| ← Matthew (12/28) → |
| 1. | Wakati ule Yesu alipita katika mashamba siku ya sabato; wanafunzi wake wakaona njaa, wakaanza kuvunja masuke, wakala. |
| 2. | Na Mafarisayo walipoona, walimwambia, Tazama! Wanafunzi wako wanafanya neno ambalo si halali kulifanya siku ya sabato. |
| 3. | Akawaambia, Hamkusoma alivyotenda Daudi, alipokuwa na njaa, yeye na wenziwe? |
| 4. | jinsi alivyoingia katika nyumba ya Mungu, akaila mikate ile ya wonyesho, ambayo si halali kwake kuila wala kwa wale wenziwe, ila kwa makuhani peke yao? |
| 5. | Wala hamkusoma katika torati, kwamba siku ya sabato makuhani hekaluni huinajisi sabato wasipate hatia? |
| 6. | Lakini nawaambieni, kwamba hapa yupo aliye mkuu kuliko hekalu. |
| 7. | Lakini kama mngalijua maana yake maneno haya, Nataka rehema, wala si sadaka, msingaliwalaumu wasio na hatia. |
| 8. | Kwa maana Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato. |
| 9. | Akaondoka huko, akaingia katika sinagogi lao. |
| 10. | Na tazama, yumo mtu mwenye mkono umepooza; wakamwuliza, wakisema, Ni halali kuponya watu siku ya sabato? Wapate kumshitaki. |
| 11. | Akawaambia, Ni mtu yupi miongoni mwenu mwenye kondoo mmoja, na yule kondoo ametumbukia shimoni siku ya sabato, asiyemshika akamwopoa? |
| 12. | Je! Mtu ni bora kuliko kondoo mara ngapi? Basi ni halali kutenda mema siku ya sabato. |
| 13. | Kisha akamwambia yule mtu, Nyosha mkono wako; akaunyosha, ukapona, ukawa mzima kama wa pili. |
| 14. | Lakini wale Mafarisayo wakatoka wakafanya shauri juu yake jinsi ya kumwangamiza. |
| 15. | Naye Yesu hali akiyafahamu hayo akaondoka huko; na watu wengi wakamfuata; akawaponya wote, |
| 16. | akawakataza wasimdhihirishe; |
| 17. | ili litimie neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, |
| 18. | Tazama, mtumishi wangu niliyemteua; Mpendwa wangu, moyo wangu uliyependezwa naye; Nitatia roho yangu juu yake, Naye atawatangazia Mataifa hukumu. |
| 19. | Hatateta wala hatapaza sauti yake; Wala mtu hatasikia sauti yake njiani. |
| 20. | Mwanzi uliopondeka hatauvunja, Wala utambi utokao moshi hatauzima, Hata ailetapo hukumu ikashinda. |
| 21. | Na jina lake Mataifa watalitumainia. |
| 22. | Wakati ule akaletewa mtu mwenye pepo, kipofu, naye ni bubu; akamponya, hata yule bubu akanena na kuona. |
| 23. | Makutano wote wakashangaa, wakasema, Huyu siye mwana wa Daudi? |
| 24. | Lakini Mafarisayo waliposikia, walisema, Huyu hatoi pepo, ila kwa Beelzebuli mkuu wa pepo. |
| 25. | Basi Yesu akijua mawazo yao, akawaambia, Kila ufalme ukifitinika juu ya nafsi yake, hufanyika ukiwa; tena mji au nyumba yo yote ikifitinika juu ya nafsi yake, haitasimama. |
| 26. | Na Shetani akimtoa Shetani, amefitinika juu ya nafsi yake; basi ufalme wake utasimamaje? |
| 27. | Na mimi nikitoa pepo kwa Beelzebuli, je! Wana wenu huwatoa kwa nani? Kwa sababu hiyo hao ndio watakaowahukumu. |
| 28. | Lakini mimi nikitoa pepo kwa Roho wa Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia. |
| 29. | Ama awezaje mtu kuingia ndani ya nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuviteka vyombo vyake, asipomfunga kwanza yule mwenye nguvu? Ndipo atakapoiteka nyumba yake. |
