← Matthew (11/28) → |
1. | Ikawa Yesu alipokwisha kuwaagiza wanafunzi wake kumi na wawili, alitoka huko kwenda kufundisha na kuhubiri katika miji yao. |
2. | Naye Yohana aliposikia huko gerezani matendo yake Kristo, alituma wanafunzi wake, kumwuliza, |
3. | Wewe ndiwe yule ajaye, au tumtazamie mwingine? |
4. | Yesu akajibu akawaambia, Nendeni mkamweleze Yohana mnayoyasikia na kuyaona; |
5. | vipofu wanapata kuona, viwete wanakwenda, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, na maskini wanahubiriwa habari njema. |
6. | Naye heri awaye yote asiyechukizwa nami. |
7. | Na hao walipokwenda zao, Yesu alianza kuwaambia makutano habari za Yohana, Mlitoka kwenda nyikani kutazama nini? Unyasi ukitikiswa na upepo? |
8. | Lakini mlitoka kwenda kuona nini? Mtu aliyevikwa mavazi mororo? Tazama, watu wavaao mavazi mororo wamo katika nyumba za wafalme. |
9. | Lakini kwa nini mlitoka? Ni kuona nabii? Naam, nawaambia, na aliye mkuu zaidi ya nabii. |
10. | Huyo ndiye aliyeandikiwa haya, Tazama, mimi namtuma mjumbe wangu Mbele ya uso wako, Atakayeitengeneza njia yako mbele yako. |
11. | Amin, nawaambieni, Hajaondokea mtu katika wazao wa wanawake aliye mkuu kuliko Yohana Mbatizaji; walakini aliye mdogo katika ufalme wa mbinguni ni mkuu kuliko yeye. |
12. | Tangu siku za Yohana Mbatizaji hata sasa ufalme wa mbinguni hupatikana kwa nguvu, nao wenye nguvu wauteka. |
13. | Kwa maana manabii wote na torati walitabiri mpaka wakati wa Yohana. |
14. | Na ikiwa mnataka kukubali, yeye ndiye Eliya atakayekuja. |
15. | Mwenye masikio, na asikie. |
16. | Lakini nitakifananisha na nini kizazi hiki? Kimefanana na watoto wanaokaa sokoni, wanaowaita wenzao, wakisema, |
17. | Tuliwapigia filimbi, wala hamkucheza; tuliomboleza, wala hamkulia. |
18. | Maana Yohana alikuja, hali wala hanywi, wakasema, Yuna pepo. |
19. | Mwana wa Adamu alikuja, akila na kunywa, wakasema, Mlafi huyu, na mlevi, rafiki yao watoza ushuru na wenye dhambi! Na hekima imejulikana kuwa ina haki kwa kazi zake. |
20. | Ndipo akaanza kuikemea miji ile ambamo ndani yake ilifanyika miujiza yake iliyo mingi, kwa sababu haikutubu. |
21. | Ole wako, Korazini! Ole wako, Bethsaida! Kwa kuwa kama miujiza iliyofanyika kwenu ingalifanyika katika Tiro na Sidoni, wangalitubu zamani kwa kuvaa magunia na majivu. |
22. | Walakini nawaambieni, itakuwa rahisi Tiro na Sidoni kustahimili adhabu zao siku ya hukumu kuliko ninyi. |
23. | Nawe Kapernaumu, je! Utakuzwa mpaka mbinguni? Utashushwa mpaka kuzimu; kwa kuwa kama miujiza iliyofanyika kwako ingalifanyika katika Sodoma, ungalikuwapo mji huo hata leo. |
24. | Walakini nawaambieni, itakuwa rahisi nchi ya Sodoma kustahimili adhabu yake siku ya hukumu kuliko wewe. |
25. | Wakati ule Yesu akajibu, akasema, Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga. |
26. | Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyopendeza mbele zako. |
27. | Akasema, Nimekabidhiwa vyote na baba yangu; wala hakuna amjuaye Mwana, ila Baba; wala hakuna amjuaye Baba, ila Mwana, na ye yote ambaye Mwana apenda kumfunulia. |
28. | Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. |
29. | Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu; |
30. | kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi. |
← Matthew (11/28) → |