Matthew (23/28)  

1. Kisha Yesu akawaambia makutano na wanafunzi wake, akasema,
2. Waandishi na Mafarisayo wameketi katika kiti cha Musa;
3. basi, yo yote watakayowaambia, myashike na kuyatenda; lakini kwa mfano wa matendo yao, msitende; maana wao hunena lakini hawatendi.
4. Wao hufunga mizigo mizito na kuwatwika watu mabegani mwao; wasitake wenyewe kuigusa kwa kidole chao.
5. Tena matendo yao yote huyatenda ili kutazamwa na watu; kwa kuwa hupanua hirizi zao, huongeza matamvua yao;
6. hupenda viti vya mbele katika karamu, na kuketi mbele katika masinagogi,
7. na kusalimiwa masokoni, na kuitwa na watu, Rabi.
8. Bali ninyi msiitwe Rabi, maana mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu.
9. Wala msimwite mtu baba duniani; maana Baba yenu ni mmoja, aliye wa mbinguni.
10. Wala msiitwe viongozi; maana kiongozi wenu ni mmoja, naye ndiye Kristo.
11. Naye aliye mkubwa wenu atakuwa mtumishi wenu.
12. Na ye yote atakayejikweza, atadhiliwa; na ye yote atakayejidhili, atakwezwa.
13. Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnawafungia watu ufalme wa mbinguni; ninyi wenyewe hamwingii, wala wanaoingia hamwaachi waingie.
14. [Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnakula nyumba za wajane, na kwa unafiki mnasali sala ndefu; kwa hiyo mtapata hukumu iliyo kubwa zaidi.]
15. Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnazunguka katika bahari na nchi kavu ili kumfanya mtu mmoja kuwa mwongofu; na akiisha kufanyika, mnamfanya kuwa mwana wa jehanum mara mbili zaidi kuliko ninyi wenyewe.
16. Ole wenu viongozi vipofu, ninyi msemao, Mtu atakayeapa kwa hekalu, si kitu; bali mtu atakayeapa kwa dhahabu ya hekalu, amejifunga.
17. Wapumbavu ninyi na vipofu; maana ni ipi iliyo kubwa, ile dhahabu, au lile hekalu liitakasalo dhahabu?
18. Tena, Mtu atakayeapa kwa madhabahu, si kitu; bali mtu atakayeapa kwa sadaka iliyo juu yake, amejifunga.
19. Vipofu ninyi; maana ni ipi iliyo kubwa, ile sadaka, au ile madhabahu iitakasayo sadaka?
20. Basi yeye aapaye kwa madhabahu, huapa kwa hiyo, na kwa vitu vyote vilivyo juu yake.
21. Naye aapaye kwa hekalu, huapa kwa hilo, na kwa yeye akaaye ndani yake.
22. Naye aapaye kwa mbingu, huapa kwa kiti cha enzi cha Mungu, na kwa yeye aketiye juu yake.
23. Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnalipa zaka za mnanaa na bizari na jira, lakini mmeacha mambo makuu ya sheria, yaani, adili, na rehema, na imani; hayo imewapasa kuyafanya, wala yale mengine msiyaache.
24. Viongozi vipofu, wenye kuchuja mbu na kumeza ngamia.
25. Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnasafisha nje ya kikombe na chano, na ndani yake vimejaa unyang'anyi na kutokuwa na kiasi.
26. Ewe Farisayo kipofu, safisha kwanza ndani ya kikombe, ili nje yake nayo ipate kuwa safi.
27. Ole wenu, waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mmefanana na makaburi yaliyopakwa chokaa, nayo kwa nje yaonekana kuwa mazuri, bali ndani yamejaa mifupa ya wafu, na uchafu wote.
28. Vivyo hivyo ninyi nanyi, kwa nje mwaonekana na watu kuwa wenye haki, bali ndani mmejaa unafiki na maasi.
29. Ole wenu, waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnayajenga makaburi ya manabii, na kuyapamba maziara ya wenye haki,
30. na kusema, Kama sisi tungalikuwako zamani za baba zetu, hatungalishirikiana nao katika damu ya manabii.
31. Hivi mwajishuhudia wenyewe, ya kwamba ninyi ni wana wao waliowaua manabii.
32. Kijazeni basi kipimo cha baba zenu.
33. Enyi nyoka, wana wa majoka, mtaikimbiaje hukumu ya jehanum?
34. Kwa sababu hiyo, angalieni, mimi natuma kwenu manabii na wenye hekima na waandishi; na wengine wao ninyi mtawaua na kuwasulibisha, na wengine wao mtawapiga katika masinagogi yenu, na kuwafukuza mji kwa mji;
35. hivyo ije juu yenu damu yote ya haki iliyomwagika juu ya nchi, tangu damu ya Habili, yule mwenye haki, hata damu ya Zakaria bin Barakia, mliyemwua kati ya patakatifu na madhabahu.
36. Amin, nawaambieni, Mambo hayo yote yatakuja juu ya kizazi hiki.
37. Ee Yerusalemu, Yerusalemu, uwauaye manabii, na kuwapiga kwa mawe wale waliotumwa kwako! Ni mara ngapi nimetaka kuwakusanya pamoja watoto wako, kama vile kuku avikusanyavyo pamoja vifaranga vyake chini ya mabawa yake, lakini hamkutaka!
38. Angalieni, nyumba yenu mmeachiwa hali ya ukiwa.
39. Kwa maana nawaambia, Hamtaniona kamwe tangu sasa, hata mtakaposema, Amebarikiwa ajaye kwa jina la Bwana.

  Matthew (23/28)