
| 15. | akasema, Ni nini mtakachonipa, nami nitamsaliti kwenu? Wakampimia vipande thelathini vya fedha. |
| 16. | Tokea wakati huo akawa akitafuta nafasi apate kumsaliti. |
| 17. | Hata siku ya kwanza ya mikate isiyotiwa chachu, wanafunzi wake wakamwendea Yesu, wakamwambia, Ni wapi utakapo tukuandalie uile Pasaka? |
| 18. | Akasema, Enendeni mjini kwa mtu fulani, mkamwambie, Mwalimu asema, Majira yangu ni karibu; kwako nitafanya Pasaka pamoja na wanafunzi wangu. |
| 19. | Wanafunzi wakafanya kama Yesu alivyowaagiza, wakaiandaa Pasaka. |
| 20. | Basi kulipokuwa jioni aliketi chakulani pamoja na wale Thenashara. |
| 21. | Nao walipokuwa wakila, alisema, Amin, nawaambia, Mmoja wenu atanisaliti. |
| 22. | Wakahuzunika sana, wakaanza kumwuliza mmoja mmoja, Ni mimi, Bwana? |
| 23. | Akajibu akasema, Yeye aliyetia mkono wake pamoja nami katika kombe, ndiye atakayenisaliti. |
| 24. | Mwana wa Adamu aenda zake, kama alivyoandikiwa; lakini ole wake mtu yule ambaye amsaliti Mwana wa Adamu! Ingekuwa heri kwake mtu yule kama asingalizaliwa. |
| 25. | Yuda, yule mwenye kumsaliti, akajibu, akasema, Ni mimi, Rabi? Akamwambia, Wewe umesema. |
| 26. | Nao walipokuwa wakila Yesu alitwaa mkate, akabariki, akaumega, akawapa wanafunzi wake, akasema, Twaeni, mle; huu ndio mwili wangu |
| 27. | Akakitwaa kikombe, akashukuru, akawapa, akisema, Nyweni nyote katika hiki; |
| 28. | kwa maana hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi. |
| 29. | Lakini nawaambieni, Sitakunywa kabisa tangu sasa uzao huu wa mzabibu, hata siku ile nitakapokunywa mpya pamoja nanyi katika ufalme wa Baba yangu. |
| 30. | Nao walipokwisha kuimba, wakatoka nje kwenda mlima wa Mizeituni. |
| 31. | Ndipo Yesu akawaambia, Ninyi nyote mtachukizwa kwa ajili yangu usiku huu kwa kuwa imeandikwa, Nitampiga mchungaji, na kondoo wa kundi watatawanyika. |
| 32. | Lakini baada ya kufufuka kwangu, nitawatangulia kwenda Galilaya. |
| 33. | Petro akajibu, akamwambia, Wajapochukizwa wote kwa ajili yako, mimi sitachukizwa kamwe. |
| 34. | Yesu akamwambia, Amin, nakuambia wewe, usiku huu kabla ya kuwika jogoo, utanikana mara tatu. |
| 35. | Petro akamwambia, Ijaponipasa kufa nawe, sitakukana kamwe. Na wanafunzi wote wakasema vivyo hivyo. |
| 36. | Kisha Yesu akaenda pamoja nao mpaka bustani iitwayo Gethsemane, akawaambia wanafunzi wake, Ketini hapa, hata niende kule nikaombe. |
| 37. | Akamchukua Petro na wale wana wawili wa Zebedayo, akaanza kuhuzunika na kusononeka. |
| 38. | Ndipo akawaambia, Roho yangu ina huzuni nyingi kiasi cha kufa; kaeni hapa, mkeshe pamoja nami. |
| 39. | Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifulifuli, akaomba, akisema, Baba yangu, ikiwezekana, kikombe hiki kiniepuke; walakini si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe. |
| 40. | Akawajia wale wanafunzi, akawakuta wamelala, akamwambia Petro, Je! Hamkuweza kukesha pamoja nami hata saa moja? |
| 41. | Kesheni, mwombe, msije mkaingia majaribuni; roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu. |
| 42. | Akaenda tena mara ya pili, akaomba, akisema, Baba yangu, ikiwa haiwezekani kikombe hiki kiniepuke nisipokunywa, mapenzi yako yatimizwe. |
| 43. | Akaja tena, akawakuta wamelala; maana macho yao yamekuwa mazito. |
| 44. | Akawaacha tena, akaenda, akaomba mara ya tatu, akisema maneno yale yale. |
| 45. | Kisha akawajia wanafunzi wake, akawaambia, Laleni sasa, mpumzike tazama, saa imekaribia, na Mwana wa Adamu anatiwa katika mikono ya wenye dhambi. |
