Matthew (14/28)  

1. Wakati ule mfalme Herode alisikia habari za Yesu, akawaambia watumishi wake,
2. Huyo ndiye Yohana Mbatizaji; amefufuka katika wafu; na kwa hiyo nguvu hizo zinatenda kazi ndani yake.
3. Maana Herode alikuwa amemkamata Yohana, akamfunga, akamtia gerezani, kwa ajili ya Herodia, mke wa Filipo nduguye.
4. Kwa sababu Yohana alimwambia, Si halali kwako kuwa naye.
5. Naye alipotaka kumwua, aliwaogopa watu, maana walimwona Yohana kuwa nabii.
6. Hata ilipofika sikukuu ya kuzaliwa kwake Herode, binti Herodia alicheza mbele ya watu, akampendeza Herode.
7. Hata akaahidi kwa kiapo ya kwamba atampa lo lote atakaloliomba.
8. Naye, huku akichochewa na mamaye, akasema, Nipe hapa katika kombe kichwa cha Yohana Mbatizaji.
9. Naye mfalme akasikitika; lakini kwa ajili ya viapo vyake, na kwa ajili ya wale walioketi chakulani pamoja naye, akaamuru apewe;
10. akatuma mtu, akamkata kichwa Yohana mle gerezani.
11. Kichwa chake kikaletwa katika kombe, akapewa yule kijana; akakichukua kwa mamaye.
12. Wanafunzi wake wakaenda, wakamchukua yule maiti, wakamzika; kisha wakaenda wakampasha Yesu habari.
13. Naye Yesu aliposikia; hayo, aliondoka huko katika chombo, akaenda mahali pasipo watu, faraghani. Na makutano waliposikia, walimfuata kwa miguu kutoka mijini mwao.
14. Yesu akatoka, akaona mkutano mkuu, akawahurumia, akawaponya wagonjwa wao.
15. Hata kulipokuwa jioni, wanafunzi wake walimwendea, wakasema, Mahali hapa ni nyika tupu, na saa imekwisha pita; uwaage makutano, waende zao vijijini, wakajinunulie vyakula.
16. Yesu akawaambia, Hawana haja kwenda zao, wapeni ninyi vyakula.
17. Wakamwambia, Hamna kitu hapa ila mikate mitano na samaki wawili.
18. Akasema, Nileteeni hapa.
19. Akawaagiza makutano waketi katika majani; akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama juu mbinguni, akabariki, akaimega ile mikate, akawapa wanafunzi, wanafunzi wakawapa makutano.
20. Wakala wote wakashiba; wakayaokota masazo ya vipande vya mikate, vikapu kumi na viwili, vimejaa.
21. Nao waliokula walikuwa wanaume wapata elfu tano, bila wanawake na watoto.
22. Mara akawalazimisha wanafunzi wake wapande chomboni na kutangulia mbele yake kwenda ng'ambo, wakati yeye alipokuwa akiwaaga mkutano.
23. Naye alipokwisha kuwaaga makutano, alipanda mlimani faraghani, kwenda kuomba. Na kulipokuwa jioni, alikuwako huko peke yake.
24. Na kile chombo kimekwisha kufika katikati ya bahari, kinataabika sana na mawimbi; maana upepo ulikuwa wa mbisho.
25. Hata wakati wa zamu ya nne ya usiku Yesu akawaendea, akienda kwa miguu juu ya bahari.
26. Wanafunzi walipomwona akienda juu ya bahari, wakafadhaika, wakisema, Ni kivuli; wakapiga yowe kwa hofu.
27. Mara Yesu alinena, akawaambia, Jipeni moyo ni mimi; msiogope.
28. Petro akamjibu, akasema, Bwana, ikiwa ni wewe, niamuru nije kwako juu ya maji.
29. Akasema, Njoo. Petro akashuka chomboni, akaenda kwa miguu juu ya maji, ili kumwendea Yesu.
30. Lakini alipouona upepo, akaogopa; akaanza kuzama, akapiga yowe, akisema, Bwana, niokoe.
31. Mara Yesu akanyosha mkono wake, akamshika, akamwambia, Ewe mwenye imani haba, mbona uliona shaka?
32. Nao walipopanda chomboni, upepo ulikoma.
33. Nao waliokuwamo ndani ya chombo wakamsujudia, wakisema, Hakika wewe u Mwana wa Mungu.
34. Na walipokwisha kuvuka, walifika nchi ya Genesareti.
35. Na watu wa mahali pale walipomtambua, walituma watu kwenda nchi zile zilizo kandokando, wakamletea wote waliokuwa hawawezi;
36. nao wakamsihi waguse hata pindo la vazi lake tu; na wote waliogusa wakaponywa kabisa.

  Matthew (14/28)