| ← Matthew (22/28) → |
| 1. | Yesu akajibu, akawaambia tena kwa mithali, akisema, |
| 2. | Ufalme wa mbinguni umefanana na mfalme mmoja aliyemfanyia mwanawe arusi. |
| 3. | Akawatuma watumwa wake wawaite walioalikwa kuja arusini; nao wakakataa kuja. |
| 4. | Akatuma tena watu kwa wengine, akisema, Waambieni wale walioalikwa, Tazameni, nimeandaa karamu yangu; ng'ombe zangu na vinono vimekwisha kuchinjwa, na vyote vimekuwa tayari, njoni arusini. |
| 5. | Lakini hawakujali, wakaenda zao, mmoja shambani kwake, mmoja kwenye biashara yake; |
| 6. | nao waliosalia wakawakamata watumwa wake, wakawatenda jeuri, na kuwaua. |
| 7. | Basi yule mfalme akaghadhibika; akapeleka majeshi yake, akawaangamiza wauaji wale, akauteketeza mji wao. |
| 8. | Kisha akawaambia watumwa wake, Arusi i tayari, lakini wale walioalikwa hawakustahili. |
| 9. | Basi enendeni hata njia panda za barabara, na wote mwaonao waiteni arusini. |
| 10. | Watumwa wale wakatoka wakaenda njia kuu, wakakusanya wote waliowaona, waovu kwa wema; arusi ikajaa wageni. |
| 11. | Lakini alipoingia yule mfalme ili kuwatazama wageni wake, akaona mle mtu mmoja asiyevaa vazi la arusi. |
| 12. | Akamwambia, Rafiki, uliingiaje humu nawe huna vazi la arusi? Naye akatekewa. |
| 13. | Mfalme akawaambia watumishi, Mfungeni mikono na miguu, mchukueni mkamtupe katika giza la nje; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. |
| 14. | Kwa maana waitwao ni wengi, bali wateule ni wachache. |
| 15. | Ndipo Mafarisayo wakaenda zao, wakafanya shauri, jinsi ya kumtega kwa maneno. |
| 16. | Wakatuma kwake wanafunzi wao pamoja na Maherodi, wakasema, Mwalimu, twajua ya kuwa wewe u mtu wa kweli, na njia ya Mungu waifundisha katika kweli, wala hujali cheo cha mtu awaye yote, kwa maana hutazami sura za watu. |
| 17. | Basi utuambie, Waonaje? Ni halali kumpa Kaisari kodi, ama sivyo? |
| 18. | Lakini Yesu akaufahamu uovu wao, akasema, Mbona mnanijaribu, enyi wanafiki? |
| 19. | Nionyesheni fedha ya kodi. Nao wakamletea dinari. |
| 20. | Akawaambia, Ni ya nani sanamu hii, na anwani hii? |
| 21. | Wakamwambia, Ni ya Kaisari. Akawaambia, Basi, mlipeni Kaisari yaliyo ya Kaisari, na Mungu yaliyo ya Mungu. |
| 22. | Waliposikia, walistaajabu, wakamwacha, wakaenda zao. |
| 23. | Siku ile Masadukayo, watu wasemao ya kwamba hakuna kiyama, wakamwendea, wakamwuliza, |
| 24. | wakisema, Mwalimu, Musa alisema, Mtu akifa, akiwa hana watoto, ndugu yake na amwoe yule mkewe, ili ampatie nduguye mzao. |
| 25. | Basi, kwetu kulikuwa na ndugu saba; wa kwanza akaoa, akafariki, na kwa kuwa hana mzao, akamwachia nduguye mke wake. |
| 26. | Vivyo hivyo wa pili naye, na wa tatu, hata wote saba. |
| 27. | Mwisho wa wote yule mwanamke akafa naye. |
| 28. | Basi, katika kiyama, atakuwa mke wa yupi katika wale saba? Maana wote walikuwa naye. |
| 29. | Yesu akajibu, akawaambia, Mwapotea, kwa kuwa hamyajui maandiko wala uweza wa Mungu. |
| 30. | Kwa maana katika kiyama hawaoi wala hawaolewi, bali huwa kama malaika mbinguni. |
| 31. | Tena kwa habari ya kiyama ya watu, hamjalisoma neno lililonenwa na Mungu, akisema, |
| 32. | Mimi ni Mungu wa Ibrahimu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo? Mungu si Mungu wa wafu, bali wa walio hai. |
| 33. | Na makutano waliposikia, walishangaa kwa mafunzo yake. |
| 34. | Na Mafarisayo waliposikia ya kwamba amewafumba kinywa wale Masadukayo, walifanya shauri pamoja. |
| 35. | Mmoja wao, mwana-sheria, akamwuliza, akimjaribu; |
| 36. | Mwalimu, katika torati ni amri ipi iliyo kuu? |
| 37. | Akamwambia, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote. |
| 38. | Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza. |
| 39. | Na ya pili yafanana nayo, nayo ni hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. |
| 40. | Katika amri hizi mbili hutegemea torati yote na manabii. |
| 41. | Na Mafarisayo walipokusanyika, Yesu aliwauliza, akisema, Mwaonaje katika habari za Kristo? |
| 42. | Ni mwana wa nani? Wakamwambia, Ni wa Daudi. |
| 43. | Akawauliza, Imekuwaje basi Daudi katika Roho kumwita Bwana, akisema, |
| 44. | Bwana alimwambia Bwana wangu, Uketi mkono wangu wa kuume, Hata niwawekapo adui zako Kuwa chini ya miguu yako? |
| 45. | Basi, Daudi akimwita Bwana, amekuwaje ni mwanawe? |
| 46. | Wala hakuweza mtu kumjibu neno; wala hakuthubutu mtu ye yote tangu siku ile kumwuliza neno tena. |
| ← Matthew (22/28) → |