| ← Mark (9/16) → |
| 1. | Akawaambia, Amin, nawaambia, Pana watu katika hawa wasimamao hapa, ambao hawataonja mauti kabisa, hata watakapouona ufalme wa Mungu umekuja kwa nguvu. |
| 2. | Hata baada ya siku sita Yesu akawatwaa Petro, na Yakobo, na Yohana, akawaleta juu ya mlima mrefu faraghani, peke yao; akageuka sura yake mbele yao; |
| 3. | mavazi yake yakimeta-meta, meupe mno, jinsi asivyoweza dobi duniani kuyafanya meupe. |
| 4. | Wakatokewa na Eliya pamoja na Musa, nao walikuwa wakizungumza na Yesu. |
| 5. | Petro akajibu, akamwambia Yesu, Rabi, ni vizuri sisi kuwapo hapa; na tufanye vibanda vitatu, kimoja chako wewe, kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya. |
| 6. | Maana, hakujua la kunena, kwa kuwa waliingiwa na hofu nyingi. |
| 7. | Kisha likatokea wingu, likawatia uvuli; sauti ikatoka katika lile wingu, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, msikieni yeye. |
| 8. | Mara hiyo walipotazama huku na huku, hawakuona mtu pamoja nao ila Yesu peke yake. |
| 9. | Na walipokuwa wakishuka mlimani aliwakataza wasimweleze mtu waliyoyaona, hata Mwana wa Adamu atakapokuwa amefufuka katika wafu. |
| 10. | Wakalishika neno lile, wakiulizana wao kwa wao, Huko kufufuka katika wafu maana yake nini? |
| 11. | Wakamwuliza, wakisema, Mbona waandishi hunena ya kwamba imempasa Eliya kuja kwanza? |
| 12. | Akajibu akawaambia, Ni kweli Eliya yuaja kwanza, na kurejeza upya yote; lakini, pamoja na haya, ameandikiwaje Mwana wa Adamu ya kwamba atateswa mengi na kudharauliwa? |
| 13. | Lakini nawaambia, Eliya amekwisha kuja, nao wakamtenda yote waliyoyataka kama alivyoandikiwa. |
| 14. | Hata walipowafikia wanafunzi, waliona mkutano mkuu wakiwazunguka, na waandishi wakijadiliana nao; |
| 15. | mara mkutano wote walipomwona walishangaa, wakamwendea mbio, wakamsalimu. |
| 16. | Akawauliza, Mnajadiliana nini nao? |
| 17. | Mtu mmoja katika mkutano akamjibu, Mwalimu, nimemleta mwanangu kwako, ana pepo bubu; |
| 18. | na kila ampagaapo, humbwaga chini, naye hutoka povu na kusaga meno na kukonda; nikasema na wanafunzi wako wamtoe pepo, wasiweze. |
| 19. | Akawajibu, akasema, Enyi kizazi kisichoamini, nikae nanyi hata lini? Nichukuliane nanyi hata lini? Mleteni kwangu. |
| 20. | Wakamleta kwake; hata alipomwona, mara yule pepo alimtia kifafa; naye akaanguka chini, akagaa-gaa, akitokwa na povu. |
| 21. | Akamwuliza babaye, Amepatwa na haya tangu lini? Akasema, Tangu utoto. |
| 22. | Na mara nyingi amemtupa katika moto, na katika maji, amwangamize; lakini ukiweza neno lo lote, utuhurumie, na kutusaidia. |
| 23. | Yesu akamwambia, Ukiweza! Yote yawezekana kwake aaminiye. |
| 24. | Mara babaye yule kijana akapaza sauti, akasema, Naamini, nisaidie kutokuamini kwangu. |
| 25. | Naye Yesu akiona ya kuwa mkutano unakusanyika mbio, akamkemea yule pepo mchafu, akamwambia, Ewe pepo bubu na kiziwi, mimi nakuamuru, mtoke huyu, wala usimwingie tena. |
