| ← Matthew (15/28) → |
| 1. | Ndipo Mafarisayo na waandishi toka Yerusalemu walipomwendea Yesu wakisema, |
| 2. | Mbona wanafunzi wako huyahalifu mapokeo ya wazee, kwa maana hawanawi mikono walapo chakula. |
| 3. | Akajibu, akawaambia, Mbona ninyi nanyi huihalifu amri ya Mungu kwa ajili ya mapokeo yenu? |
| 4. | Kwa kuwa Mungu alisema, Mheshimu baba yako na mama yako, na Amtukanaye baba yake au mama yake kufa na afe. |
| 5. | Bali ninyi husema, Atakayemwambia babaye au mamaye, Cho chote kikupasacho kusaidiwa na mimi ni wakfu, |
| 6. | basi asimheshimu baba yake au mama yake. Mkalitangua neno la Mungu kwa ajili ya mapokeo yenu. |
| 7. | Enyi wanafiki, ni vema alivyotabiri Isaya kwa habari zenu, akisema, |
| 8. | Watu hawa huniheshimu kwa midomo; Ila mioyo yao iko mbali nami. |
| 9. | Nao waniabudu bure, Wakifundisha mafundisho Yaliyo maagizo ya wanadamu. |
| 10. | Akawaita makutano akawaambia |
| 11. | Sikilizeni, mfahamu; Sicho kiingiacho kinywani kimtiacho mtu unajisi; bali kitokacho kinywani ndicho kimtiacho mtu unajisi. |
| 12. | Ndipo wanafunzi wake walipomwendea, wakamwambia, Wajua ya kuwa Mafarisayo walipolisikia neno lile walichukizwa? |
| 13. | Akajibu, akasema, Kila pando asilolipanda Baba yangu wa mbinguni litang'olewa. |
| 14. | Waacheni; hao ni viongozi vipofu wa vipofu. Na kipofu akimwongoza kipofu mwenzake, watatumbukia shimoni wote wawili. |
| 15. | Basi Petro akajibu, akamwambia, Tueleze mfano huo. |
| 16. | Yesu akasema, Hata sasa ninyi nanyi mngali hamna akili? |
| 17. | Hamjafahamu bado ya kuwa kila kiingiacho kinywani hupita tumboni, kikatupwa chooni? |
| 18. | Bali vitokavyo kinywani vyatoka moyoni; navyo ndivyo vimtiavyo mtu unajisi. |
| 19. | Kwa maana moyoni hutoka mawazo mabaya, uuaji, uzinzi, uasherati; wivi, ushuhuda wa uongo, na matukano; |
| 20. | hayo ndiyo yamtiayo mtu unajisi; lakini kula kabla hajanawa mikono hakumtii mtu unajisi. |
| 21. | Yesu akaondoka huko, akaenda kando pande za Tiro na Sidoni. |
| 22. | Na tazama, mwanamke Mkananayo wa mipaka ile akatokea, akampazia sauti akisema, Unirehemu, Bwana, Mwana wa Daudi; binti yangu amepagawa sana na pepo. |
| 23. | Wala yeye hakumjibu neno. Nao wanafunzi wake wakamwendea, wakamwomba, wakisema, Mwache aende zake; kwa maana anapiga kelele nyuma yetu. |
| 24. | Akajibu, akasema, Sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli. |
| 25. | Naye akaja akamsujudia, akisema Bwana, unisaidie. |
| 26. | Akajibu, akasema, Si vema kukitwaa chakula cha watoto na kuwatupia mbwa. |
| 27. | Akasema, Ndiyo, Bwana, lakini hata mbwa hula makombo yaangukayo mezani pa bwana zao. |
| 28. | Ndipo Yesu akajibu, akamwambia, Mama, imani yako ni kubwa; na iwe kwako kama utakavyo. Akapona binti yake tangu saa ile. |
| 29. | Yesu akaondoka huko, akafika kando ya bahari ya Galilaya; akapanda mlimani, akaketi huko. |
| 30. | Wakamwendea makutano mengi wakimletea viwete, vipofu, mabubu, vilema, na wengine wengi, wakawaweka miguuni pake; akawaponya; |
| 31. | hata ule mkutano wakastaajabu, walipowaona mabubu wanasema, vilema wanakuwa wazima, viwete wanakwenda, na vipofu wanaona; wakamtukuza Mungu wa Israeli. |
| 32. | Yesu akawaita wanafunzi wake, akasema, Nawahurumia mkutano, kwa kuwa yapata siku tatu wamekaa pamoja nami, wala hawana kitu cha kula, tena kuwaaga wakifunga sipendi, wasije wakazimia njiani. |
| 33. | Wanafunzi wake wakamwambia, Tupate wapi mikate mingi hapa nyikani, hata kushibisha mkutano mkuu namna hii? |
| 34. | Yesu akawaambia, Mnayo mikate mingapi? Wakasema, Saba, na visamaki vichache. |
| 35. | Akawaagiza mkutano waketi chini; |
| 36. | akaitwaa ile mikate saba na vile visamaki, akashukuru akavimega, akawapa wanafunzi wake, nao wanafunzi wakawapa makutano. |
| 37. | Wakala wote wakashiba; wakayaokota masazo ya vipande vya mikate makanda saba, yamejaa. |
| 38. | Nao waliokula walikuwa wanaume elfu nne, bila wanawake na watoto. |
| 39. | Akawaaga makutano, akapanda chomboni, akaenda pande za Magadani. |
| ← Matthew (15/28) → |