| 30. | Mtu asiye pamoja nami yu kinyume changu; na mtu asiyekusanya pamoja nami hutapanya. |
| 31. | Kwa sababu hiyo nawaambia, Kila dhambi na kila neno la kufuru watasamehewa wanadamu, ila kwa kumkufuru Roho hawatasamehewa. |
| 32. | Naye mtu ye yote atakayenena neno juu ya Mwana wa Adamu atasamehewa, bali yeye atakayenena neno juu ya Roho Mtakatifu hatasamehewa katika ulimwengu wa sasa, wala katika ule ujao. |
| 33. | Ufanyeni mti kuwa mzuri na matunda yake kuwa mazuri; au ufanyeni mti kuwa mbaya na matunda yake mabaya, kwa maana kwa matunda yake mti hutambulikana. |
| 34. | Enyi wazao wa nyoka, mwawezaje kunena mema, mkiwa wabaya? Maana, kinywa cha mtu huyanena yaujazayo moyo wake. |
| 35. | Mtu mwema katika akiba njema hutoa mema; na mtu mbaya katika akiba mbaya hutoa mabaya. |
| 36. | Basi, nawaambia, Kila neno lisilo maana, watakalolinena wanadamu, watatoa hesabu ya neno hilo siku ya hukumu. |
| 37. | Kwa kuwa kwa maneno yako utahesabiwa haki, na kwa maneno yako utahukumiwa. |
| 38. | Hapo baadhi ya waandishi na Mafarisayo wakamjibu, wakasema, Mwalimu, twataka kuona ishara kwako. |
| 39. | Akajibu, akawaambia, Kizazi kibaya na cha zinaa chatafuta ishara, wala hakitapewa ishara, ila ishara ya nabii Yona. |
| 40. | Kwani kama vile Yona alivyokuwa siku tatu mchana na usiku katika tumbo la nyangumi, hivyo ndivyo Mwana wa Adamu atakavyokuwa siku tatu mchana na usiku katika moyo wa nchi. |
| 41. | Watu wa Ninawi watasimama siku ya hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki, nao watawahukumu kuwa wamekosa; kwa sababu wao walitubu kwa mahubiri ya Yona; na hapa yupo aliye mkuu kuliko Yona. |
| 42. | Malkia wa kusini atasimama siku ya hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki, naye atawahukumu kuwa wamekosa; kwa sababu yeye alikuja kutoka pande za mwisho za dunia ili asikie hekima ya Sulemani, na hapa yupo aliye mkuu kuliko Sulemani. |
| 43. | Pepo mchafu, amtokapo mtu, hupitia mahali pasipo maji, akitafuta mahali pa kupumzika, asipate. |
| 44. | Halafu husema, Nitarudi nyumbani kwangu nilikotoka; hata akija, aiona tupu, imefagiwa, na kupambwa. |
| 45. | Mara huenda, akachukua pamoja naye pepo wengine saba walio waovu kuliko yeye mwenyewe, nao huingia na kukaa humo; na mtu yule hali yake ya mwisho huwa mbaya kuliko ya kwanza. Ndivyo itakavyokuwa kwa kizazi hiki kilicho kibaya. |
| 46. | Alipokuwa katika kusema na makutano, tazama, mama yake na ndugu zake walikuwa wakisimama nje, wataka kusema naye. |
| 47. | Mtu mmoja akamwambia, Tazama, mama yako na ndugu zako wamesimama nje, wanataka kusema nawe. |
| 48. | Akajibu, akamwambia yule aliyempasha habari, Mama yangu ni nani? Na ndugu zangu ni akina nani? |
| 49. | Akawanyoshea mkono wanafunzi wake, akasema, Tazama, Mama yangu na ndugu zangu! |
| 50. | Kwa maana ye yote atakayeyafanya mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni, huyu ndiye ndugu yangu, na umbu langu, na mama yangu. |
| ← Matthew (12/28) → |