| 26. | Akalia, akamtia kifafa sana, akamtoka; naye akawa kama amekufa; hata wengi wakasema, Amekufa. |
| 27. | Lakini Yesu akamshika mkono akamwinua naye akasimama. |
| 28. | Hata alipoingia nyumbani, wanafunzi wake wakamwuliza kwa faragha, Mbona sisi hatukuweza kumtoa? |
| 29. | Akawaambia, Namna hii haiwezi kutoka kwa neno lo lote, isipokuwa kwa kuomba. |
| 30. | Wakatoka huko, wakapita katikati ya Galilaya; naye hakutaka mtu kujua. |
| 31. | Kwa sababu alikuwa akiwafundisha wanafunzi wake, akawaambia, Mwana wa Adamu yuaenda kutiwa katika mikono ya watu, nao watamwua; hata akiisha kuuawa, baada ya siku tatu atafufuka. |
| 32. | Lakini hawakulifahamu neno lile, wakaogopa kumwuliza. |
| 33. | Wakafika Kapernaumu; hata alipokuwamo nyumbani, akawauliza, Mlishindania nini njiani? |
| 34. | Wakanyamaza; kwa maana njiani walikuwa wakibishana wao kwa wao, ni nani aliye mkubwa. |
| 35. | Akaketi chini, akawaita wale Thenashara akawaambia, Mtu atakaye kuwa wa kwanza atakuwa wa mwisho kuliko wote, na mtumishi wa wote. |
| 36. | Akatwaa kitoto, akamweka katikati yao, akamkumbatia, akawaambia, |
| 37. | Mtu akimpokea mtoto mmoja wa namna hii kwa jina langu, anipokea mimi; na mtu akinipokea mimi, humpokea, si mimi, bali yeye aliyenituma. |
| 38. | Yohana akamjibu, akamwambia, Mwalimu, tulimwona mtu akitoa pepo kwa jina lako, ambaye hafuatani nasi; tukamkataza, kwa sababu hafuatani nasi. |
| 39. | Yesu akasema, Msimkataze, kwa kuwa hakuna mtu atakayefanya mwujiza kwa jina langu akaweza mara kuninenea mabaya; |
| 40. | kwa sababu asiye kinyume chetu, yu upande wetu. |
| 41. | Kwa kuwa ye yote atakayewanywesha ninyi kikombe cha maji, kwa kuwa ninyi ni watu wa Kristo, amin, nawaambia, hatakosa thawabu yake. |
| 42. | Na ye yote atakayemkosesha mmojawapo wa wadogo hawa waniaminio, afadhali afungiwe jiwe la kusagia shingoni mwake, na kutupwa baharini. |
| 43. | Na mkono wako ukikukosesha, ukate; ni afadhali kuingia katika uzima u kigutu, kuliko kuwa na mikono miwili, na kwenda zako jehanum, kwenye moto usiozimika; |
| 44. | ambamo humo funza wao hafi, wala moto hauzimiki.] |
| 45. | Na mguu wako ukikukosesha, ukate; ni afadhali kuingia katika uzima, u kiwete, kuliko kuwa na miguu miwili, na kutupwa katika jehanum; [ |
| 46. | ambamo humo funza wao hafi, wala moto hauzimiki.] |
| 47. | Na jicho lako likikukosesha, ling'oe, ulitupe; ni afadhali kuingia katika ufalme wa Mungu, una chongo, kuliko kuwa na macho mawili, na kutupwa katika jehanum; |
| 48. | ambamo humo funza wao hafi, wala moto hauzimiki. |
| 49. | Kwa sababu kila mtu atatiwa chumvi kwa moto. |
| 50. | Chumvi ni njema; lakini chumvi ikiwa si chumvi tena, mtaitia nini ikolee? Mwe na chumvi ndani yenu, mkakae kwa amani ninyi kwa ninyi. |
| ← Mark (9/16) → |