← Matthew (24/28) → |
1. | Yesu akaenda zake, akatoka hekaluni; wanafunzi wake wakamwendea ili kumwonyesha majengo ya hekalu. |
2. | Naye akajibu akawaambia, Hamyaoni haya yote? Amin, nawaambieni, Halitasalia hapa jiwe juu ya jiwe ambalo halitabomoshwa. |
3. | Hata alipokuwa ameketi katika mlima wa Mizeituni, wanafunzi wake wakamwendea kwa faragha, wakisema, Tuambie, mambo hayo yatakuwa lini? Nayo ni nini dalili ya kuja kwako, na ya mwisho wa dunia? |
4. | Yesu akajibu, akawaambia, Angalieni, mtu asiwadanganye. |
5. | Kwa sababu wengi watakuja kwa jina langu, wakisema, Mimi ni Kristo; nao watadanganya wengi. |
6. | Nanyi mtasikia habari za vita na matetesi ya vita; angalieni, msitishwe; maana hayo hayana budi kutukia; lakini ule mwisho bado. |
7. | Kwa maana taifa litaondoka kupigana na taifa, na ufalme kupigana na ufalme; kutakuwa na njaa, na matetemeko ya nchi mahali mahali. |
8. | Hayo yote ndiyo mwanzo wa utungu. |
9. | Wakati huo watawasaliti ninyi mpate dhiki, nao watawaua; nanyi mtakuwa watu wa kuchukiwa na mataifa yote kwa ajili ya jina langu. |
10. | Ndipo wengi watakapojikwaa, nao watasalitiana, na kuchukiana. |
11. | Na manabii wengi wa uongo watatokea, na kudanganya wengi. |
12. | Na kwa sababu ya kuongezeka maasi, upendo wa wengi utapoa. |
13. | Lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka. |
14. | Tena habari njema ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu wote, kuwa ushuhuda kwa mataifa yote; hapo ndipo ule mwisho utakapokuja. |
15. | Basi hapo mtakapoliona chukizo la uharibifu, lile lililonenwa na nabii Danieli, limesimama katika patakatifu (asomaye na afahamu), |
16. | ndipo walio katika Uyahudi na wakimbilie milimani; |
17. | naye aliye juu ya dari asishuke kuvichukua vitu vilivyomo nyumbani mwake; |
18. | wala aliye shambani asirudi nyuma kuichukua nguo yake. |
19. | Ole wao wenye mimba na wanyonyeshao siku hizo! |
20. | Ombeni, ili kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi, wala siku ya sabato. |
21. | Kwa kuwa wakati huo kutakuwapo dhiki kubwa, ambayo haijatokea namna yake tangu mwanzo wa ulimwengu hata sasa, wala haitakuwapo kamwe. |
22. | Na kama siku hizo zisingalifupizwa, asingeokoka mtu ye yote; lakini kwa ajili ya wateule zitafupizwa siku hizo. |
23. | Wakati huo mtu akiwaambia, Tazama, Kristo yupo hapa, au yuko kule msisadiki. |
24. | Kwa maana watatokea makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, kama yamkini, hata walio wateule. |
25. | Tazama, nimekwisha kuwaonya mbele. |
26. | Basi wakiwaambia, Yuko jangwani, msitoke; yumo nyumbani, msisadiki. |
27. | Kwa maana kama vile umeme utokavyo mashariki ukaonekana hata magharibi, hivyo ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. |
28. | Kwa kuwa po pote ulipo mzoga, ndipo watakapokusanyika tai. |
29. | Lakini mara, baada ya dhiki ya siku zile, jua litatiwa giza, na mwezi hautatoa mwanga wake, na nyota zitaanguka mbinguni, na nguvu za mbinguni zitatikisika; |
30. | ndipo itakapoonekana ishara yake Mwana wa Adamu mbinguni; ndipo mataifa yote ya ulimwengu watakapoomboleza, nao watamwona Mwana wa Adamu akija juu ya mawingu ya mbinguni pamoja na nguvu na utukufu mwingi. |
31. | Naye atawatuma malaika zake pamoja na sauti kuu ya parapanda, nao watawakusanya wateule wake toka pepo nne, toka mwisho huu wa mbingu mpaka mwisho huu. |
32. | Basi kwa mtini jifunzeni mfano; tawi lake likiisha kuchipuka na kuchanua majani, mwatambua ya kuwa wakati wa mavuno u karibu; |
33. | nanyi kadhalika, myaonapo hayo yote, tambueni ya kuwa yu karibu, milangoni. |
34. | Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita, hata hayo yote yatakapotimia. |
35. | Mbingu na nchi zitapita; lakini maneno yangu hayatapita kamwe. |
36. | Walakini habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana, ila Baba peke yake. |
37. | Kwa maana kama vile ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. |
38. | Kwa kuwa kama vile siku zile zilizokuwa kabla ya Gharika watu walivyokuwa wakila, na kunywa, wakioa na kuolewa, hata siku ile aliyoingia Nuhu katika safina, |
39. | wasitambue, hata Gharika ikaja, ikawachukua wote, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. |
40. | Wakati ule watu wawili watakuwako kondeni; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa; |
41. | wanawake wawili watakuwa wakisaga; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa. |
42. | Kesheni basi; kwa maana hamjui ni siku ipi atakayokuja Bwana wenu. |
43. | Lakini fahamuni neno hili; kama mwenye nyumba angaliijua ile zamu mwivi atakayokuja, angalikesha, wala asingaliiacha nyumba yake kuvunjwa. |
44. | Kwa sababu hiyo ninyi nanyi jiwekeni tayari; kwa kuwa katika saa msiyodhani Mwana wa Adamu yuaja. |
45. | Ni nani basi yule mtumwa mwaminifu mwenye akili, ambaye bwana wake alimweka juu ya nyumba yake, awape watu chakula kwa wakati wake? |
46. | Heri mtumwa yule, ambaye bwana wake ajapo atamkuta akifanya hivyo. |
47. | Amin, nawaambieni, atamweka juu ya vitu vyake vyote. |
48. | Lakini mtumwa yule mbaya akisema moyoni mwake, Bwana wangu anakawia; |
49. | akaanza kuwapiga wajoli wake, na kula na kunywa pamoja na walevi; |
50. | bwana wake mtumwa huyo atakuja siku asiyodhani, na saa asiyojua, |
51. | atamkata vipande viwili, na kumwekea fungu lake pamoja na wanafiki; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. |
← Matthew (24/28) → |