Matthew (2/28)  

1. Yesu alipozaliwa katika Bethlehemu ya Uyahudi zamani za mfalme Herode, tazama, mamajusi wa mashariki walifika Yerusalemu, wakisema,
2. Yuko wapi yeye aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tuliiona nyota yake mashariki, nasi tumekuja kumsujudia.
3. Basi mfalme Herode aliposikia hayo, alifadhaika, na Yerusalemu pia pamoja naye.
4. Akakusanya wakuu wa makuhani wote na waandishi wa watu, akatafuta habari kwao, Kristo azaliwa wapi?
5. Nao wakamwambia, Katika Bethlehemu ya Uyahudi; kwa maana ndivyo ilivyoandikwa na nabii,
6. Nawe Bethlehemu, katika nchi ya Yuda, Hu mdogo kamwe katika majumbe wa Yuda; Kwa kuwa kwako atatoka mtawala Atakayewachunga watu wangu Israeli.
7. Kisha Herode akawaita wale mamajusi faraghani, akapata kwao hakika ya muda tangu ilipoonekana ile nyota.
8. Akawapeleka Bethlehemu, akasema, Shikeni njia, mkaulize sana mambo ya mtoto; na mkiisha kumwona, nileteeni habari, ili mimi nami niende nimsujudie.
9. Nao waliposikia maneno ya mfalme, walishika njia; na tazama, ile nyota waliyoiona mashariki ikawatangulia, hata ikaenda ikasimama juu ya mahali alipokuwapo mtoto.
10. Nao walipoiona ile nyota, walifurahi furaha kubwa mno.
11. Wakaingia nyumbani, wakamwona mtoto pamoja na Mariamu mamaye, wakaanguka wakamsujudia; nao walipokwisha kufungua hazina zao, wakamtolea tunu; dhahabu na uvumba na manemane.
12. Nao wakiisha kuonywa na Mungu katika ndoto wasimrudie Herode, wakaenda zao kwao kwa njia nyingine.
13. Na hao walipokwisha kwenda zao, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto, akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mama yake, ukimbilie Misri, ukae huko hata nikuambie; kwa maana Herode anataka kumtafuta mtoto amwangamize.
14. Akaondoka akamchukua mtoto na mama yake usiku, akaenda zake Misri;
15. akakaa huko hata alipokufa Herode; ili litimie neno lililonenwa na Bwana kwa ujumbe wa nabii, akisema, Kutoka Misri nalimwita mwanangu.
16. Ndipo Herode, alipoona ya kuwa amedhihakiwa na wale mamajusi, alighadhabika sana, akatuma watu akawaua watoto wote wanaume waliokuwako huko Bethlehemu na viungani mwake mwote, tangu wenye miaka miwili na waliopungua, kwa muda ule aliouhakikisha kwa wale mamajusi.
17. Ndipo lilipotimia neno lililonenwa na nabii Yeremia, akisema,
18. Sauti ilisikiwa Rama, Kilio, na maombolezo mengi, Raheli akiwalilia watoto wake, Asikubali kufarijiwa, kwa kuwa hawako.
19. Hata alipofariki Herode, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto huko Misri,
20. akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mamaye, ushike njia kwenda nchi ya Israeli; kwa maana wamekufa walioitafuta roho ya mtoto.
21. Akaondoka akamchukua mtoto na mamaye, akafika nchi ya Israeli.
22. Lakini aliposikia ya kwamba Arkelao anamiliki huko Uyahudi mahali pa Herode babaye, aliogopa kwenda huko; naye akiisha kuonywa katika ndoto, akasafiri pande za Galilaya,
23. akaenda, akakaa katika mji ulioitwa Nazareti; ili litimie neno lililonenwa na manabii, Ataitwa Mnazorayo.

  Matthew (2/28)