| 46. | Ondokeni, twende zetuni! Tazama, yule anayenisaliti amekaribia. |
| 47. | Basi alipokuwa katika kusema, tazama, Yuda, mmoja wa wale Thenashara akaja, na pamoja naye kundi kubwa wenye panga na marungu, wametoka kwa wakuu wa makuhani na wazee wa watu. |
| 48. | Na yule mwenye kumsaliti alikuwa amewapa ishara, akisema, Nitakayembusu, huyo ndiye; mkamateni. |
| 49. | Mara akamwendea Yesu, akasema, Salamu, Rabi, akambusu. |
| 50. | Yesu akamwambia, Rafiki, fanya ulilolijia. Wakaenda, wakanyosha mikono yao wakamkamata Yesu. |
| 51. | Na tazama, mmoja wao waliokuwa pamoja na Yesu akanyosha mkono wake, akaufuta upanga wake, akampiga mtumwa wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio. |
| 52. | Ndipo Yesu akamwambia, Rudisha upanga wako mahali pake, maana wote waushikao upanga, wataangamia kwa upanga. |
| 53. | Ama wadhani ya kuwa mimi siwezi kumsihi Baba yangu, naye ataniletea sasa hivi zaidi ya majeshi kumi na mawili ya malaika? |
| 54. | Yatatimizwaje basi maandiko, ya kwamba hivyo ndivyo vilivyopasa kujiri? |
| 55. | Saa ile Yesu akawaambia makutano, Je, mmetoka kama kumkamata mnyang'anyi, wenye panga na marungu, ili kunishika? Kila siku naliketi hekaluni nikifundisha, msinikamate. |
| 56. | Lakini haya yote yamekuwa, ili maandiko ya manabii yatimizwe. Ndipo wanafunzi wote wakamwacha, wakakimbia. |
| 57. | Nao waliomkamata Yesu wakampeleka kwa Kayafa, Kuhani Mkuu, walikokuwa wamekutanika waandishi na wazee. |
| 58. | Na Petro akamfuata kwa mbali mpaka behewa ya Kuhani Mkuu, akaingia ndani, akaketi pamoja na watumishi, auone mwisho. |
| 59. | Basi wakuu wa makuhani na baraza yote wakatafuta ushuhuda wa uongo juu ya Yesu, wapate kumwua; |
| 60. | wasiuone wangawa walitokea mashahidi wa uongo wengi. |
| 61. | Hata baadaye wawili wakatokea, wakasema, Huyu alisema, Naweza kulivunja hekalu la Mungu, na kulijenga kwa siku tatu. |
| 62. | Kisha Kuhani Mkuu akasimama akamwambia, Hujibu neno? Hawa wanakushuhudia nini? |
| 63. | Lakini, Yesu akanyamaza. Kuhani Mkuu akamwambia, Nakuapisha kwa Mungu aliye hai, utuambie kama wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu. |
| 64. | Yesu akamwambia, Wewe umesema; lakini nawaambieni, Tangu sasa mtamwona Mwana wa Adamu ameketi mkono wa kuume wa nguvu, akija juu ya mawingu ya mbinguni. |
| 65. | Ndipo Kuhani Mkuu akararua mavazi yake, akisema, Amekufuru; mna haja gani tena ya mashahidi? Tazameni, sasa mmesikia hiyo kufuru yake; |
| 66. | mwaonaje ninyi? Wakajibu, wakasema, Imempasa kuuawa. |
| 67. | Ndipo wakamtemea mate ya uso, wakampiga makonde; wengine wakampiga makofi, |
| 68. | wakisema, Ewe Kristo, tufumbulie; ni nani aliyekupiga? |
| 69. | Na Petro alikuwa ameketi nje behewani; kijakazi mmoja akamwendea, akasema, Wewe nawe ulikuwapo pamoja na Yesu wa Galilaya. |
| 70. | Akakana mbele ya wote, akisema, Sijui usemalo. |
| 71. | Naye alipotoka nje hata ukumbini, mwanamke mwingine alimwona, akawaambia watu waliokuwako huko, Huyu alikuwapo pamoja na Yesu Mnazareti. |
| 72. | Akakana tena kwa kiapo, Simjui mtu huyu. |
| 73. | Punde kidogo, wale waliohudhuria wakamwendea, wakamwambia Petro, Hakika wewe nawe u mmoja wao; kwa sababu hata usemi wako wakutambulisha. |
| 74. | Ndipo akaanza kulaani na kuapa akisema, Simjui mtu huyu. Na mara akawika jogoo. |
| 75. | Petro akalikumbuka lile neno la Yesu alilolisema, Kabla ya kuwika jogoo, utanikana mara tatu. Akatoka nje, akalia kwa majonzi. |
| ← Matthew (26/28) → |