| ← Matthew (13/28) → |
| 1. | Siku ile Yesu akatoka nyumbani, akaketi kando ya bahari. |
| 2. | Wakamkusanyikia makutano mengi, hata akapanda chomboni, akaketi; na ule mkutano wote wakasimama pwani. |
| 3. | Akawaambia mambo mengi kwa mifano, akisema, Tazama, mpanzi alitoka kwenda kupanda. |
| 4. | Hata alipokuwa akipanda, mbegu nyingine zilianguka karibu na njia, ndege wakaja wakazila; |
| 5. | nyingine zikaanguka penye miamba, pasipokuwa na udongo mwingi; mara zikaota, kwa udongo kukosa kina; |
| 6. | na jua lilipozuka ziliungua; na kwa kuwa hazina mizizi zikanyauka. |
| 7. | Nyingine zikaanguka penye miiba; ile miiba ikamea, ikazisonga; |
| 8. | nyingine zikaanguka penye udongo mzuri, zikazaa, moja mia, moja sitini, moja thelathini. |
| 9. | Mwenye masikio na asikie. |
| 10. | Wakaja wanafunzi, wakamwambia, Kwa nini wasema nao kwa mifano? |
| 11. | Akajibu, akawaambia, Ninyi mmejaliwa kuzijua siri za ufalme wa mbinguni, bali wao hawakujaliwa. |
| 12. | Kwa maana ye yote mwenye kitu atapewa, naye atazidishiwa tele; lakini ye yote asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang'anywa. |
| 13. | Kwa sababu hii nasema nao kwa mifano; kwa kuwa wakitazama hawaoni, na wakisikia hawasikii, wala kuelewa. |
| 14. | Na neno la nabii Isaya linatimia kwao, likisema, Kusikia mtasikia, wala hamtaelewa; Kutazama mtatazama, wala hamtaona. |
| 15. | Maana mioyo ya watu hawa imekuwa mizito, Na kwa masikio yao hawasikii vema, Na macho yao wameyafumba; Wasije wakaona kwa macho yao, Wakasikia kwa masikio yao, Wakaelewa kwa mioyo yao, Wakaongoka, nikawaponya. |
| 16. | Lakini, heri macho yenu, kwa kuwa yanaona; na masikio yenu, kwa kuwa yanasikia. |
| 17. | Kwa maana, amin, nawaambia, Manabii wengi na wenye haki walitamani kuyaona mnayoyaona ninyi, wasiyaone; na kuyasikia mnayoyasikia ninyi, wasiyasikie. |
| 18. | Basi ninyi sikilizeni mfano wa mpanzi. |
| 19. | Kila mtu alisikiapo neno la ufalme asielewe nalo, huja yule mwovu, akalinyakua lililopandwa moyoni mwake. Huyo ndiye aliyepandwa karibu na njia. |
| 20. | Naye aliyepandwa penye miamba, huyo ndiye alisikiaye lile neno, akalipokea mara kwa furaha; |
| 21. | lakini hana mizizi ndani yake, bali hudumu kwa muda; ikitukia dhiki au udhia kwa ajili ya lile neno, mara huchukizwa. |
| 22. | Naye aliyepandwa penye miiba, huyo ndiye alisikiaye lile neno; na shughuli za dunia, na udanganyifu wa mali hulisonga lile neno; likawa halizai. |
| 23. | Naye aliyepandwa penye udongo mzuri, huyo ndiye alisikiaye lile neno, na kuelewa nalo; yeye ndiye azaaye matunda, huyu mia, na huyu sitini, na huyu thelathini. |
| 24. | Akawatolea mfano mwingine, akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na mtu aliyepanda mbegu njema katika konde lake; |
| 25. | lakini watu walipolala, akaja adui yake akapanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake. |
| 26. | Baadaye majani ya ngano yalipomea na kuzaa, yakaonekana na magugu. |
| 27. | Watumwa wa mwenye nyumba wakaenda wakamwambia, Bwana, hukupanda mbegu njema katika konde lako? Limepata wapi basi magugu? |
| 28. | Akawaambia, Adui ndiye aliyetenda hivi. Watumwa wakamwambia, Basi, wataka twende tukayakusanye? |
| 29. | Akasema, La; msije mkakusanya magugu, na kuzing'oa ngano pamoja nayo. |
| 30. | Viacheni vyote vikue hata wakati wa mavuno; na wakati wa mavuno nitawaambia wavunao, Yakusanyeni kwanza magugu, myafunge matita matita mkayachome; bali ngano ikusanyeni ghalani mwangu. |
| 31. | Akawatolea mfano mwingine, akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na punje ya haradali, aliyoitwaa mtu akaipanda katika shamba lake; |
| 32. | nayo ni ndogo kuliko mbegu zote; lakini ikiisha kumea, huwa kubwa kuliko mboga zote, ikawa mti, hata nyuni wa angani huja na kukaa katika matawi yake. |
| 33. | Akawaambia mfano mwingine; Ufalme wa mbinguni umefanana na chachu aliyoitwaa mwanamke, akaisitiri ndani ya pishi tatu za unga, hata ukachachwa wote pia. |
| 34. | Hayo yote Yesu aliwaambia makutano kwa mifano; wala pasipo mfano hakuwaambia neno; |
| 35. | ili litimie neno lililonenwa na nabii, akisema, Nitafumbua kinywa changu kwa mifano, Nitayatamka yaliyositirika tangu awali. |
| 36. | Kisha Yesu akawaaga makutano, akaingia nyumbani; wanafunzi wake wakamwendea, wakasema, Tufafanulie mfano wa magugu ya kondeni. |
| 37. | Akajibu, akasema, Azipandaye zile mbegu njema ni Mwana wa Adamu; |
| 38. | lile konde ni ulimwengu; zile mbegu njema ni wana wa ufalme; na yale magugu ni wana wa yule mwovu; |
| 39. | yule adui aliyeyapanda ni Ibilisi; mavuno ni mwisho wa dunia; na wale wavunao ni malaika. |
| 40. | Basi, kama vile magugu yakusanywavyo na kuchomwa motoni; ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa dunia. |
| 41. | Mwana wa Adamu atawatuma malaika zake, nao watakusanya kutoka katika ufalme wake machukizo yote, na hao watendao maasi, |
| 42. | na kuwatupa katika tanuru ya moto, ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. |
| 43. | Ndipo wenye haki watakapong'aa kama jua katika ufalme wa Baba yao. Mwenye masikio, na asikie. |
| 44. | Tena ufalme wa mbinguni umefanana na hazina iliyositirika katika shamba; ambayo mtu alipoiona, aliificha; na kwa furaha yake akaenda akauza alivyo navyo vyote, akalinunua shamba lile. |
| 45. | Tena ufalme wa mbinguni umefanana na mfanya biashara, mwenye kutafuta lulu nzuri; |
| 46. | naye alipoona lulu moja ya thamani kubwa, alikwenda akauza alivyo navyo vyote, akainunua. |
| 47. | Tena ufalme wa mbinguni umefanana na juya, lililotupwa baharini, likakusanya samaki wa kila namna; |
| 48. | hata lilipojaa, walilivuta pwani; wakaketi, wakakusanya walio wema vyomboni, bali walio wabaya wakawatupa. |
| 49. | Ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa dunia; malaika watatokea, watawatenga waovu mbali na wenye haki, |
| 50. | na kuwatupa katika tanuru ya moto; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. |
| 51. | Yesu aliwauliza, Mmeyafahamu hayo yote? Wakamwambia, Naam. |
| 52. | Akawaambia, Kwa sababu hiyo, kila mwandishi mwenye elimu ya ufalme wa mbinguni amefanana na mtu mwenye nyumba atoaye katika hazina yake vitu vipya na vya kale. |
| 53. | Ikawa Yesu alipoimaliza mifano hiyo, alitoka akaenda zake. |
| 54. | Na alipofika nchi yake, akawafundisha katika sinagogi lao, hata wakashangaa, wakasema, Huyu amepata wapi hekima hii na miujiza hii? |
| 55. | Huyu si mwana wa seremala? Mamaye si yeye aitwaye Mariamu? Na nduguze si Yakobo, na Yusufu, na Simoni, na Yuda? |
| 56. | Na maumbu yake wote hawapo hapa petu? Basi huyu amepata wapi haya yote? |
| 57. | Wakachukizwa naye. Yesu akawaambia, Nabii hakosi kupata heshima, isipokuwa katika nchi yake, na nyumbani mwake mwenyewe. |
| 58. | Wala hakufanya miujiza mingi huko, kwa sababu ya kutokuamini kwao. |
| ← Matthew (13/28) → |